杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV: Yesu,kwa ishara ya mkate,anaonesha kuwa kila usaliti unaweza kuwa fursa ya wokovu!

Kupenda hadi mwisho:huu ndio ufunguo wa kuelewa moyo wa Kristo.Upendo ambao hauishii mbele ya kukataliwa,kukatishwa tamaa au hata kukosa shukrani.Upendo wa Yesu haukatai ukweli wa maumivu,lakini hauruhusu uovu kuwa na neno la mwisho.Hili ndilo fumbo ambalo Yesu anafanya kwa ajili yetu,ambalo sisi pia,wakati fulani,tunaitwa kushiriki.Ni katika Tafakari ya Papa Leo wakati wa Katekesi yake,Jumatano 20 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV  aliongoza na kifungu cha Pasaka ya Yesu: Msamaha: Mungu aliwapenda hadi mwisho (Yh 13,2) katika muktadha  wa Mzunguko Katekesi kuhusu Jubilei ya Matumaini 2025: Yesu Kristo ni Tumaini letu” kwa kuwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican,  Jumatano tarehe 20 Agosti 2025, na wakati kikundi kingine kikiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro wakifuatilia katika Skrini na kwenye uwanja nje ya Ukumbi. Kwa njia hiyo  Papa Leo akianza alisema:  “Leo tunaakisi moja ya ishara za kushtua na zenye kung'aa zaidi katika Injili: wakati ambapo Yesu, akiwa Karamu ya Mwisho, anapotoa kipande cha chakula kwa yule anayekaribia kumsaliti. Sio tu ishara ya kushiriki; ni zaidi: ni jaribio la mwisho la upendo wa kutokata tamaa. Mtakatifu Yohane, kwa usikivu wake wa kina wa kiroho, anaelezea wakati huo kwa ajili yetu hivi: "Wakati wa chakula cha jioni, wakati Ibilisi amekwisha kuweka ndani ya moyo wa Yuda, Iskariote, mwana wa Simoni, ili kumsaliti […] Yesu, akijua kwamba saa yake imefika […] Kupenda hadi mwisho: huu ndio ufunguo wa kuelewa moyo wa Kristo. Upendo ambao hauishii mbele ya kukataliwa, kukatishwa tamaa, au hata kukosa shukrani.

Katekesi ya  Papa 20 Agosti 2025
Katekesi ya Papa 20 Agosti 2025   (@Vatican Media)

Yesu anajua saa, lakini haivumilii: anaichagua. Ni yeye anayetambua wakati ambapo upendo wake unapaswa kuvumilia jeraha lenye uchungu zaidi, lile la usaliti. Na badala ya kujiudhulu, kushutumu, kujitetea ... anaendelea kupenda: anawaosha miguu, anachovya mkate ndani na kuutoa. “Nitakayechovya tonge na kumpatia ndiye”(Yh 13:26). Kwa ishara hii rahisi na ya unyenyekevu, Yesu anaupeleka upendo wake mbele na kuutia ndani zaidi. Sio kwa sababu hajui kinachotokea, lakini kwa sababu anaona wazi. Ni uwezo wa kuwaacha wengine huru, huku akiwapenda hadi mwisho. Upendo wa Yesu haukatai ukweli wa maumivu, lakini hauruhusu uovu kuwa na neno la mwisho. Hili ndilo fumbo ambalo Yesu anafanya kwa ajili yetu, ambalo sisi pia, wakati fulani, tunaitwa kushiriki. Mahusiano mangapi yanavunjika, ni historia ngapi zinakuwa ngumu, ni maneno mangapi ambayo hayajasemwa ambayo hayatasemwa. Hata hivyo, Injili inatuonesha kwamba siku zote kuna njia ya kuendelea kupendana, hata wakati kila kitu kinaonekana kuwa na matatizo yasiyoweza kurekebishwa.

Katekesi ya Papa 20 Agosti 2025
Katekesi ya Papa 20 Agosti 2025   (@Vatican Media)

Kusamehe haimaanishi kukataa maovu, bali kuyazuia yasitokee maovu zaidi tena. Haisemekani  kwamba hakuna kilichotokea,hapana bali, kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa chuki haiamui wakati ujao. Wakati Yuda anatoka chumbani, “ilikuwa usiku” (Yh 13, 30). Lakini mara baada ya hapo, Yesu anasema: “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa” (Yh 13, 31). Usiku bado upo, lakini nuru tayari imeanza kuangaza. Na inang'aa kwa sababu Kristo anabaki mwaminifu hadi mwisho, na hivyo upendo wake una nguvu zaidi kuliko chuki. Baba Mtakatifu ameendelea kukazia kuwa “ hata , sisi pia hupitia usiku wenye uchungu na wenye kuchosha. Usiku wa roho, usiku wa kukata tamaa, usiku wakati mtu ametuumiza au ametusaliti. Katika nyakati hizo, jaribu ni kujifungia, kujilinda, na kurudisha nyuma. Lakini Bwana anatuonesha kwamba tumaini lipo; daima kuna njia nyingine. Anatufundisha kwamba tunaweza kutoa tonge hata kwa wale wanaotupa kisogo. Na kwamba tunaweza kujibu kwa ukimya wa uaminifu. Na kwamba tunaweza kusonga mbele kwa heshima, bila kuacha upendo.

Katekesi  ya Papa Agosti 2025
Katekesi ya Papa Agosti 2025   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV alishauri kwamba: “Leo hii tuombe neema ya kujua jinsi ya kusamehe, hata pale tunapohisi hatuelewi, hata tunapohisi kuachwa. Kwa sababu ni katika masaa hayo ambayo upendo unaweza kufikia kilele chake. Yesu anavyotufundisha, kupenda kunamaanisha kuwaacha wengine huru, hata kwa kusalitiwa, bila kuacha kuamini kwamba hata uhuru huo, uliojeruhiwa na kupotea, unaweza kung’olewa kutoka katika udanganyifu wa giza na kurejeshwa kwenye nuru ya wema. Wakati mwanga wa msamaha unaweza kuchuja kupitia nyufa za ndani kabisa za moyo, tunaelewa kuwa sio bure. Hata kama mwingine hakukubali, hata kama inaonekana bure, msamaha huweka huru yule anayeutoa: huondoa chuki, hurejesha amani, na huturudisha sisi wenyewe ndani. Kwa kuhitimisha Papa Leo wa XIV alisisitiza kwamba “Yesu, kwa ishara rahisi ya kutoa mkate, anaonesha kwamba kila usaliti unaweza kuwa fursa ya wokovu, ikiwa utachaguliwa kama nafasi ya upendo mkuu. Yeye hakubali maovu, bali huyashinda kwa mema, na kuyazuia kuzima yale yaliyo kweli zaidi ndani yetu ya: uwezo wa kupenda.” Papa Leo XIV alihitimisha Katekesi yake.


Katekesi ya Papa 20 Agosti 2025
20 Agosti 2025, 12:07