Papa Leo XIV:Ubatizo unatupatia dhamana kuachana na utamaduni wa kifo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na Waliongokea ukristo hivi karibuni ( kwa hiyo wabatizwa wapya) na wakatekumeni kutoka nchini Ufaransa, ambalo lilikuwa kundi la watu mia nane, Jumanne tarehe 29 Julai 2025. Papa Leo XIV alianza hotuba yake kwa ishara ya Msalaba na kuwatakia amani. "Wapendwa vijana ninawasalimia ninyi nyote mliofika kwa wingi mjini Roma kwa ajili ya kuishi hija ya matumaini. "Amemsalimia Askofu Jean-Philippe Nault wa Jimbo la Nice ambaye alikuwa hapo na maaskofu wengine ambao wamewasindikiza pamoja na mapadre wao na makatekista. Papa alisema kuwa: “Ni furaha kuwaona vijana ambao wanajikita katika imani na wanataka kutoa maana ya maisha yao, kwa kuacha wasindikizwe na Kristo na Injili yake! Ubatizo unatufanya sisi kuwa wajumbe kamili wa familia kubwa ya Mungu. Mwanzo unakuja daima kutoka kwake na sisi tunajibu kwa kufanya uzoefu wa upendo wake unaookoa. Katika mchakato wao kama wakatekumeni na wabatizwa wapya, kila mmoja wao anafanya mkutano wa kibinafsi na Bwana katika Jumuiya inayokaribisha.
Sisi binafsi tunajitambua kuwa mabinti na wana wa Mungu kupitia ubatizo wetu “katika jina la Baba,” ambaye hututolea kuwa wana; "wa Mwana," ambaye hutujulisha maisha na uhusiano wake na Baba yake; na "Roho Mtakatifu," chanzo cha kila karama (taz. Gal 4:6). Mtakatifu Paulo anafunua matokeo muhimu ya ubatizo anapowaandikia Wagalatia: “Kwa maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (3:27). Ubatizo hututambulisha kwa ushirika na Kristo na hutoa uzima. Unatupatia dhamana kuachana na utamaduni wa kifo ambao umeenea sana katika jamii yetu. Utamaduni huu wa kifo unajidhihirisha leo hii kwa kutojali, kudharau wengine, madawa ya kulevya, kutafuta maisha rahisi, kujamiiana ambayo inakuwa burudani na kupinga utu wa binadamu, dhuluma, nk. Ubatizo hutufanya kuwa mashuhuda wa Kristo. Katika ibada ya ubatizo, kuna ishara kali sana, yenye nguvu sana: tunapopokea mshumaa unaowaka kutoka katika mshumaa wa Pasaka.
Baba Mtakatifu Leo alizidi kukazia kuwa ni nuru ya Kristo, aliyekufa na kufufuka, ambayo tunajitolea kuweka hai kwa kuilisha kwa kusikiliza Neno la Mungu na kwa kuungana daima na Yesu katika Ekaristi. Mtakatifu Ambrose hakuchoka kurudia: "Omnia Christus est nobis!", "Mambo yote ni Kristo kwa ajili yetu!", mwaliko wa kuwa mashahidi wa kweli wa Bwana. Pia alisema, kwa maneno yaliyojaa upendo kwa Yesu: "Omnia Christus est nobis!" Ukitaka kuponya majeraha yako, yeye ndiye tabibu; ukiungua kwa homa, yeye ndiye chemchemi ya kuburudisha; ukionewa na hatia, yeye ni haki; ukihitaji msaada, yeye ni nguvu; ukiogopa mauti, yeye ni uzima; ukitamani mbingu, yeye ndiye njia; ukikimbia giza, yeye ni nuru... Onjeni mwone jinsi Bwana alivyo mwema; amebarikiwa mtu yule anayemtumaini” (De virginitate, 16, 99).
Ili kuishi kwa furaha na amani, tunaitwa kuweka tumaini letu katika Yesu Kristo. Kwa kumfuata Bwana, Papa liongeza "ninyi pia ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu (rej. Mt 5:13-14). Kanisa linahitaji ushuhuda wenu mzuri wa imani ili kukua zaidi na kuwa karibu na kila mtu anayehitaji. Ukatekumeni ni safari ya imani ambayo haiishii kwa ubatizo, bali inaendelea katika maisha yote, yenye nyakati za furaha na nyakati za shida. Kama vile Mtakatifu Augustino anavyotukumbusha: “Kama [Kristo] hangekuwa tumaini letu, hangeweza kutuongoza. Anatuongoza kwa sababu yeye ndiye kiongozi wetu; na anatuongoza pamoja naye kwa sababu yeye ndiye njia yetu; Anatuongoza kwake kwa sababu Yeye ndiye nchi yetu” (Mt. Augustino, Ufafanuzi wa Zaburi 61).
Kwa hiyo Papa alisema kwamba wao wameitwa kushiriki uzoefu wao wa imani na wengine, kushuhudia upendo wa Kristo na kuwa wanafunzi wamisionari. Usijiwekee kikomo kwa maarifa ya kinadharia pekee, bali ishi imani yako kwa uthabiti, wakipitia upendo wa Mungu katika maisha yao ya kila siku. Safari ya imani inaweza kuwa ndefu na wakati fulani ngumu, lakini wasivunjike moyo, maana Mungu yupo siku zote kuwaunga mkono. Kama vile nabii Isaya atukumbushavyo: “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja naww; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu na kukusaidia” ( Isa 41:10 ). Papa Leo alisema kuwa ni muhimu kumwona Mungu katika sala, katika mazoezi ya sakramenti, hasa katika upataji upya wa sakramenti ya Upatanisho, na katika maisha ya jumuiya, ili kukua katika imani na upendo.
Kwa njia hiyo kwa msaada na usaidizi wa wachungaji wenu, kaka na dada zenu wakubwa katika imani, na kufuata mfano wa watakatifu waliokabili magumu ya wakati wao, ninawatia moyo kuendelea kushikamana na Bwana Yesu. Sisi si Wakristo waliozaliwa; tunakuwa Wakristo tunapoguswa na neema ya Mungu. Hata hivyo, “mguso” huu unaonyeshwa kupitia chaguo letu lililofikiriwa kwa uangalifu na safari yetu ya kibinafsi. Bila mahitaji haya ya kweli, tutavaa chapa ya Wakristo, lakini Wakristo wa urahisi, tabia, au faraja. Tunakuwa Wakristo wa kweli tunapojiruhusu sisi wenyewe kuguswa kibinafsi katika maisha yetu ya kila siku kwa neno na ushuhuda wa Yesu. Kwa kuhitimisha Papa Leo alisema kuwa "katikati ya dhiki zenu, nyakati za upweke na ukame, kutokuelewana, taabu zenu, mioyo yenu na ikae mizizi ndani yake yeye aliye “njia, na kweli, na uzima” (Yn 14:6), chanzo cha amani yote, furaha na upendo.Asante! Tusali Baba Baba Yetu, Baraka na furaha ya Jubilei!