Papa Leo XIV: Parokia Ziwe Ni Mahali pa Ujenzi wa Haki, Amani na Maridhiano
Na Sarah Pelaji, -Vatican
Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane wa XXIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani.” Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI), ametoa maoni yake kuhusu wito wa dharura uliotolewa na Papa Leo XIV kuhusu kujenga Parokia zinazosimikwa katika tunu ya amani. Katika mahojiano maalum na vyombo vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na baada ya kukutana na Balozi wa Urusi mjini Vatican, Kardinali Zuppi alieleza kwa kina umuhimu wa kuchukua hatua za kweli katika kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano, akisisitiza kwamba kila Parokia inapaswa kuwa nyumba ya amani. Kwa mujibu wa Kardinali Zuppi, ujumbe wa Papa Leo XIV unawakumbusha waamini, watu wenye mapenzi mema kuwa ujenzi wa amani si jambo la ziada ndani ya Kanisa bali ni wito wa dhati wa Kikristo wa kushughulikia mateso ya binadamu. Kardinali Zuppi amesema maneno hayo ya Papa Leo XIV aliyoyatoa tarehe 17 Juni 2025 alipokuwa akizungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia alitoa wito wa kuwa na mtazamo wa kichungaji unaozingatia uhalisia wa vita na vurugu vinavyoendelea sehemu mbalimbali za duniani. Papa Leone wa XIV, alipokuwa akizungumza juu ya amani, aliingia moja kwa moja katika mafundisho ya kijamii ya Kanisa. Wakati mwingine wapo wakosoaji wanaodai kuwa Kanisa badala ya kujihusisha na masuala ya uinjilishaji tu kwa kujikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili na kuzungumza juu ya Mungu hivyo kuona kwamba kushughulikia masuala ya kijamii kunapunguza imani ya kuitangaza na hatimaye kuishuhudia Injili.
“Ninapofikiria kuhusu jitihada za Mapapa, kuhusu Waraka wa Kitume wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” kuhusu suala la udugu na mazingira ambalo Papa Leo XIV amelisisitiza kwa nguvu, bado masuala haya huonekana kana kwamba ni ya hiari ambayo Kanisa linaweza kuyashughulikia au kuyaacha. Masuala hayo yote ni ya muhimu ili kuinjilisha katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu na kufanya jitihada za kuweka mizizi ya tunu msingi za kiinjili katika medani mbalimbali za maisha. Injili inaingia katika historia ya mwanadamu na haitoki humo. Kanisa linapaswa kufanya nini? Linapaswa kuzungumza kuhusu Kristo. Hilo ndilo alilofanya Papa Francisko ambaye hakuzungumza chochote isipokuwa Kristo Yesu. Alisema hivyo tangu mwanzo katika Waraka wake wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium.” “Evangelii gaudium” ambapo furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu na kwamba ni neno linalo maanisha “Kerigma” yaani kumtangaza Kristo Yesu. Na kuzungumza kuhusu Kristo maana yake ni kuingia katika historia, kwa sababu kuna uhusiano mkubwa kati ya uinjilishaji na kukuza utu, heshima na haki msingi za wa binadamu; kati ya meza ya Ekaristi na meza ya maskini, kati ya kuandaa meza ya Ekaristi na kuandaa meza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine. Muungano huu kati ya upendo na ukweli, kati ya uinjilishaji na ukuzaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo ambayo hayapaswa kukosekana kamwe. “Hatupaswi kuishia katika mijadala ya kitaaluma kuhusu amani. Hii ni hali ya huzuni inayoendeshwa na vita vingi mno na mantiki ya kijeshi inayodhani kuwa silaha ndio njia pekee ya kuleta amani. Ni upuuzi kufikiri kwamba mambo yatatengemaa bila kukabiliana na hali halisi,” alisema Kardinali Zuppi.
