Papa Leo XIV huko Torvergata na vijana:Ujasiri wa kuchagua unatokana na upendo!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ni jinsi gani hisia nzuri ya kusisimua, kuona Uwanja Mkubwa wa Tor Vergata, jijini Roma ambao tangu asubuhi umewaona wasanii wa muziki wakitumbuiza vijana hadi kufika kwa Baba Mtakatifu usiku kwenye mkesha wa tarehe 2 Agosti 2025 katika tukio la Jubilei ya vijana katika Mwaka Mtakatifu 2025. Uwanja ulipambwa na vijana kutoka duniani kote wakiwa na bendera na zana mbali mbali zinazoelezea utamaduni wa kila taifa. Kwa njia hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV alifika katika Uwanja huo kwa kupokelewa na wawakilishi vijana huku wakiongozana naye akiwa ameshika Msalaba wa Jubilei hadi altareni, lakini baada ya kuzunguka na kigari chake katika uwanja mzima akiwabariki vijana. Uwanja huo ni wa kihistoria ambao ulifunguliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, wakati wa ufunguzi wa Milenia mpya mwaka 2000. Mkesha huo ulianza na maswali matatu kutoka kwa vijana watatu: kwa lugha ya kihispania, kiingereza na kiitaliano. Idhaa ya kiswahili inakuletea maswali na majibu hayo kamili.
Swali la I: Urafiki
Baba Mtakatifu, sisi ni watoto wa wakati wetu. Tunaishi katika utamaduni ambao ni wetu na, bila sisi kutambua, hutuunda; ni alama na teknolojia, hasa katika nyanja ya mitandao ya kijamii. Mara nyingi tunajidanganya kwa kufikiri tuna marafiki wengi na tunaunda vifungo vya mahusiano vya ukaribu, huku tukizidi kupata aina nyingi za upweke. Tuko karibu na tumeunganishwa na watu wengi, lakini vifungo vya mahusiano haya si vya kweli na vya kudumu, bali vya muda mfupi na mara nyingi ni vya udanganyifu.
Baba Mtakatifu, hapa kuna swali langu: tunawezaje kupata urafiki wa dhati na upendo wa kweli unaotufungua katika matumaini ya kweli? Imani inaweza kutusaidiaje kujenga wakati wetu ujao?
Jibu la Papa: Vijana wapendwa, mahusiano na watu wengine ni muhimu kwa kila mmoja wetu, kuanzia na ukweli kwamba wanaume na wanawake wote duniani wanazaliwa kama watoto wa mtu. Maisha yetu huanza shukrani ya mahusiano, na ni kupitia vifungo vya mahusiano tunakua. Katika mchakato huo, utamaduni una jukumu la msingi: ni kanuni ambayo tunajitafsiri wenyewe na ulimwengu. Kama kamusi, kila utamaduni una maneno matukufu na pia machafu, maadili na makosa, ambayo ni lazima tujifunze kuyatambua. Kwa kutafuta ukweli kwa shauku, hatupokei utamaduni tu, lakini tunaubadilisha kupitia chaguzi za maisha. Kiukweli ukweli, ni kifungo kinachounganisha maneno kwa vitu, na majina kwa nyuso.
Uongo, hata hivyo, hutenganisha vipengele hivi, na kuleta mkanganyiko na kutokuelewana. Miongoni mwa miunganisho mingi ya kiutamaduni ambayo ina sifa ya maisha yetu, mtandao na vyombo vya habari vimekuwa "fursa ya ajabu ya mazungumzo, kukutana, na kubadilishana kati ya watu, na vile vile kupata habari na maarifa" (Papa Francisko, Christus Vivit, 87). Zana hizi, hata hivyo, huwa na utata zinapotawaliwa na mantiki ya kibiashara na maslahi ambayo huvuruga uhusiano wetu. Katika suala hili, Papa Francisko alikumbusha kwamba wakati mwingine "taratibu za mawasiliano, matangazo, na mitandao ya kijamii inaweza kutumika kutufanya tupate usingizi, na matumizi ya dawa za kulevya" (Christus Vivit, 105). Kwa hiyo uhusiano wetu huchanganyikiwa, husimamishwa, au kutokuwa thabiti. Wakati chombo kinapomtawala mwanadamu, mwanadamu anakuwa chombo: ndiyo, chombo cha soko, bidhaa kwa haki yake mwenyewe. Ni mahusiano ya dhati tu na vifungo vya mahusiano thabiti huendeleza historia za maisha mazuri
Wapendwa, kwa asili kila mtu anatamani maisha haya mazuri, kwani mapafu yanatamani hewa, lakini ni vigumu sana kuipata! Karne nyingi zilizopita, Mtakatifu Agostino alipata shauku kubwa ya mioyo yetu, hata bila kujua maendeleo ya kiteknolojia ya leo hii. Yeye pia alipitia katika ujana msumbufu: lakini hakuridhika, hakunyamazisha kilio cha moyo wake. Alitafuta ukweli ambao haudanganyi, uzuri ambao haupiti. Alipataje? Alipataje urafiki wa dhati, upendo wenye uwezo wa kutoa tumaini? Kwa kukutana na yule ambaye tayari alikuwa akimtafuta: Yesu Kristo.
