Kardinali André Vingt-Trois Alikazia: Msalaba, Neno la Mungu, Sakramenti na Ushuhuda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali André Vingt-Trois, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Paris, nchini Ufaransa alifariki dunia Ijumaa tarehe 18 Julai 2025, akiwa na umri wa miaka 82, huko Jimbo kuu la Paris, alikozaliwa tarehe 7 Novemba 1942. Tarehe 28 Juni 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 25 Juni 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Paris na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 14 Oktoba 1988. Tarehe 21 Aprili 1999, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tours na tarehe 11 Februari 2005 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa na hivyo kumrithi Kardinali Jean-Marie Lustiger. Tarehe 24 Novemba 2007 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamsimika kuwa ni Kardinali. Kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa “The Bishops' Conference of France; Conférence des évêques de France, (CEF.)
Tarehe 7 Desemba 2017, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia utashi wake wa kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Tarehe 18 Julai 2025 akafariki dunia, tarehe 22 Julai kukafanyika mkesha na maombolezo na hatimaye mazishi yake kufanyika Jumatano tarehe 23 Julai 2025, kwenye Kanisa kuu la “Notre-Dame de Paris” kwa kuongozwa na Askofu mkuu Laurent Ulrich wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu Laurent Ulrich wa Jimbo kuu la Paris, amependa kuonesha uwepo na ukaribu wake kiroho na ushiriki wake katika sala na sadaka kutokana na msiba huu mzito na wa kuhuzunisha uliowagusa na kuwatikisa watu wa Mungu nchini Ufaransa, lakini zaidi Jimbo kuu la Paris.
Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wapendwa wa Marehemu bila kuwasahau wafanyakazi wa huduma ya afya wa “Marie-Thérèse House” ambao walimhudumia wakati wote alipokuwa anakabiliana na changamoto ya afya. Baba Mtakatifu Leo XIV amewatumia salam za rambirambi wakleri na waamini wote wa Jimbo kuu la Paris, alikohudumu kwa takaribani miaka kumi na miwili, akifundisha, akiongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Katika nyakati za mwisho wa uhai wake, akashiriki pia kuubeba Msalaba wa Kristo Yesu katika mwili wake. Baba Mtakatifu anamwombea, ili Kristo Mfufuka aweze sasa kumkaribisha katika makazi yake ya milele, ili hatimaye, aweze kumkirimia usingizi wa amani huku mwanga wa milele ukimwangazia. Anamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, aweze kumkirimia Mtumishi wake mwaminifu ahadi za maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Leo XIV amechukua fursa hii kuwafariji wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito.
Askofu mkuu Laurent Ulrich wa Jimbo kuu la Paris, katika mahubiri yake amesema: Masomo ya Ibada ya Misa takatifu wakati wa mazishi ni: Hosea 11; Zab 116; 1 Yoh 4:7-13; Yoh 3:1-21 yalichaguliwa zamani sana na Kardinali Vingt-Trois mwenyewe na ni sehemu ya wosia wake ambao katika maisha yake alikazia sana kuhusu: Fumbo la Msalaba, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na kuhakikisha kwamba, Injili inamwilishwa kila siku katika uhalisia wa maisha ya waamini, kama fursa ya kuwafanya watu wengine waweze kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Mambo makuu matatu yaani: Liturujia, Majadiliano kati ya Kanisa na Walimwengu pamoja na Injili ya upendo ni sehemu ya amana na urithi kutoka kwa Kardinali André Vingt-Trois, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Paris. Alipenda kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu aliokutana nao; huu ni upendo uliogusa maisha yake, kiasi cha kuamua kumfuasa Kristo katika maisha na wito wa Upadre. Alitambua na kuthamini uwepo hai wa Kristo katika maadhimisho ya Liturujia, ili kumtukuza Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.
Kardinali André Vingt-Trois, ni kiongozi aliyekuwa na fadhila ya unyenyekevu, aliyetaka kuona waamini wanamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; sanjari na utamadunisho, yaani kujikita kikamilifu katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. (Mdo. 17:23). Ni kiongozi aliyekazia zaidi malezi na majiundo makini ya majandokasisi, yaani Mapadre wa baadaye. Alipenda kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa dhati ndani ya Kanisa. Alisikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa kuwajengea watu 200 wasiokuwa na makazi. Kardinali André Vingt-Trois aliwahi kusema “Kifo ni kiini cha uzoefu wa kibinadamu, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu aliye teswa, kufa na kufufuka kwa wafu. Kaburi ni ishara kwamba, Mwenyezi Mungu anawafahamu na anataka warejee kwake, ili kuwa na umoja na ushirika na Mwenyezi Mungu.