MAP

Wadau wa tasnia ya mawasiliano  ya jamii ni mahujaji wa matumaini. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii ni mahujaji wa matumaini.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe wa Siku ya 59 ya Upashanaji wa Habari Ulimwenguni 2025

Kauli mbiu: Daima muwe tayari kujibu kila mtu awaulizaye sababu ya tumaini lililo ndani yenu; lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima.” (1 Pet 3:15-16). Katika mazingira ya sasa ambapo taarifa nyingi zinatolewa na vituo vichache vyenye ushawishi mkubwa, mawasiliano yamekuwa silaha badala ya daraja la maelewano. Mawasiliano haya mara nyingi huchochea hisia kali, upotoshaji wa makusudi na uhasama unaovuruga umoja, amani, upendo na mshikamano!

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Katika ujumbe wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, amewataka waandishi wa habari na wataalamu wa mawasiliano kuwa ‘wawasilishaji wa tumaini’ katika dunia inayokumbwa na mwelekeo wa habari zenye hofu, chuki na upotoshaji wa ukweli. Ujumbe wake kwa Mwaka 2025 unaoongoza na kauli mbiu iliyotolewa katika kifungu cha Barua ya Kwanza ya Mtakatifu Petro kisemacho: “Shirikishaneni kwa upole matumaini yaliyomo moyoni mwenu (IPt3;15-16).” Katika ujumbe wake wa kina uliotolewa mjini Roma, katika Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Sales tarehe 24 Januari 2025, Papa Francisko alieleza kuwa, ujumbe umetolewa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei Kuu 2025 wakati wa neema na tafakari ya kiroho kwa Wakristo kote duniani. Ukijikita katika mafundisho ya Biblia hasa 1 Petro 3:15-16, ujumbe huu unahimiza wadau wa sekta ya mawasiliano ya jamii kuwa tayari kutoa sababu ya tumaini lililo ndani yao, kwa upole na heshima.

Muwe tayari kujibu kila mtu awaulizaye sababu ya tumaini lililo ndani yenu.
Muwe tayari kujibu kila mtu awaulizaye sababu ya tumaini lililo ndani yenu.

“Mtakase Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Daima muwe tayari kujibu kila mtu awaulizaye sababu ya tumaini lililo ndani yenu; lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima.” (1 Pet 3:15-16). Katika mazingira ya sasa ambapo taarifa nyingi zinatolewa na vituo vichache vyenye ushawishi mkubwa, mawasiliano yamekuwa silaha badala ya daraja la maelewano. Katika ujumbe huo, imeelezwa kuwa mawasiliano haya mara nyingi huchochea hisia kali, upotoshaji wa makusudi na uhasama unaovuruga umoja na mshikamano wa kijamii. Hayati Papa Francisko katika ujumbe huo aliongeza kuwa matumizi mabaya ya teknolojia za kidijitali yamechangia kwa kiasi kikubwa kutawanywa kwa makusudi kwa umakini wa watu, hali ambayo inaharibu uwezo wa jamii kuungana, kusikilizana na kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hata hivyo, ujumbe huo unatoa mwanga mpya kwa kuhimiza matumaini yasiyoyumba yenye tumaini ambalo halitegemei hisia bali lina msingi wa kiimani, lina nguvu ya kubadili maisha na jamii. Tumaini hili, kama walivyoeleza ni zawadi na wito kwa Wakristo wote.

Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii ni mahujaji wa imani na matumaini
Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii ni mahujaji wa imani na matumaini   (Vatican Media)

“Yule mwenye tumaini anaishi kwa namna tofauti; yule anayetarajia amepewa zawadi ya maisha mapya,” aliwahi kusema Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume “Spe salvi” yaani “Tumaini linalookoa” anakaza kusema waandishi wa habari, wanablogu na wana mawasiliano waliombwa kutumia karama na vipawa vyao kwa njia chanya kuandika, kuripoti na kuzungumza kwa njia inayojenga badala ya kubomoa, kwa kutumia ukweli na heshima kama nguzo kuu za Taaluma yao. Ujumbe huo unaweka wazi kuwa katika kila taarifa, kila picha, kila sauti ina nafasi ya kutoa tumaini: si kwa njia ya kukwepa uhalisia bali kwa kuangaza uwepo wa mema hata katika giza kubwa zaidi. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitoa wito kwa ulimwengu wote kuendeleza mawasiliano yenye upole, heshima na tumaini katika kuuenzi Mwaka huu wa Jubilei unaoadhimishwa kama ‘Mwaka wa Neema.’

Sarah Pelaji alipokutana na Hayati Papa Francisko
Sarah Pelaji alipokutana na Hayati Papa Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Akinukuu maneno ya Mtakatifu Petro, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alisisitiza kuwa majibu yetu kwa changamoto na maswali ya maisha yawe kwa upole na kwa heshima. Ameeleza kuwa mawasiliano ya Kikristo yanapaswa kuwa kama mazungumzo ya wasafiri wanaotembea pamoja, mawasiliano yanayochochea matumaini, huruma na mshikamano wa kweli. Katika hotuba hiyo, Baba Mtakatifu Francisko alimrejea Yesu wa Nazareti kama mfano mkuu wa mwasilishaji, akitaja simulizi la wanafunzi wa Emau ambapo Yesu alizungumza nao kwa upendo na kuwaamsha mioyo yao kupitia Maandiko. Hili limechukuliwa kama kielelezo cha jinsi mawasiliano yanavyoweza kuwa chombo cha uponyaji na umoja. Akielezea juu ya mawasiliano yasiyochochea hofu wala hasira, Baba Mtakatifu Francisko ameonya dhidi ya mawasiliano ya fujo, ya kujitukuza, au yenye nia ya kushindana au kushambulia. Badala yake, amehimiza mawasiliano yanayogusa moyo wa binadamu, yanayofichua wema hata katika mazingira ya kukata tamaa, na yanayozalisha utamaduni wa kujali.

Wafanyakazi wa Jugo Media katika ubora wao
Wafanyakazi wa Jugo Media katika ubora wao   (@jugomedia)

Katika kuangazia ujumbe wa kijamii wa Jubilei, Baba Mtakatifu Leo XVI ametaja umuhimu wa mawasiliano yanayofikisha matumaini kwa watu walioko pembezoni mwa jamii kama: wafungwa, maskini, wahamiaji, na waathirika wa vita na migogoro. Ametoa changamoto kwa wanahabari na watangazaji kuwa ‘wachimba dhahabu’ wa simulizi za wema na matumaini zilizojificha katika kivuli cha matukio ya kila siku. “Tumaini ni mradi wa kijamii,” amesema Baba Mtakatifu Francisko huku akisisitiza kuwa, safari ya maadhimisho ya Jubilei ni ya pamoja na kila mtu amealikwa kupita katika Lango Takatifu ishara ya mwanzo mpya, msamaha na rehema ya Mungu. Pamoja na hayo, amewahimiza wanahabari na wadau wa mawasiliano kutunza maisha yao ya ndani, wasisahau nyuso na mioyo ya watu wanaowahudumia na wajiepushe na miitikio ya haraka au ya kihisia isiyo na tafakari. Hayati Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha kwa kutoa wito wa kuwa mashuhudi wa mawasiliano yasiyo ya fujo, mawasiliano yanayojenga madaraja badala ya kuta na hadithi zinazojenga matumaini katika Ulimwengu unaoweza kugawanyika. “Kwa neema ya Mungu, tunaweza kuwa waandishi wa historia mpya ya matumaini, huruma na maisha ya pamoja,” amesema Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika baraka zake kwa wote wanaojihusisha na tasnia ya mawasiliano ya jamii.

Upashanaji Habari 2025
31 Julai 2025, 14:44