Je aliyajengaje maisha yake ya baadaye? Kwa kumfuata, rafiki yake wa maisha. Haya ndiyo maneno yake: “Hakuna urafiki ulio mwaminifu isipokuwa katika Kristo. Ni ndani Yake pekee ndipo inawezekana kuwa na furaha na milele" ( Dhidi ya Barua Mbili za Wapelagi, I, I, 1); "Anampenda sana rafiki yake ambaye anampenda Mungu katika rafiki yake" (Mahubiri 336). Urafiki na Kristo, ambao ni msingi wa imani, sio msaada mmoja kati ya mingine mingi tu katika kujenga siku zijazo: ni nyota yetu inayoongoza. Kama Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati alivyoandika, "Kuishi bila imani, bila urithi wa kulinda, bila kuendeleza mapambano kwa ajili ya Ukweli, si kuishi, bali kutafuta riziki"(Barua, Februari 27, 1925). Mahusiano yetu yanapoakisi uhusiano huu mkubwa na Yesu, hakika tunakuwa wanyoofu, wakarimu na wa kweli.
Swali la 2 Ujasiri wa kuchagua
Baba Mtakatifu, miaka yetu ina alama ya maamuzi muhimu ambayo tunaalikwa kuchukua ili kuelekeza mstakabali wa maisha yetu. Licha ya hayo, kwa sababu ya hali ya ukosefu wa urafiki unaotuzunguka, tunashawishika kusubiri na woga kwa ajili ya wakati ujao usiojulikana na unatugandisha. Tunajua kwamba kuchagua ni sawa na kujikatalia kitu kwa hiyo kinatukwamisha, licha ya yote tunaelewa kwamba matumaini yanapeleka katika lengo la kufikia, hata kama linaakisiwa na hali ya hatari ya wakati huu.
Baba Mtakatifu, tunakuuliza: tupate wapi ujasiri wa kuchagua? Tunawezaje kuwa wajasiri na kuishi maisha ya uhuru wa kweli, tukifanya chaguzi za dhati na zenye maana?
Jibu la Papa: Chaguo ni tendo la msingi la mwanadamu. Kulitazama kwa uangalifu, tunaelewa kuwa sio kuchagua kitu tu, bali ni juu ya kuchagua mtu. Tunapochagua, kwa maana ya kina, tunaamua tunataka kuwa nani. Chaguo la mwisho, kiukweli, ni uamuzi wa maisha yetu: unataka kuwa mtu wa aina gani? Unataka kuwa mwanamke wa aina gani? Vijana wapendwa, tunajifunza kuchagua kupitia majaribu ya maisha, na kwanza kabisa kwa kukumbuka kwamba tulichaguliwa. Kumbukumbu hii lazima ichunguzwe na kukuzwa. Tulipokea uzima kwa uhuru, bila kuchagua! Katika asili ya sisi wenyewe haikuwa uamuzi wetu, lakini upendo ambao ulitutaka. Katika maisha yetu yote, rafiki wa kweli ni yule anayetusaidia kutambua na kufanya upya neema hii katika chaguzi ambazo tumeitwa kufanya.
