Papa Leo XIV: Wazee Ni Baraka na Neema! Ishara ya Matumaini! Mashuhuda wa Sala na Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku za usoni. Vijana wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanatenda tendo jema la huruma na mapendo kwa wazee wanaowazunguka. Upendeleo wa pekee utolewe kwa wazee wanaoishi peke yao au kwenye nyumba za kutunzia wazee, ambao kwa muda mrefu uliopita hawajapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki zao.
Vijana watambue na kuthamini nafasi na dhamana ya wazee katika jamii na kamwe wasiwaache kuelemewa na upweke hasi unaoweza kuwafanya wachungulie kaburi mapema pengine hata kabla ya wakati. Vijana wahakikishe kwamba, wanatumia uzoefu na mang’amuzi yao ili kuwaonjesha upendo kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii pale inaposhindikana kuwatembelea mubashara! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanawaalika kuwapongeza wazee kwa uwepo na ushiriki wao katika maisha na utume wa jamii. Upendo ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu utaweza kukua na kuzaa matunda. Hakuna familia inayoweza kukua na kustawi, ikiwa kama inasahau mizizi yake, yaani asili yake. Watoto na vijana wajifunze kutoka kwa wazee, ili hatimaye, mizizi yao iweze kuzama zaidi katika maisha yao ya kila siku.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 21 Julai 2025 amewatembelea na hatimaye kusalimiana na wazee wanaotunzwa kwenye Nyumba ya Mapumziko na Wazee ya “Santa Marta” iliyoko Castel Gandolfo, mjini Albano. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia wazee hao kwamba, wao kwa hakika ni ishara ya matumaini na mashuhuda wa sala na imani. Hawa ni wazee wenye umri kati ya miaka 80 hadi 101, kwa hakika wamekula chumvi nyingi. Amewashukuru kwa kukuza na kudumisha moyo wa sala, huduma na ukarimu na kwamba, Kristo Yesu anapenda kuwatembelea, ili hatimaye, kuonesha ukaribu wake na kuwafariji. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa sala, matumaini, imani na mapendo. Na kila mtu na kila familia, itatoa kile ambacho Mwenyezi Mungu katika wema na upendo wake wa daima amewakirimia waja wake. Sr. Eliana Martinelli, Mkuu wa Nyumba ya Mapumziko na Wazee ya “Santa Marta” anasema, wazee walifurahi sana kutembelewa na hatimaye, kusalimiana na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye pia alionesha furaha sana machoni pake. Hii inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV ni mtu ambaye hawezi kuficha hisia zake sana!