MAP

Mkutano huu unajikita zaidi katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa Mkutano huu unajikita zaidi katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa 

Papa Leo XIV Ujumbe Kwa Wadominikani: Uinjilishaji wa Kina

Baba Mtakatifu Leo XIV amemwandikia barua, Padre Gerard Francisco Timoner III, OP., Mkuu wa Shirika la Wadominikani kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa wakuu wa kanda kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuanzia tarehe 17 Julai hadi tarehe 8 Agosti huko Cracovia, nchini Poland. Mkutano huu unajikita zaidi katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hadhira Nne”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alizaliwa huko mjini Calarogo, ambao kwa sasa mji huu unajulikana kama Caleruega huko nchini Hispania tarehe 8 Agosti 1170. Alifariki dunia tarehe 6 Agosti 1221 na kuzikwa kwenye Kanisa kuu la “San Domenico Jimbo kuu la Bologna nchini Italia. Papa Gregori IX tarehe 2 Julai 1234 akamtangazwa kuwa ni Mtakatifu. Ni muasisi wa Shirika la Wahubiri, maarufu kama Wadominikani, “Order of Preacher, OP.” Mama Kanisa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulijalia Kanisa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliyepyaisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili. Alitangaza Habari Njema ya Wokovu iliyokita mizizi yake katika huruma ya upendo wa Mungu, ukweli unaokoa na kama chemchemi ya nguvu ya wokovu. Alikazia utume, umoja, maisha ya Kijumuiya na umisionari wa kitume. Mtakatifu Dominiko wa Guzmán anatambulika kuwa ni Mhubiri wa Neema ya Mungu inayokita mizizi yake katika karama na utume wa Shirika la Wadominikani: Mapadre, Watawa na Waamini Walei bila kuvisahau vyama vya vijana. Kila mtakatifu alikirimiwa utume maalum katika maisha yake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, utakatifu na kuendelea kukazia umoja na maisha ya kijumuiya kwa kuyaishi kikamilifu mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Useja kamili, chachu ya mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hizi ni tunu msingi zilizowapambanua Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alianzisha Jumuiya ya wahubiri, waliopenda kusoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu, wakajikita katika maisha matakatifu na adili na hivyo wakawa kweli ni mashuhuda wa chemchemi ya maisha na ukweli wa Neno la Mungu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, Wadominikani wanaendelea kutoa changamoto kwa Wakristo kuwa kweli ni Mitume wamisionari, wanaokwenda pembezoni mwa jamii ili kutangaza na kushuhudia mwanga wa Injili na upendo wenye huruma kutoka kwa Kristo Yesu. Kiini cha Kanisa na ari na moto wa umisionari sanjari na ujenzi wa Kanisa la kisinodi unaopaswa kuendelea kuwaka!

Wadominikani wakishiriki mkutano mkuu wa Kanda
Wadominikani wakishiriki mkutano mkuu wa Kanda

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alitangaza Habari Njema ya Wokovu iliyokita mizizi yake katika huruma ya upendo wa Mungu, ukweli unaokoa na kama chemchemi ya nguvu ya wokovu. Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliguswa na mateso na mahangaiko na vifo vya watu wa Mungu, akauza baadhi ya mali zake ili kujenga kituo cha huduma ya upendo, ili kushuhudia upendo wa Kristo Yesu unaoganga na kuponya. Alikazia umoja wa ukweli unaosimikwa katika upendo, nguzo ya haki msingi za binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuendeleza urafiki na udugu wa kibinadamu, ili “kufyekelea” mbali mifumo tenge ya uchumi na siasa, tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani. Waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika utakatifu, haki na amani. kibinadamu, kama kielelezo cha utawala bora. Ni utawala shirikishi uliofumbatwa katika mang’amuzi na maamuzi kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Shirika. Udugu wa Kiinjili ni ushuhuda wa unabii wa Mpango wa Mungu kama chombo cha umoja na upatanisho wa familia ya binadamu. Na huu ni utambulisho makini wa karama ya Wadominikani na kama sehemu ya mchakato wa kuragibisha upyaisho wa maisha ya Kikristo na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu mamboleo! Mtakatifu Dominiko wa Guzmán na Mtakatifu Francisko wa Assisi walitambua kwamba, kutangaza Injili kunapaswa kwenda sanjari na ushuhuda wa ujenzi wa jumuiya ya kitawa inayosimikwa katika umoja wa kidugu na utume wa kimisionari. Watakatifu, wasanii na wasomi wa nyakati mbalimbali wametambua na kuthamini mchango wa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán. Kifodini cha baadhi ya Wadominikani ni mahubiri ya nguvu, yenye mvuto na mashiko. Hawa ni watu waliosimama kidete kutangaza Injili ya Kristo pembezoni mwa jamii, bila kusahau kuwashirikisha vijana ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika utume wa uinjilishaji wa kina ni jambo linalopewa kipambele cha kwanza kwa nyakati hizi.