Vijana wapendwa, mlisema kwa usahihi: "Kuchagua pia kunamaanisha kuacha kitu kingine, na hii wakati mwingine hutuzuia." Ili kuwa huru, lazima tuanze kutoka katika msingi thabiti, kutoka katika mwamba unaounga mkono hatua zetu. Mwamba huo ni upendo unaotutangulia, unatushangaza, na unatuzidi sana: ni upendo wa Mungu. Kwa hiyo, mbele yake, uchaguzi unakuwa hukumu isiyoondoa mema, lakini daima inaiongoza kwa ubora. Ujasiri wa kuchagua unatokana na upendo, ambao Mungu anatuonesha katika Kristo. Ni Yeye ambaye alitupenda kwa nafsi yake yote, akiokoa ulimwengu na hivyo kutuonesha kwamba zawadi ya uzima ndiyo njia ya utimilifu wetu binafsi. Kwa hiyo, kukutana na Yesu kunalingana na matamanio ya ndani kabisa ya mioyo yetu, kwa sababu Yeye ndiye Upendo wa Mungu aliyemfanya mwanadamu.
Kwa habari hiyo, miaka ishirini na mitano iliyopita, hapa tulipo, Papa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alisema: “Ni Yesu mnayemtafuta, tunapoota furaha; Ni Yeye ambaye uwaudhi kwa kiu hiyo ya itikadi kali ambayo haiwaruhusu kutulia kwa maafikiano; Yeye ndiye anayewasukuma kumwaga vinyago vinavyofanya maisha kuwa ya uwongo; ndiye asomaye moyoni mwenu maamuzi ya kweli ambayo wengine wangeweza kuyakandamiza” (Mkesha wa Maombi kwa ajili ya Siku ya 15 ya Vijana Duniani, Agosti 19, 2000). Hofu basi huleta tumaini, kwa sababu tuna hakika kwamba Mungu hukamilisha kile anachoanza. Tunatambua uaminifu wake katika maneno ya wale wanaopenda kweli, kwa sababu wamependwa kweli.
"Wewe ni maisha yangu, Bwana": hivi ndivyo kuhani na mwanamke aliyewekwa wakfu hutamka, amejaa furaha na uhuru. "Nakukaribisha kama bibi arusi na mume wangu": huu ni msemo unaobadilisha upendo wa mwanamume na mwanamke kuwa ishara yenye matokeo ya upendo wa Mungu. Hizi ni chaguo kali na za maana: ndoa, madaraja matakatifu, na kujitolea kwa utawa huonesha zawadi ya bure na ya ukombozi ya nafsi ambayo hutufanya kuwa na furaha ya kweli. Chaguzi hizi hutoa maana kwa maisha yetu, zikibadilisha kuwa mfano wa Upendo kamili, uliowaumba na kuwakomboa kutoka katika uovu wote, hata kifo.
Ninatoa mawazo hata ya wasichana wawili, Maria, mwenye umri wa miaka ishirini kutoka Hispania, na Pascale, mwenye umri wa miaka kumi na minane kutoka Misri. Wote wawili walichagua kuja Roma kwa ajili ya Jubilei ya Vijana, na kifo kiliwapata katika siku za hivi karibuni. Tuwaombee pamoja, mahujaji wa matumaini; tuwaombee familia zao, marafiki zao, na jumuiya zao. Yesu Mfufuka awakaribishe katika amani na furaha ya Ufalme wake. Na tumwombee kijana Mhispania, Ignacio Gonzalvez, aliyelazwa katika hospitali ya Bambino Gesù. Jinsi gani ulimwengu unavyohitaji wamisionari wa Injili ambao ni mashuhuda wa haki na amani! Ni kiasi gani wakati ujao unahitaji wanaume na wanawake ambao ni mashuhuda wa matumaini! Hii, vijana wapendwa, ndiyo kazi ambayo Bwana Mfufuka anatukabidhi.
Swali la 3:Wito kwa Wema na thamani ya ukimya
Baba Mtakatifu, tunavutiwa na maisha ya ndani hata kama kwa mtazamo wa kwanza tunahukumiwa kuwa wa juu juu na wasio na wasiwasi. Tunahisi ndani yetu mwito wa uzuri na wema kama chanzo cha ukweli. Thamani ya ukimya, kama ilivyo kwenye Mkesha huu, inatuvutia, hata kama wakati fulani inatia hofu kutokana na hisia ya utupu.
