ŠÓMAPµ¼ŗ½

Papa Leo XIV anawaalika Makatekista kupyaisha ufahamu na upendo wao kwa Kristo Yesu, wakuze hamu ya kumtangaza na kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Papa Leo XIV anawaalika Makatekista kupyaisha ufahamu na upendo wao kwa Kristo Yesu, wakuze hamu ya kumtangaza na kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. 

Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Chanzo na Kilele Cha Katekesi: Atangazwe na Kushuhudiwa

Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Makatekista kupyaisha ufahamu na upendo wao kwa Kristo Yesu, wakuze hamu ya kumtangaza na kumshuhudia; wawe tayari kueneza Injili yake na kuwaongoza watu katika imani. Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Padre Mario Segura Bonilla. Kristo Yesu ni chanzo na kilele cha katekesi yote, muhtasari wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama mhutasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu.

Shirikisho la Makatekista Amerika ya Kusini
Shirikisho la Makatekista Amerika ya Kusini

Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waandaaji na washiriki wa Mkutano wa Kawaida wa XIII wa Shirikisho la Makatekista Amerika ya Kusini ā€œSociedad de Catequetas Latinoamericanosā€ (Scala), uliofunguliwa Jumatatu tarehe 7 na kuhitimishwa rasmi, Ijumaa tarehe11 Julai 2025 huko Asunción, mji mkuu wa Paraguay, kupyaisha ufahamu na upendo wao kwa Kristo Yesu, wakuze hamu ya kumtangaza na kumshuhudia; wawe tayari kueneza Injili yake na kuwaongoza watu katika imani. Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Padre Mario Segura Bonilla.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Makatekista nchini Brazili
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Makatekista nchini Brazili

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mkutano huu ni fursa ya kumtfakari Kristo Yesu, kama kiini na hatima ya Katekesi yote. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wajumbe wa mkutano huu kupyaisha ufahamu na upendo wao kwa Kristo Yesu, wakuze hamu ya kumtangaza na kumshuhudia; wawe tayari kueneza Injili yake na kuwaongoza watu katika imani. Wajikite katika uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wa maisha amini na adili. Kiini cha Katekesi ni Kristo Yesu anayeweza kuwaingiza waamini katika mapendo ya Baba ndani ya Roho Mtakatifu na kuwafanya washiriki uzima wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kiini cha Katekesi ni Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kutokana na elimu hii ya upendo kwa Kristo Yesu inazaliwa tamaa ya kutangaza na kueneza Injili, kuwaongoza wengine kukubali imani katika Kristo Yesu na hivyo kuwasaidia waamini kuifahamu vyema zaidi imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na ni Bwana; mambo yanayojidhihirisha katika Fumbo la Umwilisho na hatimaye katika Fumbo la Pasaka. Rej. KKK 426-429. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka wajumbe hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema, na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Katekesi Amerika ya Kusini
10 Julai 2025, 16:16