Uzinduzi wa Picha mpya ya Mama Yetu wa Amani ya Korea katika Bustani za Vatican
Vatican News
Ijumaa tarehe 20 Septemba 2024, ikiwa Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Watakatifu Andrew Kim Taegon, Paul Chong Hasang na mashahidi wenzake (Wakorea), uzinduzi wa picha ya Kikorea ya ‘Mama wa Amani’ ulifanyika saa 10.00 jioni maasa ya Ulaya katika bustani za Vatican, mbele ya Kardinali Fernando Vérgez Alzaga L.C., Gavana wa mji wa Vatican, Kardinali Lazzaro You Heung sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri, Baraza la Maaskofu wa Korea, ambao wako katika ziara ya kitume ad limina, jijini Roma. Kwa njia hiyo pia walikuwepo watu wapatao 200 wakiwemo waamini walei, watawa na mapdre. Ibada ya kubariki ilifuatiwa na sala ya Rozari kwa nia ya Baba Mtakatifu, hasa kuomba, kwa umoja na Papa, zawadi ya amani.
Mnamo Mei 2023, Kardinali Lazzaro You alimwagiza msanii wa Korea Shim Soonhwa Catherine kuunda picha ya “Mama Yetu wa Amani” kwa ajili ya Bustani za Vatican. Msanii huyo alifichua kuwa Kardinali huyo alimweleza kuwa amepata kibali cha Papa Francisko kupitia kwa Gavana wa mji wa Vatican na kumwalika kutembelea bustani ya Vatican kwa ajili ya ukaguzi na kubaini vipimo vya kazi hiyo. Shim Soonhwa alianza kuchora picha kwenye turubai tangia Oktoba iliyopita na,baada ya kumaliza, aliunda mosaic.
Turubai lina urefu wa 160sentimita na upana wa 105se, iliyopakwa rangi ya akriliki, wakati mosaic ina urefu wa 150cm na upana wa 100cm, ikijumuisha ukingo wa marumaru, kwa jumla ya ukubwa wa 186cm na upana wa 130cm. Turubai ilitolewa na kuoneshwa katika makao makuu ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, huko Uwanja Pio XII, 3. Kuna kipande cha glasi cha 0.6cm kwenye mosaic ili kuondoa mng'ao wa glasi na kutoa hisia laini. Mosaic ilitolewa nchini Korea na kusafirishwa kwa ndege, wakati ukingo wa marumaru ulifanyiwa nchini Italia, huko Carrara.
Sanamu ya "Mama Yetu wa Amani" imevaa hanbok, yaani vazi la kiutamaduni la Kikorea,na ina rangi nyekundu na kijani, ambapo nyekundu inawakilisha amani ya akina mama na turquoise. Katika kazi hiyo, Mama Yetu, akiwa ameshikilia taji la rozari mkononi mwake, anakanyaga nyoka, ambayo ni ishara ya uovu, wakati taji linaashiria silaha ya maombi ya kushinda uovu. Kazi hiyo pia inaonesha baraka ya Mtoto Yesu, akiwa ameshikilia ulimwengu mkononi mwake.
Nguo ambazo Mtoto Yesu amevaa ni zile za kiutamaduni za Kikorea zinazovaliwa na watoto wadogo na kwa kuwa ni za thamani, lazima zilindwe kila wakati na kuoneshwa kwa mavazi ya rangi ya tabia ya watu wa Kikorea. Mwandishi alionesha Bikira Maria akiwa amesimama na Mtoto Yesu mikononi mwake, akionesha matumaini kwamba dunia iliyotiwa giza, hasa vita inaweza kupata maelewano na amani tena kupitia maombezi yenye nguvu ya Malkia wa Amani na kufanya enzi mpya na kustawi kwa ubinadamu wote. Picha hiyo pia inaonesha njiwa, ishara ya Roho Mtakatifu, pamoja na tawi la mzeituni. Asili ni ya manjano, dhahabu kwa sababu rangi ni ishara ya utukufu na ufalme wa Mungu na nuru. Picha hii ya Maria ni uwakilishi wa kumi na mbili wa Bikira Maria aliyepo katika bustani za Vatican kati ya kazi nyingine kutoka kila kona ya sayari.