ĐÓMAPµĽş˝

, Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", inatoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani tarehe 23 Julai 2023. , Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", inatoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani tarehe 23 Julai 2023.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee 2023: Rehema Kamili 23 Julai 2023

Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne, asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema kamili. Rehema Kamili 23 Julai 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa Katoliki yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa. Huu ni msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne, asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema kamili.

Rehema kamili kutolewa siku ya wazee duniani 23 Julai 2023
Rehema kamili kutolewa siku ya wazee duniani 23 Julai 2023   (Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", inatoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Waamini waliojiandaa kikamilifu kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa ili kujipatia rehema kamili, watapata. Ikiwa kama watawatembelea na kuwahudumia wazee wanaohitaji zaidi msaada au wenye ulemavu. Wanaweza kuwatembelea na kuonana nao mubashara au kuwasaidia kwa njia ya mitandao ya kijamii. Wazee, wagonjwa na walemavu wanaweza kujipatia rehema kamili ikiwa kama kutoka katika undani wa nyoyo zao, wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya maadhimisho haya.

Waamini wafuate mashari ya kupata rehema kamili.
Waamini wafuate mashari ya kupata rehema kamili.   (Vatican Media)

Wazee, wagonjwa na walemavu wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anapenda kutumia fursa hii kutoa mwaliko kwa Mapadre waliopewa dhamana ya kuungamisha waamini, kutekeleza dhamana na wajibu huu, pamoja na uwepo na utayari wao wa kusikiliza maungamo kama kielelezo cha upendo wa shughuli za kichungaji. Tamko hili ni halali tu, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Mwaka 2023. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 23 Julai 2023. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao!

Rehema kamili
21 Julai 2023, 13:17