MAP

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 9 Julai 2025 akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 9 Julai 2025 akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote!

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 9 Julai 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, katika nyakati hizi ambako dunia inaendelea kuwaka moto kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia, athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, Nyaraka za Kitume za Hayati Baba Mtakatifu Francisko; “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na "Fratelli tutti": Mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume; “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anatoa mwelekeo wa ustaarabu mpya wa maisha unaojikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi; binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mazingira na kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa ili kuilinda, kuitunza na kuiendeleza. Kimsingi Waraka huu unazungumzia kwa muhtasari: mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kuitafakari dunia mintarafu jicho la Mungu, ili kuitunza dunia, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kupyaisha mahusiano kati ya mfumo wa maisha ya binadamu na mazingira.

Papa Leo XIV akiendesha Ibada ya Misa Takatifu: Utunzaji wa mazingira
Papa Leo XIV akiendesha Ibada ya Misa Takatifu: Utunzaji wa mazingira   (@Vatican Media)

Inasikitisha kuona kwamba, shughuli nyingi zinazofanywa na binadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na uwiano bora zaidi ili kazi ya uumbaji iweze kuleta mafao kwa binadamu, kwa leo na kwa jili ya vijana wa kizazi kipya. Kwa mwamini mazingira ni jambo takatifu linalonesha mahusiano makubwa kati ya Mungu na viumbe wake. Kumbe, maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie kuboresha mazingira na kamwe yasiwe ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha umaskini na majanga kwa watu na mali zao sehemu mbalimbali za dunia. Hapa kuna umuhimu wa kuwa na mwelekeo mpya katika kufikiri, kutenda na kuishi ili kupambana na kinzani za kimazingira na kijamii zinazoendelea kumwandama mwanadamu.

Waamini wakiwa na Papa Leo XIV baada ya Misa Takatifu
Waamini wakiwa na Papa Leo XIV baada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Waraka wa Kitume wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko “Laudate deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” ulichapishwa tarehe 4 Oktoba 2023, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na mwanzo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Waraka huu wa Kitume umechapishwa baada ya miaka minane tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Kumbe, Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi anasema kwamba, watu wengi wanaathrika sana mintarafu afya ya binadamu, kazi, upatikanaji wa rasilimali, makazi pamoja na uhamiaji wa nguvu. Haya ni matatizo ya kijamii yanayogusa na kutikisa na kusigina: utu, heshima, haki msingi na maisha ya binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani yamepelekea ongezeko la kiwango cha joto na matokeo yake ni mvua kubwa zinazoambatana na mafuriko na sehemu nyingine ukame wa kutisha. Ongezeko la kiwango cha joto duniani kunapelekea kuyeyuka kwa barafu na matokeo yake ni ongezeko la kina cha maji baharini. Kumekuwepo na upinzani pamoja na hali ya kuchanganyikiwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari hali ambayo kwa siku za usoni, itawalazimisha watu kuhama kutoka kwenye fukwe za bahari.

Laudato si! Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Laudato si! Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Ni katika muktadha wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 9 Julai 2025 akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, katika nyakati hizi ambako dunia inaendelea kuwaka moto kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia, athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, Nyaraka za Kitume za Hayati Baba Mtakatifu Francisko; “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni vyombo madhubuti katika kukuza na kudumisha mchakato wa utamaduni wa majadiliano, amani, haki jamii na udugu wa kibinadamu. Waraka unaonesha umuhimu wa dini kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa wote! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema licha ya dhoruba kali inayoendelea kutishia maisha ya mwanadamu, Kanisa kati kati ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linasimama kutangaza Injili ya matumaini, kwani waamini wamekutana na Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Asifiwe Mungu kwa ajili ya viumbe vyake
Asifiwe Mungu kwa ajili ya viumbe vyake   (@Vatican Media)

Kristo Yesu kwa nguvu za Kimungu anatuliza dhoruba, hii ni nguvu inayounda, inayomwezesha mtu kuwapo na kuonja maisha mapya. “Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii? Mt 8:27 Hili ni swali msingi linalowaondoa waamini kutoka katika mazingira ya hofu, woga na wasiwasi. Kristo Yesu yuko kando ya Ziwa la Galilaya, hapa ni mahali ambapo Kristo Yesu aliishi na kusali; ni mahali ambapo aliwaita Mitume wake wa kwanza, kutoka katika kazi na shughuli zao, akatangaza na kushuhudia uwepo angavu wa Ufalme wa Mungu. Kuna mwingiliano mkubwa wa eneo hili, musimu pamoja na maisha ya viumbe hai. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema: “Tunazungumzia kuhusu tabia ya moyo, ambayo huyaangalia maisha kwa umakini, ambayo ipo tayari kwa ajili ya mwingine bila kujali yatakayotokea, ambayo pia huupokea kila wakati kama zawadi itokayo kwa Mungu na kuuishi kikamilifu.” Laudato si 226. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwinjili Mathayo anatumia neno “Msukosuko mkuu baharini” “Seismos”, atalitumia neno hili tena wakati wa kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, anaendelea kushiriki historia na maisha ya waja wake. Kristo Yesu anatuliza dhoruba, huku akionesha nguvu zake katika maisha na wokovu dhidi ya nguvu zinazotishia usalama na maisha ya binadamu.

