Papa Leo XIV kwa vijana wa Peru:Bwana ametuchagua kuwa sehemu ya familia kubwa ya Kanisa!
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana mjini Vatican Jumatatu tarehe 28 Julai 2025 na kikundi cha wajumbe vijana kutoka nchini Peru katika fursa ya kushiriki Jubilei ya Vijana, Awali ya yote akianza hotuna aliwashukutua sana huku akiwakaribisha katika nyumba ya Petro, ambapo walifika kama mahujaji wa matumaini, na wote ni mahujaji wa matumaini, wakifika na kukutana na maelfu na maelfu ya vijana wengine na kusherehekea Jubilei pamoja. Papa Leo XIV kwa kuwaona alifikiria pia familia zao na watu wengi katika jumuiya za parokia zao ambao kwa hakika wamewasaidia, kwa kujitolea na kazi kubwa, kufanikisha safari hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu. Kwa njia hiyo aliwasalimia wote na kwa shukrani na furaha.
Katika mkesha wa tukio hili muhimu kwa vijana duniani kote, Injili ya Misa ya leo(28 Julai ) inatupatia mwanga wa pekee. Hii ni mifano miwili inayotusaidia katika safari yetu ya Kikristo: ya kwanza inazungumza juu ya mbegu ndogo ya haradali, na ya pili ya chachu kidogo (taz. Mt 13:31-35). Papa Leo alisisitiza kuwa kama tunavyoona hivi ni vipengele viwili ambavyo tunaweza kuviita karibu visivyo na maana; hata hivyo, kwa nguvu ya maisha waliyobeba ndani yao, wanaweza kubadilishwa, kukua, na kutumikia kusudi ambalo kwa ajili yake waliumbwa. Sisi pia ni wadogo, lakini hatuko peke yetu; Bwana ametuchagua sisi kuwa sehemu ya familia kubwa, yaani familia ya Kanisa.” Tukiingizwa ndani yake katika Kristo, kama matawi ya mizabibu kwenye mzabibu, tunaweza kukua na kuzaa matunda, tukisaidiwa na neema ya Bwana. Mtakatifu Augustino anazungumza juu ya mifano hii miwili katika ufafanuzi wake juu ya moja ya zaburi, Zaburi 68, na pia anaelezea uwezo wa vitu vidogo, ambavyo, vinapokua, vinatia mizizi ndani ya watu, watu wa Mungu walioenea duniani kote (taz. Tafakari ya Zaburi 68, I, 1).
Katika siku hizi za furaha za Jubilei ya Vijana, Papa Leo XIV alisema kuwa wote watakuwa na uzoefu mzuri wa kuhisi kuwa sehemu ya watu wa Mungu, sehemu ya Kanisa la kiulimwengu, ambalo linakumbatia na kuzunguka dunia nzima, bila ubaguzi wa rangi, lugha, au taifa; kueneza kama kichaka cha haradali na kuchachuka kama chachu. Papa Leo XIV aliwataka kila mara waweke mioyoni mwao kila kitu wanachopitia siku hizi, lakini wasihifadhi wao wenyewe tu. Hili ni muhimu sana: kile watakachopitia jijini Roma, kisiwe chao binafsi: “Lazima tujifunze kushirikisha. Tafadhali, haya yote yasibaki kuwa kumbukumbu tu, kama picha zingine nzuri, yaani kitu cha zamani,” aliwasihi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba wakati watakaporudi nchini Peru, wataweza kujaza nchi hizo furaha na nguvu ya Injili, kwa Habari Njema ya Yesu Kristo. Watu wote wanaokutana nao waone ndani yako uso wa Kristo ambaye anapenda na kujitoa, ambaye anabaki kuwepo ndani ya kila mbatizwa.
Kwa hiyo, watumikie kwa uhuru, katika mambo ya kila siku, katika mambo madogo, katika mambo yaliyofichwa, kwa sababu wamepata furaha ya kupendwa kwanza, na kwa sababu wamepokea kila kitu bure kutoka kwa Baba yetu, Mungu. Mikoba watakayoambatana nayo siku hizi, wakiwa wamebeba yale muhimu tu, ni ishara ya utume wanaokabidhiwa na Papa hivi leo hii yaani “ muwe wamisionari popote mwendapo, muwe uwazi wa uwepo wa Bwana, kama walivyokuwa watakatifu wetu wapendwa wa Peru.” Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa waanajua kwamba Papa Francisko daima alizungumza juu ya Peru kama "nchi takatifu," yenye watakatifu wengi, lakini sio tu kutoka zamani, lakini pia watakatifu wa leo hii na kesho. Mungu awabariki na Mama yetu wa Uinjilishaji awalinde daima. Asante. Kristo anaishi!