Kumbukizi la Miaka 166 Tangu Afariki Dunia Mt. Yohane Maria Vianney
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2025 anaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 166 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia. Papa Pio XI kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi na Mwombezi wa Maparoko Duniani. Ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 40 alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa sala, toba na wongofu wa ndani, uliofumbatwa katika maisha ya unyenyekevu. Akajitahidi kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Changamoto na mwaliko kwa Mapadre wote, kuiga mfano wa Kristo Yesu mchungaji mwema. Kristo Yesu ni mchungaji mwema kwa sababu anawapenda watu wake upeo. Ni katika muktadha huu, Mapadre na viongozi wa Kanisa katika ujumla wao, wanapaswa kuonesha ule moyo wa upendo na ukarimu kwa kulisha Kondoo wa Kristo, ili kuwatangazia na kuwashuhudia huruma na upendo wake, kutokana na madonda ambayo kila mmoja wao anayo! Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata: amani na utulivu, faraja na usalama wao!Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaandikia Mapadre wote ujumbe akisema kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa upendo ni mwili ulio hai na wa uzima unaomkaribisha kila mmoja wao, ukiwageuza kuwa mfano wa Mchungaji Mwema na hapo ndipo wanapoelewa utambulisho wa kweli wa huduma yao: kuchomwa na rehema ya Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya upendo wake ambao huponya, kuandamana na kukomboa. Kumbe, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inapyaisha mioyoni mwao wito wa zawadi kamili ya wao wenyewe katika huduma ya watu watakatifu wa Mungu. Huu ni utume unaoanza kwa sala na kuendelea katika muungano na mafungamano na Kristo Yesu, ambaye anaendelea kuhuisha ndani mwao karama yake: wito mtakatifu wa ukuhani.
Kukumbuka neema hii, kama Mtakatifu Augustino asemavyo, ina maana ya kuingia “patakatifu pa patakatifu pasipo mwisho” ambayo haihifadhi tu kitu kutoka kwa wakati uliopita, lakini daima hufanya kile kilichohifadhiwa humo kuwa kipya na cha sasa. Ni kwa kukumbuka tu ndipo wanapoishi na kuhuisha kile ambacho Kristo Yesu amewakirimia na wao kwa zamu kukirithisha kwa jina lake. Kumbukumbu inaunganisha mioyo yao katika Moyo wa Kristo Yesu na maisha yao katika maisha ya Kristo Yesu, ili waweze kuwa na uwezo wa kuleta Neno na Sakramenti za wokovu kwa watu watakatifu wa Mungu, kwa ulimwengu uliopatanishwa kwa upendo. Ni katika Moyo wa Kristo Yesu pekee, ndipo Mapadre wanapopata ubinadamu wao wa kweli kama watoto wateule wa Mungu na ndugu kati yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, changamoto mamboleo ni kushughulikia kwa haraka, ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa umoja na amani.Katika Ulimwengu mamboleo wenye kinzani na mivutano inayoongezeka kila kukicha hata ndani ya familia na Jumuiya za Kikanisa, Padre anaitwa kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho unaozalisha umoja na ushirika. Wanahamasishwa kuwa ni wajenzi wa umoja na amani, wakiwa na utambuzi na wajenzi wa umoja, ili kuwasaidia watu kupata mwanga wa Injili katika taabu na magumu ya maisha yanayowaandama kila kukicha. Hii inamaanisha kwamba, Mapadre wawe wasomaji wenye busara katika ukweli, kwa kwenda zaidi ya hisia za wakati huo, hofu na mitindo; maana yake ni kutoa mapendekezo ya shughuli za kichungaji yanayozalisha na kupyaisha imani kwa kujenga mafungamano na mahusiano mema; kwa kukuza na kudumisha vifungo vya mshikamano, jumuiya ambamo mtindo wa udugu wa kibinadamu unaendelea kung’aa. Kuwa wajenzi wa umoja na amani maana yake si kujilazimisha, bali ni kujisadaka na kutumikia. Udugu wa Kikuhani unakuwa ni ishara ya kuaminika ya uwepo wa Kristo Yesu, Mfufuka kati ya waja wake, anayeonesha safari ya pamoja na Mapadre wake.
Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika Makuhani kupyaisha tena ile “ndiyo” yao mbele ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu wake watakatifu, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya: neema, watu wanaohifadhi ule moto wa Roho Mtakatifu walioupokea wakati walipokuwa wanawekwa wakfu, ili kwa kuunganishwa naye wapate kuwa ni Sakramenti ya upendo wa Kristo Yesu ulimwenguni. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia Makuhani wenzake kwamba, wasiogope kuhusu udhaifu na mapungufu yao kwani Kristo Yesu hatafuti Makuhani wakamilifu, lakini anawapenda wale wenye moyo wa unyenyekevu, ulio wazi kwa toba na wongofu wa ndani, tayari kupenda kama Kristo Yesu mwenyewe alivyowapenda waja wake. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alipendekeza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu iwe ni mahali muafaka pa kukutana binafsi na Kristo Yesu; Mahali ambapo Makuhani wanaweza kutatua migogoro na changamoto za maisha zinazoendelea kuusambaratisha ulimwengu mamboleo, kwani ndani mwake, wanakuwa na uwezo wa kuhusianisha ulimwengu huu wenye furaha na upendo katika kujenga umoja na upendo wa moyo wenye afya na ule wa Kristo Yesu unaweza kufanya muujiza huu wa kijamii. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ni mwaliko kwa Makuhani kuwa ni mahujaji wa matumaini na kwamba, huduma yao itaweza kuzaa matunda mengi zaidi ikiwa kama watakita maisha yao katika Sala, Msamaha; Ukaribu na Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii. Ikiwa wataonesha ukaribu kwa familia na vijana katika kutafuta na kuuambata ukweli na kwamba, Padre Mtakatifu hufanya utakatifu ustawi karibu naye. Baba Mtakatifu Leo XIV Mwishoni mwa ujumbe wake kwa Makuhani kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Mitume na Mama wa Makuhani na hatimaye, akawabariki wote.
Katika maadhimisho ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akatangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani. Huu ukawa ni muda wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Ukuu, Utakatifu, Wito na Maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa. Mapadre walikumbushwa kwamba, utambulisho na uhuru wa wafuasi wa Kristo Yesu ni mambo makuu mawili yanayowawezesha hata Mapadre katika maisha na utume wao, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Kama binadamu watambue udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, changamoto ni kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya: Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Maisha ya Sala, Sakramenti za Kanisa, mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbalimbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini.
Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya kisakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Katika Maadhimisho haya, Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbalimbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika barua hii alipenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Hayati Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao. Ushuhuda wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Maria Vianney uwe ni mfano bora wa sadaka na majitoleo ya maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1786. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwa shida kubwa, alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815. Akafariki dunia tarehe 4 Agosti 1859 akiwa na umri wa miaka 73. Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani.