ĐÓMAPµĽş˝

2025.07.25 Papa na Washiriki wa Kozi ya Waseminari na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Ndugu wa Mtakatifu Xaveri. 2025.07.25 Papa na Washiriki wa Kozi ya Waseminari na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Ndugu wa Mtakatifu Xaveri.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:kujali malezi ya upadre na umisionari kwa nchi zilizojeruhiwa!

Papa akikutana na Wafundaji wa kozi ya Malezi ya mapadre iliyoandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Regina Apostolorum na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Xaveri,mjini Vatican,Julai 25,aliwahimiza mambo matatu:kusitawisha urafiki na Yesu kwamba ndio msingi wa nyumba unaopaswa kuwekwa katikati ya kila wito na utume wa kitume.Pili:kuishi udugu mzuri na wenye upendo kati yetu na tatu kushiriki utume na wabatizwa wote!

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 25 Julai 2025 alikuwa na furaha ya kukutana katika hitimisho la matukio mawili muhimu jijini Roma na Wafundaji wa Kozi ya Walezi wa Seminari iliyohamasishwa kwa miaka mingi na Taasisi ya Kipapa ya Regina Apostolorum na Wajumbe washiriki wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Ndugu Waxaveri. Kwa hakika Papa Leo alisema kuwa,  haya ni matukio mawili tofauti na kwamba tunaweza kutambua jambo muhimu la pamoja linalowaunganisha, hata kwa njia tofauti na kwamba "tumeitwa kuingia katika mvuto wa utume na kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji. Wito huu unadai kwa wote, wahudumu wa daraja na waamini walei, kwa malezi thabiti na ya kina. Malezi haya hayakomei kwa ujuzi mdogo wa utambuzi, bali yanapaswa kulenga kubadilisha ubinadamu wetu na hali yetu ya kiroho ili ichukue namna ya Injili, na ili nia ile ile iliyokuwa ndani ya Kristo Yesu”(Flp 2:5) ipate nafasi ndani yetu.

Picha ya Pamoja na Papa wafundaji wa seminari na shirika la Xaveri
Picha ya Pamoja na Papa wafundaji wa seminari na shirika la Xaveri   (@Vatican Media)

Papa Leo aliendelea kukazia kwa wasimamizi, wale wanaohusika na malezi, na Ndugu wa shirika la Xaveri, ambao hasa wamejitolea kwa ajili ya Missio ad gentes,yaani  utume wa watu, kuwapa jambo la kufikiria.  Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Wakleri liliandaa mkutano wa kimataifa wa mapadre wenye mada: "Furaha ya Mapadre." Kwa njia hiyo alisema “Tunaweza pia kusema, hata hivyo, kwamba lazima sote tuambukizwe na furaha ya Injili, na kwa hiyo tunaweza kuzungumza juu ya Wakristo wenye furaha, wanafunzi wenye furaha, na wamisionari wenye furaha.” Ili tumaini hili lisibaki kuwa kauli mbiu, malezi ni muhimu. “Nyumba” ya maisha yetu na safari yetu, iwe ya kikuhani au ya walei, lazima iwekwe juu ya “mwamba” (rej. Mt,  7:24-25), yaani, juu ya misingi imara inayotuwezesha kustahimili dhoruba za kibinadamu na za kiroho ambazo hata maisha ya Mkristo, Padre na mmishenari hayasamehewi,” Papa alisisitiza. Kwa kuendelea aliuliza: Je, tunajengaje nyumba juu ya mwamba?

Kwa njia hiyo Papa alitoa mawazo matatu madogo kwa ufupi. La kwanza ni  kusitawisha urafiki na Yesu. Huu ndio msingi wa nyumba, unaopaswa kuwekwa katikati ya kila wito na utume wa kitume. Papa alisema kuwa ni lazima binafsi tuonjeshe urafiki wa karibu na Bwana, tukiwa tumetazamwa, kupendwa, na kuchaguliwa Naye bila sifa na kupitia neema safi, kwa sababu kimsingi ni uzoefu wetu huu ambao tunasambaza katika huduma: Tunapowazoeza wengine kwa ajili ya maisha ya ukuhani na wakati, katika wito wetu mahususi, tunatangaza Injili katika nchi za misheni, kwanza tunasambaza uzoefu wetu wa kibinafsi wa urafiki na Kristo, ambao unang'aa kwa njia yetu ya kuwa, mtindo wetu, ubinadamu wetu, na uwezo wetu wa kusitawisha uhusiano mzuri." Papa akiendelea alisema "Akikumbuka Waraka wa Evangelii Nuntiandi wakati wa Katekesi, Papa Francisko alithibitisha kuwa: "Uinjilishaji ni zaidi ya kusambaza mafundisho na maadili tu. Ni shuhuda wa kwanza kabisa [...], shuhuda wa kukutana kibinafsi na Yesu Kristo, Neno lenye Mwili ambamo ndani yake wokovu ulitimizwa [...]. Si kusambaza itikadi au 'fundisho' kuhusu Mungu, hapana. Ni kupitisha Mungu ambaye anaishi ndani yangu" (Katekesi Machi 22, 2023).

