Papa Leo XIV: Siku ya Vijana Ulimwenguni 3 hadi 8 Agosti 2027 Jimbo Kuu la Seoul
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 3 Agosti 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana na kuhudhuriwa na: Vijana zaidi ya milioni moja kutoka katika nchi 146; Mapadre 7,000 na Maaskofu ni 450, na wadau wa tasnia ya mawasiliano walikuwa ni 850, matendo makuu ya Mungu. Baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Vijana mahujaji wa matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV ametangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Corea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yatanogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya nyoyo za waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini hadi miisho ya dunia. Amewakaribisha vijana wengi zaidi huko Seoul, Corea ya Kusini, ili kwa pamoja waweze kuendeleza ndoto na matumaini.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha vijana kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni sadaka ya upendo kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake, mwaliko kwa vijana kufuata ile hija ya Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Wakampokea na kumkaribisha kama mwandani wa safari ya maisha yao. Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha kikatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumainia kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Rej Lk 24:13-35.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 3 Agosti 2025 kwenye Uwanja wa Tor Vergata, Roma, amesema, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, vijana wanayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana, kwani kwa hakika limekuwa ni tukio la neema na baraka. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea Marehemu Maria Cobo Vergara aliyekuwa na umri wa miaka 20 kutoka Hispania aliyefariki dunia tarehe 30 Julai 2025 pamoja na Pascale Rafic kutoka Misri aliyefariki dunia Ijumaa tarehe 1 Agosti 2025. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza: Maaskofu, walezi na waalimu pamoja na wale wote walioandaa na hatimaye, kufanikisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa vijana, bila kuwasahau wale wote walioshiriki kiroho katika maadhimisho ya Jubilei hii. Baba Mtakatifu amewakumbuka pia vijana kutoka Ukraine na Ukanda wa Gaza, alama na ushuhuda kwamba, amani ya kweli inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi ni msingi wa amani ya kudumu. Baba Mtakatifu amewasihi vijana wa kizazi kipya waliohudhuria maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo, kuwafikishia vijana wengine salam zake na matashi mema. Kuna sehemu ambazo vijana hawakuweza kushiriki kwa sababu zinazoeleweka. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya vijana kupeleka furaha, ari na moyo mkuu sehemu mbalimbali za dunia, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Huu ni ujumbe mahususi wa matumaini kwa vijana waliopondeka moyo na kukata tamaa katika maisha yao!