Papa Leo XIV:Hatupaswi kujiuzulu kwa kuenea kwa mantiki ya migogoro na silaha!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika lango la Jumba la Kipapa huko Castel Gandolfo, siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Siku Kuu ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, tarehe 15 Agosti 2025, alisema: “Leo tunataka kukabidhi ombi letu la amani kwa maombezi ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni. Yeye kama Mama anateseka kwa maovu yanayowatesa watoto wake, hasa watoto wadogo na wanyonge. Amethibitisha hili mara nyingi kwa karne nyingi kwa ujumbe na maonesho.”
Papa aliendelea kusema kuwa: “Katika kutangaza dogma ya Kupalizwa mbinguni, wakati tukio la kutisha la Vita vya Pili vya Kidunia ambavyo vilikuwa bado moto vinaunguza, Papa, Pio XII aliandika: “Tunapaswa kutumainia kwamba wote wanaotafakari juu ya mfano mtukufu wa Maria wataendelea kusadikishwa zaidi kuhusu thamani ya maisha ya mwanadamu,” na alikuwa na matumaini kwamba “maisha ya mwanadamu hayapotezwi tena kwa kuchochea vita” (Katiba ya Kitume Munificentissimus Deus ).
Ni kwa jinsi gani maneno haya yanafaa sana! Kwa bahati mbaya, hata leo tunahisi kutokuwa na msaada katika kukabiliana na kuenea kwa jeuri duniani kote, inazidi kuwa kiziwi na kutokuwa na hisia kwa kila msukumo wa binadamu. Licha ya hayo hatupaswi kupoteza tumaini: Mungu ni mkuu kuliko dhambi ya wanadamu. Hatupaswi kujiuzulu kwa kuenea kwa mantiki ya migogoro na silaha.
Pamoja na Maria, tunaamini kwamba Bwana anaendelea kuwasaidia watoto wake, akikumbuka huruma yake. Ni ndani yake tu ndipo inawezekana kugundua tena njia ya amani.
Papa Leo XIV aliendelea kutoa salamu zake kwa wote, mahujaji kutoka Italia na nchi mbalimbali. Aliwasalimia jumuiya ya uinjilishaji ya Chuo kikuu kutoka Honduras; familia za Harakati ya Upendo wa Familia, ambao wamehitimisha Mafungo yao ya Kiroho; na kikundi cha "Mtakatifu Rita" cha wanandoa na wachumba. Heri na siku kuu njema kwa wote!