MAP

Papa leo XIV tarehe 2 Julai 2025 amekutana na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki. Papa leo XIV tarehe 2 Julai 2025 amekutana na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki.   (ANSA)

Mshikamano wa Imani na Mapendo wa Papa Leo XIV na Watu wa Mungu Ukraine

Katika hotuba yake, Papa Leo XIV aligusia changamoto wanazokumbana nazo waamini wa Ukraine, hasa katika kipindi hiki kigumu cha vita. “Katika muktadha wa kihistoria wa sasa, si rahisi kuzungumza juu ya tumaini, wala si rahisi kupata maneno ya faraja kwa familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao kutokana na vita hii isiyo na maana,” alisema kwa uchungu. Hata hivyo, alieleza kuguswa na ushuhuda mwingi wa imani na matumaini waliyonayo watu wa Ukraine.

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Baba Mtakatifu Leo XIV mnamo tarehe 2 Julai 2025 amekutana na kuzungumza n na viongozi na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki kutoka Ukraine, wanaokutanika mjini Vatican kwa ajili ya mkutano wao wa kichungaji ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha pia Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ambao unalenga kupyaisha tena tumaini la Taifa la Mungu, sehemu mbalimbali za dunia. Akizungumza na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo na Maaskofu waliokuwa wameshiriki mkutano huo, Papa Leo XIV   alieleza furaha yake ya kukutana nao baada ya kuwa amewasalimu mahujaji wa Kanisa hilo waliokuwa wamekusanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mnamo tarehe 18 Juni 2025.

Mshikamano wa Papa Leo XIV na Watu wa Mungu nchini Ukraine
Mshikamano wa Papa Leo XIV na Watu wa Mungu nchini Ukraine   (ANSA)

Katika hotuba yake, Papa Leo XIV aligusia changamoto kubwa wanazokumbana nazo waamini wa Ukraine, hasa katika kipindi hiki kigumu cha vita. “Katika muktadha wa kihistoria wa sasa, si rahisi kuzungumza juu ya tumaini, wala si rahisi kupata maneno ya faraja kwa familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao kutokana na vita hii isiyo na maana,” alisema kwa uchungu. Hata hivyo, alieleza kuguswa na ushuhuda mwingi wa imani na matumaini waliyonayo watu wa Ukraine, akisema kwamba, huo ni ushuhuda wa nguvu ya Mungu inayoendelea kudhihirika hata katikati ya uharibifu utokanao na vita. Alisema anafahamu kuwa Kanisa Katoliki la Kigiriki lina mzigo mkubwa, si tu katika kutoa huduma ya kiroho, bali pia ya kibinadamu kwa watu waliopondeka na kuvunjika mioyo; watu waliojeruhiwa kwa njia mbalimbali. “Niko karibu nanyi na kupitia kwenu niko karibu na waamini wote wa Kanisa la Ukraine. Tudumu katika imani moja na tumaini moja,” alesema.

Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine
Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine   (UGCC Department of Information)

Baba Mtakatifu Leo XIV alikumbusha kuwa muungano wa Kanisa ni fumbo kuu, unaojumuisha hata wale wote waliopoteza maisha yao kwa sababu ya vita, lakini sasa wako salama kwa kuwa wamepumzika kwa Mungu Baba Mwenyezi. Alitoa pole na sala kwa familia zote zilizoathirika na akasisitiza kwamba, Maombi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, yaendelee kuwa tegemeo la matumaini na njia ya kuelekea kwa Kristo Yesu ambaye ni amani ya ulimwengu. Akihitimisha hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuwashukuru Maaskofu na kuwabariki huku akikumbuka kwa furaha tukio la hivi karibuni ambapo waliimba sala ya “Baba Yetu” kwa lugha ya Kiukraine, na akawaalika waimbe tena sala hiyo kwa pamoja. Baada ya sala hiyo alitoa baraka zake za Kitume kwa wote waliokuwepo.

Papa Wajumbe wa Sinodi
02 Julai 2025, 16:29