MAP

Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani itakayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025 Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani itakayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025  (@Comunità Sant'Egidio)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Siku ya 5 Ya Bibi, Babu na Wazee Duniani Kwa Mwaka 2025

Katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani inayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025, Papa Leo XIV ametoa wito wa matumaini kwa wazee akisisitiza umuhimu wao kama mashuhuda wa imani, hekima na upendo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Heri wale ambao hawajapoteza tumaini” (rej. Sir 14:2). Papa Leo XIV amesema, Jubilei inayoendelea ni nafasi ya kutambua kuwa tumaini ni chanzo cha furaha ya kweli kwa wazee.

Na Sarah Pelaji, Vatican.

Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni nafasi muafaka ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuyafanyia kazi na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili na kiutu. Changamoto ya kwanza ni kuubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha na utume wa ndoa na familia sanjari na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu. Kimsingi, familia zinahitaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, zitakazowawezesha wanandoa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Familia inapaswa kusimikwa katika upendo wenye huruma, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linayotangaza na kushuhudia uwepo mwanana wa Mwana wa Mungu. Katika shida na magumu, familia zisaidiwe kwa hali na mali, ili kuweza kupita vipindi hivi vigumu kwa kusindikizwa na upendo wenye huruma. Familia zinazoogelea kwenye shida na ugumu wa maisha zisikilizwe na zisaidiwe. Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao.

Siku ya tano ya Bibi, Babu na Wazee Ulimwenguni 2025
Siku ya tano ya Bibi, Babu na Wazee Ulimwenguni 2025   (ANSA)

Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na ukahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Siku ya Mababu, Mabibi na Wazee ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha: Umoja, udugu, upendo na faraja tunu msingi katika maisha ya kijamii. Ni muda kwa waamini kujifunza sanaa ya kupenda na kupendwa na katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa magwiji kwa vijana wa kizazi kipya! Ndoto, kumbukumbu na sala ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa.

Familia isimikwe katika upendo wenye huruma
Familia isimikwe katika upendo wenye huruma

Kila mwaka Kanisa Katoliki Kiulimwengu huadhimisha siku ya Wazee Ulimwenguni kila ifikapo Dominika ya nne ya Mwezi Julai. Siku hii ilianzishwa na Papa Francisko mnamo 2021 kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa kizazi cha wazee katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, Familia na Maisha, katika mwaka huu 2025, lilichapisha kauli mbiu inayoongoza Siku V ya Wazee Ulimwenguni itakayoadhimisha tarehe 27 Julai 2025. Katika taarifa hiyo inabainisha kuwa: “Baba Mtakatifu Leo XIV alichagua mada ya maadhimisho hayo isemayo “Heri ambaye hajapoteza matumaini yake” (Sir 14:2). Maneno haya, yaliyotolewa katika kitabu cha Sira, yanaonesha baraka za wazee na kuonesha katika tumaini lililowekwa kwa Bwana katika njia ya Mkristo na kupatanishwa na uzee. Katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Wazee Duniani itakayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa matumaini kwa wazee kote ulimwenguni, akisisitiza umuhimu wao kama mashuhuda wa imani, hekima na upendo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Heri wale ambao hawajapoteza tumaini” (rej. Sir 14:2). Papa Leo XIV amesema kuwa Jubilei inayoendelea ni nafasi ya kutambua kuwa tumaini ni chanzo cha furaha ya kweli, haswa kwa wale walio katika uzee. Akinukuu mifano ya kibiblia ya Abrahamu, Sara, Zakaria na Elizabeti, ameeleza jinsi Mungu huwaita watu katika uzee wao kushiriki katika mpango wa wokovu, na hivyo kuonyesha kuwa uzee ni wakati wa neema na baraka. “Tunaweza kumfikiria Abrahamu na Sara, ambao wakiwa wamekomaa kwa miaka, walipata ugumu kuamini walipoahidiwa mtoto na Mungu. Kutokuwa na mtoto kulionekana kuwa kikwazo kwao kuendelea kuwa na matumaini ya baadaye.

