Papa Leo XIV Akutana na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume: Kumfuasa Kristo Kwa Karibu
Na Sarah Pelaji, -Vatican
Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujenga Kanisa na Kisinodi na Kimisionari.
Papa Leo wa XIV amekutana na watawa wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume wanaoshiriki katika maadhimisho ya mikutano yao mikuu ya mashirika, kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Jumamosi tarehe 12 Julai 2025 ambako anapumzika kwa likizo yake ya kipindi cha kiangazi. Ingawa Mapapa kwa kawaida huwa na mikutano michache wakati wa likizo yao katika Ikulu hiyo ndogo iliyopo kando ya Ziwa kusini mashariki mwa Roma, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwapokea washiriki wa Mikutano Mikuu ya Mashirika yafuatayo: Taasisi ya Kipapa ya Utume wa Nchi za Nje (P.I.M.E.); Walimu wa Kidini wa Filipino, Walimu wa Dini wa Venerini, Mabinti wa Kanisa, Masista wa Kisalazi wa Moyo Mtakatifu na Masista Wafrancisko wa Mtakatifu Angela (Wafrancisko wa Angela).
Baba Mtakatifu Leo XIV alianza kwa kuwashukuru kwa kazi yao na uwepo wao wa uaminifu katika maeneo mengi duniani, akigusia waasisi wao waliokuwa watii kwa maongozi na matendo ya Roho Mtakatifu, waliowaachia karama mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Papa alibainisha kuwa Mashirika yao yanaakisi vipengele vinavyotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wao kwa watu wa Mungu akitaja hasa kutoa nafsi zao kwa kuungana na sadaka ya Kristo Yesu; Utume wa uinjilishaji kwa watu wa Mataifa (ad gentes), upendo kwa Kanisa uliolindwa na kurithishwa na malezi pamoja na elimu kwa vijana wa kizazi kipya. Vipengele hivi, alisema, ni njia mbalimbali zinazoendeshwa na uhalisia mmoja wa milele, yaani upendo wa Mungu kwa binadamu. Papa Leo XIV alitambua kuwa kila Shirika limekuwa na mitazamo maalum ya kutafakari urithi waliorithi, ili kuupyaisha kwa kusma alama za nyakati kwa njia ya sala na kusikiliza kwa dhati.
Papa Leo XIV akinukuu maneno ya Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliyesema kwamba, ni Roho Mtakatifu ambaye kupitia michango ya wengi chini ya uongozi wa viongozi wa Kanisa, husaidia Jumuiya ya Kikristo kutembea katika upendo kuelekea ukweli kamili. Katika muktadha huu, Papa alisisitiza umuhimu wa kufufua roho halisi ya kimisionari, kuiga moyo wa Kristo Yesu, kutegemea tumaini lao kwa Mwenyezi Mungu, kuendelea kuwasha moto wa Roho Mtakatifu mioyoni mwao, kukuza amani na kuhimiza uwajibikaji wa kichungaji katika Makanisa ya mahalia. Jambo hilo litasaidia kuthamini amana na utajiri wa kuwa Jumuiya hasa kama watawa walio kwenye safari ile ile ya kumfuata Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi.
“Jambo hili lifufue na kuimarisha ndani yetu sote ufahamu na furaha ya kuwa Kanisa,” alisema Papa Leo XIV huku akieleza matumaini yake kuwa jambo hili litawasaidia katika maamuzi katika vikao vyao mbalimbali vya chapta, kufikiri kwa ujasiri kama kufikia matarajio ya jumuiya zenu na Kanisa kwa ujumla zaidi ya matarajio yenu binafsi.” Mintarafu mpango wa wokovu, Papa Leo XIV alieleza kuwa ni mpango ambao Mwenyezi Mungu anatamani kuwarudisha wanadamu wote kwake kama familia moja kubwa. Kama taa ndogo zisizozima, aliwahimiza kusaidia kuchochea mwangaza wa Kristo usiozimika kamwe kuenea duniani kote. Kabla ya kutoa Baraka yake ya Kitume, Papa Leo XIV aliwaalika watawa hao kuungana naye kumwomba Mwenyezi Mungu kwa pamoja, ili awafanye watii kwa sauti ya Roho Wake Mtakatifu, ambaye hufundisha mambo yote na ambaye bila msaada wake katika udhaifu wa kibinadamu hawajui hata namna ya kusali ipasavyo. Hotuba hiyo ilihitimishwa kwa wito wa pamoja wa kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie katika udhaifu wao, kwa kuwa bila msaada wake, hata sala za wakristo haziwezi kuwa kamili (rej. Rum 8:26). Viongozi hao walipewa baraka maalum na shukrani kwa huduma yao ya uaminifu katika maeneo mbalimbali duniani.