Papa aelezea masikitiko kuhusu maporomoko ya ardhi yaliyoua zaidi ya watu elfu huko Darfur
Vatican News
Baba Mtakaifu Leo XIV , tarehe 2 Septemba 2025 alielezea huzuni, ukaribu na maombi kwa kuwahakikishia wale wote walioathiriwa na maporomoko ya ardhi yaliyokikumba kijiji cha Tarasin, katika eneo la Darfur ya Kati nchini Sudan. Katika barua iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin na kuelekezwa kwa Askofu Askofu Yunan Tombe Trille Kuku Andali, wa Jimbo la El Obeid, Papa "anawahakikishia wale wote walioguswa na janga hili ukaribu wake wa kiroho. Akiombea hasa pumziko la milele la marehemu, kwa wale wanaoomboleza kupoteza wapendwa wao, na kwa watu wengi ambao bado wanakosa katika harakati za uokoaji wa dharura, kupitia wafanyakazi katika juhudi zao zinazoendelea za kutoa misaada." Papa alihitimisha ujumbe wake kwa kuomba faraja na baraka za kimungu kwa nchi.”
Maporomoko ya ardhi
Kuna mtu mmoja tu aliyenusurika, kwa mujibu wa kundi la waasi linalodhibiti eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan, ambako maporomoko makubwa ya ardhi yalitokea Septemba Mosi, 2025 jioni, na kuua zaidi ya watu elfu moja na kuharibu sehemu ya eneo linalojulikana kwa uzalishaji wake wa machungwa.
"Janga la kibinadamu kwa nchi nzima"
Gavana wa Darfur Minni Minnawi, akishirikiana na jeshi, alitaja maporomoko hayo kuwa "janga la kibinadamu linalovuka mipaka ya eneo hilo" na kutoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya kibinadamu "kuingilia kati haraka na kutoa msaada na usaidizi katika wakati huu muhimu, kwani janga hilo ni zaidi ya watu wetu wanaweza kustahimili."
Vita Vilivyosahaulika nchini Sudan
Sehemu kubwa ya Darfur bado haiwezi kufikiwa na Mashirikia yasiyo ya kiserikali(NGOs), ikiwa ni pamoja na eneo lililoathiriwa na maporomoko ya ardhi, kutokana na mapigano ambayo yanazuia kwa kiasi kikubwa utoaji wa misaada ya kibinadamu. Vita nchini Sudan vilianza tangu Aprili 2023 na hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na kuwakimbia takriban watu milioni 13. Majuma mawili yaliyopita Umoja wa Mataifa (UN) uliripoti kuwa makumi ya watu wanakufa kila Juma kutokana na njaa na utapiamlo katika kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk.