Papa Leo XIV Akumbatiwa na Mtoto, Kielelezo cha Upendo wa Dhati
Na Sarah Pelaji, -Vatican.
Maandiko Matakatifu yanasema: “Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.” Mt 19:14 Katika mazingira ya heshima na utulivu katika Ukumbi wa Sala Ducale ndani ya Jumba la Kipapa la Vatican, tarehe 7 Juni iliyopita, tukio la kipekee na lenye mguso wa kiroho lilijitokeza wakati wa mkutano wa faragha kati ya Baba Mtakatifu Leo XIV na familia ya Giovanni Giordano, ambaye ni mshiriki wa huduma zaa kichungaji kwa Jeshi la Carabinieri katika Kambi ya “V.B. Salvo D’Acquisto” huko Tor di Quinto, Roma. Miongoni mwa waliohudhuria, alikuwapo pia mke wa Giordano pamoja na mtoto wao mvulana aliyeonekana mchangamfu, mwenye nguvu na asiyeweza kukaa kimya.
Wakati wa kusubiri kuingia kwa Papa Leo XIV, mtoto huyo alikuwa akizunguka ukumbini bila kuchoka, akicheza na kukimbia huku na kule kana kwamba yupo kwenye uwanja wa michezo. Hakutaka kujishughulisha na watu waliokuwapo wala kuacha kucheza kutokana na heshima ya mahali. Papa Leo XIV alipoingia ukumbini, huku watu wazima wakiwa wamesimama kimya, wakiwa na hisia za mshangao na heshima, yule mtoto alionesha tabia nyofu ya moyo wa mtoto ambaye bila kusita, alikimbilia kwa Baba Mtakatifu na kumkumbatia kwa upendo wa kweli, wa dhati, bila woga wala aibu. Papa Leo XIV, akiwa ameguswa na tendo hilo la upendo usio na masharti, alicheka kwa upole kisha akamkumbatia mvulana huyo, akionesha upendo na mapokezi ya kimoyo kwa tendo hilo la ajabu.
Ili Ilikuwa ni kumbatio la imani, la utu, la Mungu aliye hai kati ya waja wake. Tukio hili limeacha tafakari ya maneno ya Yesu: “Mtu asipofanywa kama mtoto mdogo, hatauingia Ufalme wa Mbinguni” (Rej. Mathayo 18:3). Katika tendo hili la kawaida lakini la kiroho kwa undani, tunakumbushwa kuwa mara nyingi ni wale walio na roho huru kama watoto ndio wanaoweza kuona ukweli, uzuri na upendo wa Mungu kwa macho ya imani yasio na mawaa. Ni kupitia matukio kama haya ambapo tunaweza kumsikia Mungu katika ujumbe wake wa upendo, ukaribu na pendo la Baba wa milele linalowakumbatia na kuwaambata wote bila ubaguzi.