Wito wa Papa kwa Sudan ili kusitisha janga la kibinadamu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Akiwageugia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 3 Septemba 2025 kwa ajili ya Katekesi yake, katika salamu zake kwa lugha mbali mbali alitoa wito kwa ajili ya nchi ya Sudan iliyogubikwa na matatizo mengi sana. Papa alisema “ kwa namna ya pekee huko Darfur zinafika habari za kutisha. Huko El Fasher, idadi kubwa ya raia. Raia wengi wamekwama katika jiji hilo, waathiriwa wa njaa na ghasia. Huko Tarasin, maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vingi, na kuacha nyuma maumivu na kukata tamaa. Na, kama hiyo haitoshi, kuenea kwa kipindupindu kunatishia mamia ya maelfu ya watu ambao tayari wamechoka.”
Kwa njia hiyo Papa ameonesha kuwa “karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote na watu wa Sudan, hasa familia zao, watoto, na watu waliokimbia makazi yao.” Amsisitiza uhakika wa maombi kwamba “ Nawaombea wahanga wote.” Kutokana na hili Papa ametoa wito kwamba “Ninatoa wito wa dhati kwa wale wanaohusika na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa kuna maeneo ya misaada ya kibinadamu na kutekeleza jibu lililoratibiwa ili kukomesha janga hili la kibinadamu. Umefika wakati wa kuanzisha mazungumzo mazito, ya dhati na ya kujumuisha pande zote ili kumaliza mzozo huo na kurejesha matumaini, utu na amani kwa watu wa Sudan.”