Simameni kidete kulinda mazingira nyumba ya wote
Simameni kidete kulinda mazingira nyumba ya wote   (@Vatican Media)

Kuhusu lile swali na msingi, Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika utenzi kwa Kristo Yesu, kichwa cha kila kiumbe anasema, “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.” Kol 1:15-16. Mitume wa Kristo Yesu katika muktadha wa hali na mazingira ya dhoruba kali, hawakuweza kukiri na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu. Lakini leo hii, Wafuasi wa Kristo Yesu wanaweza kutangaza na kukiri kwamba; “Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.” Kol 1:18. Haya ni maneno yanayowawajibisha waamini kuwa ni sehemu ya fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ndiye kichwa cha mwili huu yaani Kanisa.

Uharibifu wa mazingira ni kikwazo cha maendeleo endelevu
Uharibifu wa mazingira ni kikwazo cha maendeleo endelevu   (@Vatican Media)

Dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewadhaminisha wafuasi wake ni kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora, kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani na upatanisho; wawe ni wasikivu makini wa kilio cha Dunia Mama na Maskini kwa sababu kilio hiki kinafika na kugusa Moyo wa Mungu kwani hasira yetu ni hasira yake, kazi yetu ni kazi yake.”  Mzaburi anakiri kuhusu uweza wa Neno la Mungu akisema “Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi. Sauti ya Bwana ina nguvu, Sauti ya Bwana inaadhama.” Zab 29: 3-4. Hii ni sauti ambayo inaliwajibisha Kanisa kutekeleza wajibu wake wa kinabii, kwa kuendeleza mahusiano na mafungamano kati ya Muumba na viumbe vyake, ili kuleta mabadiliko, kutoka katika ubaya na kuelekea katika wema; kutoka katika ukosefu wa haki msingi za binadamu na kuzijeresha tena, kutoka katika mipasuko na hatimaye, kujenga umoja. Mwenyezi Mungu ni Muumbaji na ndiye asili ya uhai kwa viumbe vyote ambavyo Mtakatifu Francisko wa Assisi anaviita kuwa ni ndugu zake. Kimsingi maisha ya mwanadamu yapo katika uhusiano wa aina tatu: Uhusiano na Mwenyezi Mungu, Uhusiano na jirani na uhusiano na dunia, lakini kutokana na mpasuko ambao ni dhambi, uhusiano mwema ukaingia katika mgogoro.

Kanisa linatumwa kutangaza Injili ya matumaini
Kanisa linatumwa kutangaza Injili ya matumaini   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “Borgo laudato si” ni kazi ya ubunifu iliyotekelezwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuliwezesha eneo hili kuwa ni “maabara” ya kuweza kuishi kwa amani na utulivu na kwamba, hii ni dhamana ya kuganga na kuponya; na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho, kwa kuangalia njia mpya na zenye ufanisi katika utekelezaji wa mradi huu na kwamba Baba Mtakatifu Leo XIV ataendelea kuwapatia ushirikiano pamoja na kuwatia shime. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, ni katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambapo vitu vyote vilivyoumbwa vinapata hadhi kubwa. Neema inayoonekana dhahiri, ilipata njia bora zaidi ya kujidhihirisha pale ambapo Mwenyezi Mungu mwenyewe alijifanya kuwa mwanadamu na akajitoa kama chakula kwa ajili ya watu wake. Katika fumbo la Umwilisho Bwana Yesu alichagua kuufikia undani wa mwanadamu kwa njia ya sehemu ndogo sana ya maada. Yeye haji kutoka juu bali kutoka ndani, na anakuja ili tuweze kukutana naye katika ulimwengu wetu. Katika Ekaristi Takatifu, ulimwengu mzima unamshukuru Mungu. Rej. Laudato si 236. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa maneno ya Mtakatifu Augustino katika kurasa za mwisho za Maungamo yake, anayeunganisha vitu vilivyoumbwa na wanadamu katika sifa ya ulimwengu: Ee Bwana, "matendo yako yanakusifu hata sisi tunakupenda, na tunakupenda ili kazi zako zikusifu" (SAINT AUGUSTINE, Confessions, 833, XII). Na haya yawe ni maridhiano yanayoenezwa ulimwenguni kote.

Papa Leo XIV Borgo Laudato
09 Julai 2025, 15:32