Siku ya Babu, Bibi na Wazee inaadhimishwa Dominika 27 Julai 2025
Siku ya Babu, Bibi na Wazee inaadhimishwa Dominika 27 Julai 2025   (Vatican Media)

Zakaria naye alipoambiwa juu ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, alisema: “Nitawezaje kuwa na hakika ya jambo hili? Maana mimi ni mzee, na mke wangu naye ni mzee sana” (Lk 1:18). Uzee, utasa na udhaifu wa kimwili vilionekana kuwa vizuizi vya tumaini na uhai. Swali la Nikodemo kwa Yesu pia linaonekana kuwa la kejeli: “Je, mtu anaweza kuzaliwa tena akiwa mzee? Anaweza kuingia tumboni mwa mama yake mara ya pili na kuzaliwa?” (Yn 3:4). Lakini kila tunapofikiri kuwa mambo hayawezi kubadilika, Bwana hutushangaza kwa tendo la wokovu. Wazee ni mashahidi wa kwanza wa tumaini mbele za Mungu,” amesema Baba Mtakatifu Leo XIV huku akiongeza kuwa Maandiko Matakatifu yanadhihirisha jinsi Mungu huweka thamani kubwa kwa uzee na mchango wake katika jamii ya waamini. Amekemea utamaduni uliopo katika jamii wa kuwasahau na kuwaweka wazee kando akitoa mwito kwa Kanisa zima kufanya mapinduzi ya shukrani na utunzaji. Amezitaka parokia, jumuiya na mashirika ya Kikristo kujitokeza kwa wingi katika kuwahudumia wazee kupitia kutembelea, sala na kusaidia kurejesha matumaini kwao. “Jamii zetu zimezoea kuwaacha wazee nyuma, jambo ambalo linahitaji mabadiliko ya dhati. Tunaitwa kurejesha thamani na heshima wanayostahili,” amesema Baba Mtakatifu Leo XIV. Katika muktadha wa Jubilei ya Mwaka 2025 wa Ukristo, Papa Leo XIV amekumbusha kwamba hii ni fursa ya ukombozi kwa wazee wanaoteseka kutokana na upweke hasi na kutelekezwa. Akitaja mafundisho ya Yesu katika Sinagogi la Nazareti, amesisitiza kuwa Jubilei ni muda wa Habari Njema, uhuru na urejesho wa heshima kwa kila mtu, hasa wazee.

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV pia ametangaza kuwa wazee wasioweza kusafiri kwenda Roma kwa ajili ya hija ya Jubilei wanaweza kupata rehema kamili kwa kuwatembelea wenzao wanaoishi peke yao, akieleza kuwa matendo hayo ni njia ya kukutana na Kristo aliye ndani yao. Amewahimiza wazee kutazama siku zijazo kwa matumaini badala ya kutazama nyuma kwa huzuni. Amewakumbusha kuwa licha ya udhaifu wa miili, bado wana uwezo mkubwa wa kupenda, kusali, na kuwa na mchango muhimu katika jamii. “Hata ikiwa utu wa nje unadhoofika, utu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku, 2 Kor 4:16-18,” amesema, akinukuu 2 Kor 4:16-18. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu Leo XIV unaendeleza wito huo kwa msisitizo mpya kwamba tumaini halifi, na wazee ni walinzi wake wakuu.Licha ya Kanisa Katoliki ulimwenguni kuadhimisha maadhimisho hayo, Kijamii pia huadhimishwa ambapo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UN mnamo tarehe 14 Desemba 1990 liliteua tarehe Mosi Oktoba, kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee (azimio 45/106).  Mwaka 1991, Baraza Kuu lilipitisha Kanuni za Umoja wa Mataifa kwa Wazee (azimio 46/91). yakilenga kuelimisha jamii haki na stahili mbalimbali zinazohitajika kwa Wazee hao, sanjari na kuwakumbusha umuhimu wa uwepo wao katika jamii husika. Waswahili husema ‘Uzee ni dawa na kwamba uzee na wazee ni chemchemi ya neema na baraka’ lakini pamoja na umaarufu wa msemo huo, bado wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo afya kutokana na kunyemelewa na maradhi mbalimbali yasiyoambukiza. Wazee ni watu muhimu na kutokana na ukweli huu, Serikali inatakiwa kubadili mfumo wa upatikanaji wa huduma ya wazee uliopo na ijikite katika kuwapatia wazee bima ya Afya ya Daraja la juu kuweza kuwasaidia kiuhakika. Ikumbukwe kwamba wazee wengi huchukuliwa kama tabaka lilotengwa, hivyo Serikali katika kuwatunza zihasiiishie kutoa huduma za matibabu pekee, bali hata kujua makazi yao, vyakula na kuwasaidia vipato.

Siku ya 5 ya Wazee Duniani 2025

 

24 Julai 2025, 15:56