Papa Leo XIV akiwa na wafundaji wa Seminari na shirika la Xaveri
Papa Leo XIV akiwa na wafundaji wa Seminari na shirika la Xaveri   (@Vatican Media)

Hii ina maana ya safari endelevu ya uongofu. Walezi na wale wanaowajali wasisahau kwamba wao wenyewe wako katika safari ya uwongofu wa Kiinjili unaoendelea; wamisionari, wakati huo huo, wasisahau kwamba wao daima ni wapokeaji wa kwanza wa Injili, wa kwanza kuinjilishwa.Na hii ina maana ya kujishughulisha mara kwa mara, kujitolea kuzama ndani ya mioyo yetu wenyewe na kutazama hata vivuli na vidonda vinavyotutia alama, ujasiri wa kuacha vinyago vyetu, kusitawisha urafiki wa karibu na Kristo. Hivyo, tutajiruhusu wenyewe kubadilishwa na maisha ya Injili na kuwa wanafunzi wa kimisionari halisi.

Kipengele cha pili: kuishi udugu mzuri na wenye upendo kati yetu. Baba Mtakatifu Francisko alipozungumzia maisha ya kipadre na migogoro inayopaswa kuzuiwa, alipenda kukazia mambo manne ya ukaribu: na Mungu, na Askofu, kati ya mapadre, na watu (rej. Hotuba kwa Washiriki katika Kongamano la “Kwa Taalimungu Msingi wa Ukuhani,” Februari 17, 2022). Kwa maana hiyo, Papa Leo XIV alisema "ni muhimu kujifunza kuishi kama ndugu kati ya mapadre, na pia katika jumuiya za kitawa na pamoja na maaskofu na wakubwa wetu; tunapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kushinda ubinafsi na hamu ya kuwashinda wengine, ambayo inatugeuza kuwa washindani, kujifunza hatua kwa hatua kujenga uhusiano mzuri na wa kidugu wa kibinadamu na wa kiroho. Kimsingi, Papa amekazia kusema kuwa, kila mtu anakubaliana juu ya hilo, lakini kiukweli, bado kuna njia ndefu ya kutembea."

Papa akitoa Baraka
Papa akitoa Baraka   (@Vatican Media)

Jambo la tatu na la mwisho ni: kushiriki utume na wabatizwa wote. Katika karne za mwanzo za Kanisa, ilikuwa ni kawaida kwa waamini wote kujiona kama wanafunzi wamisionari na kujitoa kibinafsi kama wainjilishaji. Na huduma iliyowekwa wakfu ilikuwa katika huduma ya misheni hiyo iliyoshirikishwa na wote. Leo hii tunahisi sana haja ya kurejea katika ushiriki huu wa wabatizwa wote katika ushuhuda na utangazaji wa Injili. Katika nchi ambazo wao kama Waxaverian, wanatekeleza utume, bila shaka watakuwa wamejionea wenyewe jinsi ilivyo muhimu kufanya kazi pamoja na dada na kaka wa jumuiya hizo za Kikristo. Wakati huo huo, Papa Leo XIV alipenda kuwaambia Walezi kwamba mapadre lazima wafundishwe kwa hilo kuwa: wasijifikirie kama viongozi wapweke, wasichukue ukuhani waliowekwa wakfu kwa hisia ya ubora. Tunahitaji mapadre wenye uwezo wa kupambanua na kutambua ndani ya kila mtu neema ya Ubatizo na karama zinazobubujika kutoka humo, pengine hata kuwasaidia watu kufunguka kwa karama hizo, ili kupata ujasiri na ari ya kujihusisha na maisha ya Kanisa na jamii.

Kwa hakika, hii ina maana kwamba, maandalizi ya mapadre wajao yanapaswa kuzamishwa zaidi katika uhalisia wa Watu wa Mungu na kutekelezwa kwa mchango wa washiriki wake wote: mapadre, walei, na watu waliowekwa wakfu, wanaume na wanawake. Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV aliwashukuru, kwa nafasi hiyo, lakini zaidi ya yote aliwashukuru kwa utumishi wao kwa kujali malezi ya kipadre, na kwa ajili ya utume wao wa kueneza Injili katika nchi zilizojeruhiwa mara nyingi na zinazohitaji tumaini la Injili.  Papa amewahimiza waendelee na safari yao. Bikira Maria awasindikize na kuwaombea! 

Papa na Wafundaji wa Waseminari na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Xaveri
25 Julai 2025, 13:47