MAP

Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki yamefunguliwa rasmi tarehe 28 Julai na yamehitimishwa Jumanne tarehe 29 Julai 2025, kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Tagle. Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki yamefunguliwa rasmi tarehe 28 Julai na yamehitimishwa Jumanne tarehe 29 Julai 2025, kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Tagle.  (@Vatican Media)

Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki: Wamisionari wa Matumaini

Hii ni changamoto kwa wamisionari kuendelea kupyaisha utume wa kutangaza Injili ya matumaini katika mitandao ya kijamii na katika ulimwengu wa kidijitali. Kuna haja ya kutafuta, kutangaza na kuishirikisha Injili ya amani na kwamba, pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia, wamisionari wajizatiti kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kutoka kwa Kristo Mfufuka na kuendelea kuwa ni mashuhuda wa sauti ya matumaini hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki yamefunguliwa rasmi tarehe 28 Julai na yamehitimishwa Jumanne tarehe 29 Julai 2025, kwa Ibada ya Misa Takatifu, Kumbukumbu ya Mtakatifu Martha, Maria na Lazaro, Marafiki wa Kristo Yesu na watakatifu, ambayo imeongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV akawapatia wosia wake wa Kitume. Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa kidijitali na Washawishi Wakatoliki inanogeshwa na kauli mbiu “Wamisionari wa matumaini, wakiwa wameshawishiwa na Kristo Yesu, wanatumwa kutangaza Injili ya Matumaini” kwa uaminifu na ubunifu mkubwa wakitambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mshawishi wao wa kwanza. Kristo Yesu, anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali Tagle akiongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili wamisionari
Kardinali Tagle akiongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili wamisionari   (@Vatican Media)

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, amesema, ushawishi ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya kila siku katika familia, ujenzi wa ujirani mwema, serikalini, shuleni na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu; ushawishi huu unafanyika katika mazingira na katika shughuli mbalimbali. Mwenyezi Mungu ndiye Mshawishi wa kwanza kwa sababu Mungu ni upendo. Watakatifu Martha, Maria na Lazaro walikuwa na ushawishi mkubwa kwa Kristo Yesu, kiasi cha Martha kuamua kuwa ni Mfuasi Mtume wa Kristo Yesu. Kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia, jumuiya, mifumo ya elimu, utawala bora na kazi yana athari kubwa kwa maisha ya watu. Kumbe, Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi wa Kikatoliki ni mwaliko kwa wahusika, kutoa ushawishi ili hatimaye, kuweza kupata matokeo chanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, wanapaswa kutambua kwamba, wao ni wamisionari.

Mashuhuda na wajenzi wa Injili ya amani na matumaini
Mashuhuda na wajenzi wa Injili ya amani na matumaini   (@Vatican Media)

Mwenyezi Mungu ndiye Mshawishi wa kwanza kwa sababu Mungu ni upendo na katika huruma na upendo wake wa daima akamtuma Mwanaye wa pekee, Neno aliyefanyika Mwili kwa yeye Bikira Maria kwa njia ya Roho Mtakatifu na kukaa kati ya waja wake. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, kiasi hata cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Wamisionari wa Kidigitali na Washawishi wa Kikatoliki, kusaidia kuhakikisha kwamba, huruma na upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu usaidie kuzuia sumu inayomwagika katika nyoyo za wat una jamii katika ujumla wake. Kristo Yesu alikuwa na ushawishi mkubwa sana kwa Martha, Maria na Lazaro, kiasi kwamba, wakawa ni marafiki wake wa ndani, Maria akakaa miguuni pa Kristo Yesu kumsikiliza Mwalimu wake, Martha, akachakarika katika huduma na Ufufuko wa Lazaro ni ishara ya utukufu wa Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Lazaro aliyekuwa amekufa kitambo, akasikia sauti ya Kristo Yesu, akafufuka kwa wafu: Rej. Yn 11:43.

