Papa amemteua Mons.Ruben Dario kuwa Balozi wa Vatican nchini Benin&Togo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatatu tarehe 28 Oktoba 2024 Baba Mtakatifu amemteua Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo, Mons Rubén Darío Ruiz Mainardi, ambaye hadi uteuzi alikuwa ni mshauri wa Ubalozi kwa kumwinua wakati huohu kuwa na makao ya Ursona na hadhi ya Uaskofu Mkuu.
Wasifu wake
Mons. Rubén Darío Ruiz Mainardi huko Córdoba nchini Argentina, tarehe 17 Novemba 1964. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 26 Mei 1991 kwa ajili ya Jimbo la Mtakatifu Tomé. Alipata leseni katika Taalimungu ya Kidogma na Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanoni.
Baada ya kuingia katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican tarehe 1 Machi 2000, alifanya kazi kama mwakilishi wa Kipapa katika Jamhuri ya Congo na Gabon, Slovenia na Macedonia, Uswiss na Liechtenstein, Cuba, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad, Ufaransa na hivi karibuni amekuwa katika huduma kwenye Sehemu ya Masuala ya Jumla ya Sekretarieti ya Vatican. Anajua Kifaransa, Kiingereza, Kiitaliano na Kireno.