Baba Mtakatifu ninakuuliza: ni kwa jinsi gani tunaweza kweli kukutana na Bwana Mfufuka katika maisha yetu na kuwa na uhakika wa uwepo wake hata katikati ya magumu na mashaka?
Jibu la Papa: Mwanzoni kabisa mwa Hati ambayo alitangaza Jubilei, Papa Francisko aliandika kwamba: "katika moyo wa kila mtu kuna tumaini kama hamu na matarajio ya mema" (Spes non confundit, 1). Kusema "moyo," katika lugha ya kibiblia, inamaanisha kusema "dhamiri”: kwa kuwa kila mtu anatamani mema moyoni mwake, kutoka katika chanzo hiki huchipua tumaini la kuipokea. Lakini wema ni nini? Ili kujibu swali hili, tunahitaji shuhuda: mtu anayetufanyia wema. Hata zaidi, tunahitaji mtu ambaye ni mwema wetu, anayesikiliza kwa upendo shauku inayochochea dhamiri yetu. Bila mashuhuda hawa, tusingalizaliwa, wala hatungekua katika wema: kama marafiki wa kweli, wanaunga mkono hamu yetu ya pamoja ya wema, wakitusaidia kutambua hilo katika uchaguzi wetu wa kila siku.
Vijana wapendwa, rafiki ambaye daima anaandamana na dhamiri zetu ni Yesu. Je, mnatamani kweli kukutana na Bwana Mfufuka? Sikilizeni neno lake, ambalo ni Injili ya wokovu! Tafuteni haki, mkitengeneza upya njia yenu ya maisha, ili kujenga ulimwengu wa kibinadamu zaidi! Watumikie maskini, mkishuhudia wema tunaotamani kuupokea kutoka kwa jirani zetu! Tuabudu Ekaristi, chemchemi ya uzima wa milele! Jifunzeni, kufanya kazi, na mpende kwa namna ya Yesu, Mwalimu mwema ambaye daima hutembea kando yetu.
Katika kila hatua, tunapotafuta mema, na tumwombe: Kaa nasi, Bwana (rej. Lk 24:29)! Kaa nasi, kwani bila Wewe hatuwezi kufanya mema tunayotamani. Unatutakia mema; Wewe ni mwema wetu. Wale wanaokutana Nawe wanatamani kwamba wengine pia wakutane Nawe kwa sababu neno Lako ni nuru angavu zaidi kuliko nyota yoyote, na kuangaza hata usiku wa giza zaidi. Kama vile Papa Benedikto XVI alivyopenda kurudia, kwamba wale wanaoamini hawako peke yao. Kwa hiyo, kiukweli tunakutana na Kristo Kanisani, yaani, katika ushirika na wale ambao Bwana mwenyewe huwakusanya karibu naye kukutana naye, katika historia, kila mtu anayemtafuta kwa dhati. Jinsi gani ulimwengu unavyohitaji wamisionari wa Injili ambao ni mashuhuda wa haki na amani! Ni kiasi gani wakati ujao unahitaji wanaume na wanawake ambao ni mashuhuda wa matumaini! Hii, vijana wapendwa, ndiyo kazi ambayo Bwana Mfufuka anatukabidhi.
Katika ahadi hii ya kudumu, kama Mtakatifu Agostino alivyoandika: “Mwanadamu, chembe ya uumbaji wako, Ee Mungu, anataka kukusifu. Ni Wewe unayemtia moyo kufurahia sifa zako, kwa sababu umetufanya kwa ajili yako, na mioyo yetu haina utulivu mpaka inatulia ndani yako. Nikutafute wewe, Bwana, nikikuomba, na nikuombe kwa kukuamini wewe” (Confessions, I). Kwa kuchanganya ombi hili na maswali yenu, wapendwa vijana, ninawakabidhi sala: “Asante, Yesu, kwa kutufikia: Nia yangu ni kubaki miongoni mwa marafiki zako, ili, kwa kukukumbatia, niwe mshiriki wa safari kwa wote wanaokutana nami. Ewe Bwana Mjalie kila anayekutana nami akutane na Wewe, hata kwa mapungufu yangu, hata katika udhaifu wangu.” Kupitia maneno haya, mazungumzo yetu yataendelea kila wakati tunapotazama Msalaba: ndani yake mioyo yetu itakutana. Kwa hiyo, dumu katika imani kwa furaha na ujasiri. Asante!