Papa kuhusu shambulio la Israel dhidi ya Hamas nchini Qatar:"Hali ni mbaya sana"
Vatican News
Papa Leo XIV alizungumzia "habari nzito kweli," akimaanisha mashambulizi ya Israel dhidi ya viongozi kadhaa wa Hamas huko Doha, Qatar. Shambulio hilo lilipiga majengo kadhaa ya makazi katika mji mkuu. Papa alihojiwa na vyombo vya habari Jumanne tarehe 9 Septemba 2025, nje ya Eneo la Villa Barberini, makazi yake huko Castel Gandolfo, ambapo aliamua kutumia chini ya siku moja, kuanzia jana jioni tarehe 8 Septemba hadi mchana wa Jumanne Septemba 9, 2025.
Kuomba kwa Bidii na Kufanya Kazi kwa ajili ya Amani
Alisimama kwa muda mfupi na waandishi wa habari mbele ya lango kuu, huku msururu mrefu wa watu ukimpigia makofi na kuimba jina lake, ambapo Papa Leo XIV, akijibu maswali kwenye waandishi wa Runinga ya Italia ( Rai News,) alionesha wasiwasi wake kwa kile kinachotokea Mashariki ya Kati: "Hali nzima ni mbaya sana," alisema. "Hatujui mambo yanakwenda wapi; siku zote ni mbaya. Ni lazima tuombe kwa bidii na kuendelea kufanya kazi, kutafuta na kusisitiza amani."
Agizo la Uokoaji huko Gaza
Kuhusu agizo la Israel la kuhama mara moja kwa wakazi wa Mji wa Gaza kwa kutarajia kuongezeka kwa operesheni za kijeshi, Papa alieleza kuwa alijaribu kuwasiliana na Paroko wa Familia Takatifu, Padre Gabriel Romanelli. "Nilijaribu kumpigia simu Padre wa parokia sasa, lakini sina habari," alisema. "Kwa hakika walikuwa sawa, lakini baada ya utaratibu huu mpya, sina uhakika."
Kurudi Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kisha alisalimiana na baadhi ya waamini waliokuwepo kabla ya kurejea Mjini Vatican. Alifika Castel Gandolfo jana jioni tarehe 8 Septemba na alitumia asubuhi na alasiri huko, na kutekeleza majukumu yake ya siku ambayo hakuna vikao vilivyopangwa.