Jubilei ya Miaka 75 ya Parokia ya B. Maria wa Fatima, Mpwapwa, Jimbo kuu Dodoma
Na Ndahani Lugunya, Mpwapwa, Dodoma, Tanzania.
Parokia ni kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya: kitamaduni, kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya upendo na huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia katika maisha na utume wa Kanisa.”
Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kujisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa upendo na huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake. Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa kimisionari na kisinodi.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo zaidi. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Parokia ya Bikira Maria wa Fatima- Mpwapwa, Jimbo kuu Katoliki la Dodoma, kuadhimisha Jubilei ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake na Shirika la Mapadre wa Mateso “Congregatio Passionis Iesu Christi, kifupi: C.P.) “Passionisti” watu wa Mungu wanaliangalia tukio hili kwa imani na matumaini zaidi na hasa katika Kipindi hiki cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 ya Ukristo yalizinduliwa tarehe 31 Mei 2024 na kilele chake kuadhimishwa hivi karibuni, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo kuu la Dodoma. Katika Ibada hiyo, vijana 104 waliimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara.
Parokia imeendelea kuimarisha Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristoambazo kimsingi ni Kanisa dogo mahalia la familia zinazopakana na ambalo kazi yake hasa ni kusali pamoja, kusikiliza na kutafakari kwa pamoja Neno la Mungu, kwa kulimwilisha na kulieneza. Wanajumuiya wanahamasishana kuishi maisha adili ya Kikristo na hivyo kuwa mashuhuda wa imani yao. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo msingi wake ni Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ambavyo huwaimarisha katika imani, upendo na matumaini katika umoja (Koinonia - Umoja), wakimshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na ambaye alifufuka na kumtangaza kama Mwenyezi Mungu na Mwokozi ndiyo imani ya Kanisa (Kerygma - Imani); na hatimaye, ni kuonesha imani hiyo kwa huduma wanayotoa miongoni mwao wenyewe na kwa maskini (Diakonia – Utumishi.) Tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Parokia ya Bikira Maria wa Fatima- Mpwapwa, Jimbo kuu Katoliki la Dodoma, kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka, changamoto anasema Askofu msaidizi Kibozi ni kwa wana Kanisa kuyaendeleza mema na mazuri yote waliyojichotea katika kipindi cha mwaka mzima.Waamini waendelee kushikamana katika imani, matumaini na mapendo; waendelee kujikita katika maisha ya Sala, Sakramenti za Kanisa pamoja na Matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji, lengo anasema, Askofu msaidizi Kibozi ni kuacha alama ya kudumu na kwamba, maadhimisho haya yaendelee kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Waamini wajibidiishe kumpenda Mungu aliyewaumba pasipo mastahili yao. Kwa upande wake Padre Kizito Mchana, amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu Parokia ya Bikira Maria wa Fatima- Mpwapwa inayoundwa na Vigango 16 na Jumuiya Ndogo ndogo 101. Kunako mwaka 1954 Shirika la Mapadre wa Mateso wakaikabidhi Parokia hii kwa Mapadre Wazalendo, yaani Mapadre wa Jimbo ambao walikuwa ni Padre Peter Lubuva na Padre Fausto na ilipowadia tarehe 8 Desemba 1963 wakaikabidhi Parokia hii kwa Shirika la Ndugu Wafranciskani Wakapuchini, Tanzania hadi mwaka 1982 na hatimaye, Parokia ikarejeshwa tena mikononi mwa Mapadre wazalendo.