Wadominikani: Mahujaji wa matumaini na watu wa Mungu
Wadominikani: Mahujaji wa matumaini na watu wa Mungu

Mama Kanisa anawashukuru Wadominikani waliojielekeza zaidi katika masomo ya taalimungu kwa kufafanua mafumbo ya imani kwenye vyuo mbalimbali vya taalimungu Barani Ulaya. Ni masomo, malezi na makuzi yanayokita mizizi yake katika: Maandiko Matakatifu, Taalimungu na Elimu dunia ili kusaidia mchakato wa majadiliano katika ukweli kwa ajili ya huduma ya Ufunuo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Wadominikani wamekuwa mstari wa mbele katika sekta ya elimu kwa kuanzisha taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, ili kusaidia majadiliano kati ya akili na imani, ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mchango mkubwa ambao umetolewa na Wadominikani kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake. Mama Kanisa anawaombea ili wadumu katika uaminifu wa karama ya Mwanzilishi wa Shirika lao, amana na urithi wa karama ya mwanzilishi wao, pamoja na ongezeko la miito mitakatifu ya kipadre na kitawa. Baba Mtakatifu Leo XIV amemwandikia barua, Padre Gerard Francisco Timoner III, OP., Mkuu wa Shirika la Wadominikani kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa wakuu wa kanda kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuanzia tarehe 17 Julai hadi tarehe 8 Agosti huko Cracovia, nchini Poland. Mkutano huu unajikita zaidi katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hadhira Nne” yaani wale watu ambao bado hawamjui Kristo Yesu; Waaminifu wa Kristo, Wale ambao wamejitenga na Kristo na Kanisa; sanjari na Vijana katika hali zote hizi; ni muhimu sana kwa wakati unaofaa.” Mama Kanisa anasema, Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu.

Wadominikani katika Uinjilishaji wa kina
Wadominikani katika Uinjilishaji wa kina

Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujenga Kanisa na Kisinodi na Kimisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika wajumbe wa mkutano huu, kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu fursa ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kupyaisha matumaini yao ambayo kamwe hayadanganyi. Itakumbukwa kwamba, Tamko la Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Yote haya yawawezeshe kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kusimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Anawaalika kumsikiliza zaidi Roho Mtakatifu ambaye anaendelea kuliongoza Kanisa katika utimilifu wa ukweli wote. Rej. Yn 16:13. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, hii ni fursa kwa Wadominikani kuendelea kujisadaka na kujizatiti zaidi katika kulihudumia Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa kwa njia ya maisha ya Kiinjili kama alivyofanya Mtakatifu Dominiko wa Guzmán. Uzoefu na mang’amuzi yao pamoja na udugu wa kibinadamu na maisha ya sala yaendelee kuimarisha vifungo vya ushirika na umoja wa Shirika, mambo yanayowaunganisha kama Wadominikani na hivyo kuwatia moyo kuishi kwa ukamilifu zaidi wito wao kama wahubiri na wanatafakari wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Wadominikani, wawe waaminifu kwa karama na hali ya maisha yao ya kiroho ndani kiroho. Baba Mtakatifu Leo XVI amewakabidhi washiriki wa mkutano huu chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hatimaye, Papa Leo XVI akawapatia baraka zake za kitume.

Papa Leo XIV Wadominikani
24 Julai 2025, 15:32