Tarehe 30 Julai Katekesi za Papa Leo XIV zinaanza tena!
Vatican News.
Baada ya mapumziko ya kiangazi, Katekesi ya Papa Leo XIV itaanza tena tarehe 30 Julai 2025. Ikumbukwe Katekesi ya kila Jumatano, kabla ya mapumziko ya kawaida ya majira ya kiagazi, ilifanyika tarehe 25 Juni 2025 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, ambapo Papa Leo XIV kisha alisafiri hadi Castel Gandolfo kwa kipindi cha mapumziko. Baba Mtakatifu atarejea katika mji wa Lazio siku ya Ijumaa, tarehe 15 Agosti 2025 kuadhimisha Misa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni na kusali sala ya Malaika wa Bwana katika Uwanja wa Libertà. Dominika tarehe 17 Agosti 2025 Papa Leo XIV pia ataongoza sala ya Malaika wa Bwana huko katika Uwanja wa Libertà; na wakati huo alasiri, basi atarudi moja kwa moja mjini Vatican.
Ratiba ya Jubilei ya vijana
Wakati huo huo, baada ya juma na ratiba iliyojaa ya matukio na hadhira ya umma na ya kibinafsi, Papa Leo XIV atakabiliana na Jubilei ya Vijana mwishoni mwa Juma hili. Maelfu na maelfu ya vijana bado wanaendelea kuwasili Roma kutoka pande zote za dunia kushiriki katika tukio kuu la Jubilei; wote watakusanyika Jumamosi, tarehe 2 Agosti huko Tor Vergata, katika uwanja mkubwa sana ambao miaka ishirini na mitano iliyopita ulikuwa eneo la mkesha usiosahaulika pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II.
Mkesha na misa ya kuhitimisha Jubilei
Na tarehe 2 Agosti, vile vile Papa atarejea Tor Vergata kuhitimisha siku ya muziki, shuhuda, na ushirika, huku mkesha ukipangwa kuanzia saa 2:30 usiku. Wakati huo huo siku itayofuata, saa 3:00 kamili asubuhi ambapo itakuwa saa 4 kamili masaa ya Afrika Mashariki na Kati, tena huko Tor Vergata, Papa Leo XIV ataongoza Misa pamoja na vijana na, pamoja nao, saa 6:00 kamili mchana atasali sala ya Malaika wa Bwana. Ndiyo utakuwa mwisho wa Jubilei ya vijana ambayo imeanza tarehe 28 Julai 2025.