Papa Leo XIV anaomboleza Vifo vya Watu Kutokana na Janga la Moto Nchini Iraq
Na Sarah Pelaji, -Vatican
Zaidi ya watu 60 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa uliozuka usiku wa tarehe 16 Julai 2025 katika jengo la ghorofa tano la kibiashara lililokuwa na mgahawa na soko la bidhaa, ambalo lilikuwa limefunguliwa kwa siku saba tu zilizopita. Baba Mtakatifu Leo XIV ametuma ujumbe wa telegramu uliotiwa saini na Kardinali Pietro Parolini Katibu Mkuu wa Vatican kutokana na huzuni kubwa aliyoipata baada ya kusikia taarifa za moto mkubwa uliotokea mjini Kut, Iraq, na kusababisha vifo na majeruhi wengi. Papa Leo XIV amewahakikishia wote walioathirika na janga hilo mshikamano wake wa kiroho.
Kupitia kwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Papa Leo XIV ameelezea huzuni yake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, na kuwaombea wote waliojeruhiwa wapate nafuu ya haraka. Papa Leo XIV amewakabidhi marehemu wote katika huruma ya Mungu na ameendelea kuwaombea wafanyakazi wa dharura wanaotoa msaada kwa waathirika huku akiwaombea baraka za Mungu za nguvu, faraja na amani. Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq ilisema Vifo vimekuwa vya zaidi ya watu 60 vilitokana na kukosa hewa katika moto huo uliotokea Jumatano jioni ambapo bado miili ya watu 14 iliyoteketea vibaya bado haijatambuliwa.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, timu za ulinzi wa raia zimefanikiwa kuwaokoa zaidi ya watu 45 waliokuwa wamekwama ndani ya jengo. Licha ya kuwa moto umedhibitiwa, bado juhudi za kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana waliokuwemo kwenye jengo hilo zinaendelea. Kutokana na moto huo Gavana wa al Kut, Mohammed al-Mayyeh ametangaza siku tatu za maombolezo. Amesema chanzo cha moto bado kinaendelea kuchunguzwa lakini mmiliki wa jengo amefunguliwa kesi. Hata hivyo hakukutolewa ufafanuzi wa madai ya kesi hiyo.