Papa Leo XIV akutana na Rais wa Zimbabwe,Bw.Mnangagwa
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 30 Agosti alikutana na Bwana Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe. Kwa mjibu wa taarifa kutoka Vyombo vya habari, Vatican imebainisha kuwa: "Leo tarehe 30 Agosti 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV amempokea kwa mkutano, katika Jumba la Kitume la Vatican, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa, ambaye baadaye alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, akifuatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Uhusiano wa Kimataifa na Mashirika ya Kimataifa."
Taarifa hiyo aidha inaongeza kusema: “Wakati wa mazungumzo ya dhati katika Sekretarieti ya Vatican ilibanishwa uhusiano mzuri kati ya Vatican na Zimbabwe. Kisha tahadhari ilitolewa kwa nyanja mbalimbali za hali ya kisiasa na kijamii na kiuchumi ya nchi, hasa ushirikiano wake na Kanisa mahalia kuhusu mazingira, elimu na afya.” Wakati wa mijadala hiyo, pia kulikuwa na “kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kikanda, yakisisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa pande nyingi, mazungumzo na ushirikiano kati ya mataifa.”