Mwenyezi Mungu ndiye Mshawishi wa kwanza
Mwenyezi Mungu ndiye Mshawishi wa kwanza   (@Vatican Media)

Huu ni mwaliko kwa wamisionari hawa kuhakikisha kwamba, sauti zao zinawafikia hata wale waliolala makaburini, ili hata wao waweze kuonja upendo wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu yule ajaye Ulimwenguni. Rej. Yn 11:27. Watakatifu Martha, Maria na Lazaro ni mifano bora ya wamisionari washawishi, tayari kutangaza na kumshuhudia Kkristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu. Watambue kwamba, Kristo Yesu anawapenda na kwamba, Kristo Yesu aendelee kuwa ni mshawishi ili kweli haki, ukweli, upendo na amani ya Mwenyezi Mungu iweze kusambaa sehemu mbalimbali za dunia. Upendo wa Kristo Yesu uendelee kusambaa kati ya waja wake kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji. Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Misa takatifu, amewataka Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki, kuwa ni vyombo na wajumbe wa amani, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba, ameshinda dhambi na mauti; amewakirimia watu wa Mungu msamaha wa dhambi na maisha, huku akiwaonesha njia upendo. Hii ni changamoto kwa wamisionari hawa kuendelea kupyaisha dhamana na utume wao wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini katika mitandao ya kijamii na katika ulimwengu wa kidijitali. Kuna haja ya kutafuta, kutangaza na kuishirikisha Injili ya amani na kwamba, pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maisha ya mwanadamu, wamisionari wajizatiti kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kutoka kwa Kristo Mfufuka na kuendelea kuwa ni mashuhuda wa sauti ya matumaini hadi miisho ya dunia. Rej. Mdo 1: 3-8.

Familia ya Martha, Maria na Lazaro: Ilikuwa nai Ushawishi mkubwa kwa Yesu
Familia ya Martha, Maria na Lazaro: Ilikuwa nai Ushawishi mkubwa kwa Yesu   (@Vatican Media)

Haya ni matumaini yanayopaswa kutia nanga nyoyoni mwa watu, lakini zaidi wale wanaoteseka, ili kujenga utamaduni mpya unaosimikwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini ukiwa unabaki umesimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yana ushawishi mkubwa katika maisha ya watu, kiasi cha kuathiri mahusiano kati ya watu wenyewe, Mwenyezi Mungu na jirani zao, kiasi hata cha kuathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki wanayo dhamana na wajibu ya kujenga mtandao wa utu wa binadamu na Kikristo na kwamba, huu ndio uzuri wa mtandao huu. Katika mabadiliko makubwa, Mama Kanisa ataendelea kuwaangazia wanadamu, kwa mwanga wa matumaini ya Kristo Yesu, ili waweze kuwa na mang’amuzi bora, kwa kuchagua kile kilicho chema, ili kuleta mabadiliko kwa kutakaswa. Katika ulimwengu wa maendeleo makubwa ya matumizi ya teknolojia ya akili unde, hii ni changamoto inayopaswa kupokelewa kwa mikono miwili, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujenga uzoefu na utamaduni wa kusikiliza na kuzungumza; kuelewa na kueleweka. Kumbe, kuna haja ya kuunda lugha itakatotangaza na kushuhudia Upendo wa Mungu; kwa kushikamana na wale wote wanaoteseka; ili kuganga na kuponya madonda yao; kwa wale walioteleza na kuanguka, waweze kusimama tena; kwa kuishi katika uhalisia wao na kuendelea kutambua kwamba, wao ni watu wa kwanza wanaohitaji Injili.

Changamoto ya matumizi ya teknolojia ya akili unde
Changamoto ya matumizi ya teknolojia ya akili unde   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki, kwenda kutengeneza nyavu, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu. Rej. Mt 4:21-22. Leo hii wanaitwa na kutumwa kutengeneza mitandao ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; mitandao ya upendo, umoja na ushirikiano; kama sehemu ya ujenzi wa urafiki wa kijamii, ili kujenga, kuganga na kuponya kile kilichokuwa kimeharibika, ili hatimaye, kuambata upendo unaotoa nafasi kwa jirani, kuliko kujitafuta mwenyewe; upendo unaotoa sauti kwa wale wasiokuwa na sauti. Hii ni mitandao inayookoa na inayowawezesha watu kuona uzuri kwa kuangaliana machoni. Hii ni mitandao ya ukweli yaani mitandao ya Mungu. Wamisionari na Washawishi hawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa umoja na ushirika, tayari kuvunjilia mbali: ubinafsi na uchoyo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuvunjilia mbali mantiki ya habari za kughushi “fake news” kwa kujikita katika uzuri, mwanga na kweli za Kiinjili. Baba Mtakatifu Leo XIV kabla ya kuwapatia baraka zake za kitume, amewashukuru kwa ushuhuda wao ambao umesaidia kujenga maisha mapya; kwa ndoto walizo nazo, kwa upendo wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa msaada na mshikamano na maskini na watu wanaoteseka na kwa safari yao katika barabara za ulimwengu wa kidijitali.

Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali
29 Julai 2025, 14:15