Alielezea hatua zinazopaswa kuchukuwa kwa sasa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuwa, hatua ya kwanza ni sala, na akazungumzia tukio la Pentekoste lililopendekezwa na CEI kama mwanzo wa mchakato wa sala za pamoja kwa ajili ya amani. Alisisitiza pia umuhimu wa mapokezi na mshikamano, akitoa mfano wa watoto wa Ukraine waliopokelewa kwa muda mjini Vatican, kwa usaidizi wa Padre Franco Fontana. “Kupokea watu waliokimbia vita kunaondoa chuki na kuleta mshikamano na haya ndiyo mambo ya msingi ya kuijenga jamii ya amani,” alisema. Alipoulizwa iwapo elimu ni njia kuu ya kuleta amani, Kardinali Zuppi alikubaliana na jambo hilo akisema kuwa elimu ndiyo msingi wa nyumba ya amani. Alielezea hatari ya kile alichokiita ‘elimu ya vita’ yaani malezi yanayojenga chuki, ubaguzi na vurugu, hasa kupitia mitandao ya kijamii. “Vita havianzii tu katika kushika na kubonyeza bastola bali huanzia mioyoni mwa watu katika mazingira yenye chuki na ujinga,” alisema Kardinali Zuppi. Alipongeza jitihada za parokia nyingi zinazoendesha shule za lugha na vituo vya baada ya shule ambavyo huwasaidia watoto wahamiaji na kuwaunganisha na jamii. Kardinali Zuppi alitupilia mbali dhana kwamba Kanisa linapozungumzia kuhusu amani au mazingira linatoka nje ya wito wake wa kiroho. Alisisitiza kuwa Mafundisho jamii ni sehemu muhimu sana ya uinjilishaji na kwamba tangazo la Kristo haliwezi kutenganishwa na kujali utu, heshima na haki msingi za binadamu. “Kuna muungano mkubwa kati ya uinjilishaji na ukuzaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu kati ya meza ya Ekaristi na meza ya masikini,” alisema. Kwa kuhitimisha mahojiamo haya maalum alieleza kuwa jitihada hizi haziwezi kuachwa kuwa jambo la hiari bali ni moyo wa imani ya Kikristo, ambapo upendo na ukweli vinatakiwa kwenda sambamba kama mapigo mawili ya moyo wa Kanisa.
Kwa Ufupi Papa Leo XIV anataka kila jumuiya ya Kikristo kuwa nyumba ya amani huku Kardinali Zuppi akisisitiza ujenzi wa amani ndani ya Kanisa kupitia sala, kupokea wahanga wa vita na kuwaonesha mshikamano pamoja na kutoa elimu yenye ujenzi wa amani. Amesisitiza uwepo wa Shule zakufundisha wahanga wa vita wakiwemo watoto lugha ya eneo mahalia ili waweze kujumuika na jamii, kuanzisha vituo vya kutoa malezi na huduma za kibinadamu baada ya shule huku akisisitiza kuwa Parokia zina nafasi kubwa katika kujenga jamii zenye amani. Katika mahojiano hayo, Kardinali Zuppi ametoa tafakari ya kina kuhusu wito wa Papa Leo XIV wa kuzifanya parokia kuwa nyumba za amani. Amesema kuwa, mwaliko huo umechukuliwa kama fursa ya kutafakari upya juu ya asili ya parokia, hatima yake, na haja ya mabadiliko yanayolenga kuimarisha mshikamano wa kijamii na kiroho. Inasisitizwa kuwa parokia hazipaswi kuwa tu vituo vya ibada, bali mahali pa ujenzi wa udugu wa kibinadamu wa kweli ambapo kila mtu anajisikia nyumbani, hasa katika dunia ya leo inayozidi kutawaliwa na: vita, upweke na migawanyiko. Pia kuna mwangaza kuhusu miezi miwili ya mwanzo ya upapa wa Papa Leo XIV, ikisisitiza jinsi alivyopokelewa kwa mshangao lakini pia kwa furaha na matumaini makubwa. Anaelezewa kuwa na mtazamo wa upole, uthabiti na hamu ya kuendeleza Kanisa linalosafiri. Uchaguzi wake unatajwa kama tukio lililoongozwa na Roho Mtakatifu, likiwa ni alama ya umoja wa Kanisa licha ya tofauti za lugha na mataifa. Katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, wito unatolewa wa kumuunga mkono Papa Leo XIV kwa sala, utii na ushirikiano wa kweli, ili kuishi vyema Jubilei hii ya matumaini ambacho ni kipindi cha kuimarisha: Umoja na ushirika wa ndani ya Kanisa na kati ya watu wote.