MAP

Papa Leo XIV amelaani matumizi ya baa la njaa kama silaha ya kivita katika ujumbe kwa FAO katika mkutano wake wa 44. Papa Leo XIV amelaani matumizi ya baa la njaa kama silaha ya kivita katika ujumbe kwa FAO katika mkutano wake wa 44.  (AFP or licensors)

Papa Leo XIV Ujumbe Kwa FAO: Alaani Matumizi ya Njaa Kama Silaha za Vita

Papa: Kuna watu wanaoteseka vibaya na wanatamani kuona mahitaji yao mengi yakitimizwa kwasababu hawawezi kuyatimiza wenyewe. “Janga la kudumu la njaa na utapiamlo, linaloendelea katika nchi nyingi leo, ni la kusikitisha na la kuaibisha hata zaidi tunapotambua kuwa, ingawa dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa wanadamu wote, na licha ya ahadi za kimataifa kuhusu usalama wa chakula, maskini wengi duniani bado hawapati mkate wao wa kila siku."

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linafanya mkutano wake wa 44 mjini Roma kuanzia Juni 28 hadi Julai 4 2025. Papa Leo XIV alishukuru kupata fursa ya kuzungumza kwa mara ya kwanza na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na washiriki wa mkutano huo, huku FAO ikisherehekea miaka 80 tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kupambana na uhaba wa chakula na utapiamlo duniani. Katika ujumbe wake, Papa Leo XIV alisema Kanisa linaunga mkono juhudi zote za kumaliza aibu ya baa la njaa duniani akimkumbuka Yesu ambaye aliulisha umati uliokuwa umefika kumsikiliza. “Kanisa linaunga mkono kila juhudi zinazolenga kumaliza aibu ya njaa duniani, likiongozwa na moyo, ari na nia ileile ya Yesu Kristo, ambaye kama tunavyosoma katika Injili, alipoona kundi kubwa linamfuata kusikiliza Neno lake, alihangaika kwanza kuwapa chakula, na kwa sababu hiyo akawaambia wanafunzi wake wajishughulishe kutatua tatizo hilo, kisha akabariki mikate na samaki ikaongezeka (rej. Yn 6:1-13).

Papa Leo XIV alaani matumizi ya njaa kama silaha za kivita
Papa Leo XIV alaani matumizi ya njaa kama silaha za kivita   (AFP or licensors)

Hata katika simulizi hili la muujiza wa kuongezeka kwa mikate (rej. Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:12-17; Yn 6:1-13), tunaelewa kuwa muujiza wa kweli uliofanywa na Kristo ulikuwa ni kuonesha kwamba njia ya kushinda njaa iko zaidi katika ukarimu wa kutoa, kushirikiana kwa moyo kutatua tatizo kuliko uchu na tamaa ya kujilimbikizia mali.  Ingawa kuna hatua fulani zimepigwa, hali ya usalama wa chakula duniani inaendelea kuzorota, jambo linalofanya kufikia lengo la “Njaa Sifuri” la Ajenda ya 2030 kuonekana kuwa jambo lisilowezekana. Hii ina maana kuwa bado tuko mbali na kutimiza dhamira iliyosababisha kuanzishwa kwa Shirika hili mnamo mwaka wa 1945,” alieleza Papa Leo XIV. Pia ameiambia FAO kuwa, Kuna watu wanaoteseka vibaya na wanatamani kuona mahitaji yao mengi yakitimizwa kwasababu hawawezi kuyatimiza wenyewe. “Janga la kudumu la njaa na utapiamlo, linaloendelea katika nchi nyingi leo, ni la kusikitisha na la kuaibisha hata zaidi tunapotambua kuwa, ingawa dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa wanadamu wote, na licha ya ahadi za kimataifa kuhusu usalama wa chakula, maskini wengi duniani bado hawapati mkate wao wa kila siku,” alisema Baba Mtakatifu Leo XIV.

Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO: Njaa bado ipo!
Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO: Njaa bado ipo!   (AFP or licensors)

Kwa upande mwingine, Papa Leo XIV ameeleza namna njaa inavyotumika kama silaha ya vita. Kuwafisha kwa njaa watu wa kawaida ni njia ya gharama nafuu sana ya kuendesha vita. Hii ni kwa sababu leo vita nyingi hazipiganwi tena na majeshi ya kitaifa, bali na makundi ya raia wenye silaha chache, hivyo kuchoma mashamba, kuiba mifugo na kuziba misaada ni mbinu zinazotumika zaidi ili kuwatawala watu wasio na uwezo wa kujilinda. Katika muktadha huu, vitu vya kwanza kulengwa ni njia za usambazaji maji na mawasiliano. Wakulima hawana uwezo wa kuuza mazao yao katika maeneo yenye vitisho vya vurugu na mfumuko wa bei unapaa sana. Hili linasababisha watu wengi kufa kwa njaa, huku viongozi wa kisiasa wakiendelea kunufaika kwa rushwa na ukwepaji wa adhabu. Hivyo basi, ni wakati wa dunia kuweka mipaka wazi ya kueleweka na inayokubalika kwa pamoja ili kuwaadhibu wahusika wa unyanyasaji huu na kuwafikisha mbele ya haki. “Migogoro ya kisiasa, vita na misukosuko ya kiuchumi vinachangia sana kuzorota kwa hali ya chakula duniani. Vinazuia misaada ya kibinadamu, vinadhoofisha uzalishaji wa kilimo wa ndani na kuwanyima watu si tu chakula, bali pia haki ya kuishi maisha ya heshima na fursa. Ubinafsi na kutojali vinapaswa kuwekwa kando kwa ajili ya kutoa nafasi ya mazungumzo ya pamoja na kuelewana, ili amani na utulivu viweze kuruhusu jamii kujenga mifumo imara ya chakula na kilimo,” Papa leo ameisisitiza FAO.

Vita na kinzani za kisiasa zinachangia sana kukua kwa baa la njaa
Vita na kinzani za kisiasa zinachangia sana kukua kwa baa la njaa   (AFP or licensors)

Wakati huo huo, mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya chakula vimeunganishwa kwa karibu, maana uharibifu wa kimoja unaathiri pia kingine. Huwezi kutenganisha mabadiliko tabianchi na mifumo ya chakula duniani. Ukosefu wa haki za kijamii unaosababishwa na majanga ya asili na kupotea kwa bioanuwai alisema lazima urekebishwe ili kufanikisha mpito wa haki wa kiikolojia ambao unaweka mazingira na watu katikati. Alitoa wito wa kulinda mifumo ya ikolojia kupitia hatua za pamoja dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa moyo wa mshikamano, kwani rasilimali za dunia yetu zinapaswa kutumika kuhakikisha kila mtu anapata usalama wa chakula na lishe bora. Papa Leo XIV alihuzunishwa na jinsi rasilimali za kifedha na teknolojia za kisasa zinavyotumika kutengeneza silaha na biashara ya silaha. Matokeo yake, itikadi zenye mashaka zinapewa kipaumbele, huku mahusiano ya kibinadamu yakidorora yakiua mshikamano na kuondoa undugu na urafiki wa kijamii. Katika hitimisho, Papa Leo XIV aliwaalika wote kuwa wajenzi wa amani, wanaofanya kazi kwa ajili ya manufaa ya wote kwa kuweka kando maneno matupu na kushughulikia tatizo la njaa kwa nia ya kweli ya kisiasa. “Ili kufanikisha lengo hili tukufu alisema Papa Leo XIV nataka kuwahakikishia kuwa Vatican daima itahudumia sababu ya maelewano kati ya Mataifa na haitachoka kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia kubwa ya Mataifa hasa kwa wale wanaoteseka zaidi na wanaokumbwa na njaa na kiu.”

Papa Leo XIV FAO
01 Julai 2025, 15:58