Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Jimbo Kuu Chicago:Upendo wa Mungu unaweza kuponya
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV akianza ujumbe usiku wa tarehe 14 Juni 2025 kwa washiriki wa hafla ya kuadhimisha kuchaguliwa kwake aliwasalimia na kuonesha furaha yake wote mliokusanyika Uwanja wa White Sox kwa sherehe hiyo kuu kama jumuiya ya imani katika Jimbo kuu la Chicago. "Salamu za pekee kwa Kardinali Cupich, kwa Maaskofu wasaidizi, marafiki zangu wote ambao wamekusanyika leo kwenye Maadhimisho ya Utatu Mtakatifu. Na ninaanza hapa kwa sababu Utatu ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwetu. Mungu: Baba, Mwana, na Roho. Watu watatu katika Mungu mmoja wanaoishi pamoja katika kina cha upendo, katika jumuiya, wakishiriki ushirika huo nasi sote.” Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kuwa kwa hiyo, wakikusanyika hapo kwa ajili ya adhimisho hilo kuu, alipenda kutoa shukrani zake na wakati huohuo kuwatia moyo kuendelea kujenga jumuiya, urafiki, kama kaka na dada katika maisha yao ya kila siku, katika familia zao, katika parokia zao katika Jimbo kuu, na duniani kote. Papa alipenda kutuma salamu maalum kwa vijana wote - kwenu mliokusanyika hapa leo na kwa wale ambao labda wanatazama salamu hii kwa njia za kiteknolojia, kwenye mtandao. Mnapokuwa pamoja, unaweza kupata uzoefu - hasa baada ya kuishi wakati wa janga - nyakati za kutengwa, shida kubwa, wakati mwingine hata shida katika familia zenu au katika ulimwengu wetu wa sasa.”
Wakati mwingine inaweza kuwa hali ya maisha yenu haijakupa nafasi ya kuishi imani yenu kuishi kama washiriki wa jumuiya ya imani, na ningependa kuchukua nafasi hii kuwaalika kila mmoja wenu kutazama ndani ya moyo wake, kutambua kwamba Mungu yuko na kwamba, labda kwa njia nyingi tofauti, Mungu anakutafuta, anakuita, anakualika kumjua Mwana wake Yesu Kristo, kupitia Maandiko, labda kupitia kwa rafiki, babu au bibi ambaye angeweza ...ambaye anaweza kuwa mtu wa imani. Kugundua jinsi ilivyo muhimu kwa kila mmoja wetu kutilia maanani uwepo wa Mungu ndani ya moyo wetu, kwenye ile shauku ya upendo maishani mwetu , kutafuta kikweli, na kutafuta njia ambazo tunaweza kufanya jambo fulani na maisha yetu kuwatumikia wengine. Na katika huduma hiyo kwa wengine tunaweza kugundua kwamba, kwa kuungana katika urafiki, kwa kujenga jumuiya, sisi pia tunaweza kupata maana halisi ya maisha yetu. Nyakati za wasiwasi, za upweke….
Baba Mtakatifu Leo XIV kadhalika alisisitiza kuwa: “Watu wengi wanaoteseka kutokana na uzoefu mbalimbali wa huzuni wanaweza kugundua kwamba upendo wa Mungu kweli unaweza kuponya, kwamba huleta tumaini na kwamba kiukweli, kwa kukutana kama marafiki, kama kaka na dada, katika jumuiya, katika parokia, katika uzoefu wa maisha tulioishi pamoja kwa imani, tunaweza kugundua kwamba neema ya Bwana, upendo wa Mungu, unaweza kweli kutuponya, inaweza kutupa nguvu zote tunazohitaji katika maisha ambayo tunaweza kuwa na tumaini. Kushiriki ujumbe huu wa matumaini sisi kwa sisi - kukuza ufahamu, kutumikia, kutafuta njia za kufanya ulimwengu wetu kuwa mahali pazuri, hutupati maisha halisi sisi sote na ni ishara ya matumaini kwa ulimwengu mzima.
Kwa vijana waliokusanyika hapa, ninataka kusema tena kwamba ninyi ni ahadi ya matumaini kwa wengi wetu. Ulimwengu unawatazama mnapotazama pande zote na kusema: tunawahitaji, tunataka muwe pamoja nasi kushiriki nasu utume huu - kama Kanisa na katika jamii - wa kutangaza ujumbe wa matumaini ya kweli na kukuza amani, kukuza maelewano kati ya watu wote. Ni lazima tuangalie zaidi ya zetu - ikiwa tunaweza kuziita hivyo - njia za ubinafsi. Ni lazima tutafute njia za kuunganisha na kuendeleza ujumbe wa tumaini. Mtakatifu Agostino anatuambia kwamba ikiwa tunataka ulimwengu kuwa mahali bora zaidi, lazima tuanze na sisi wenyewe, lazima tuanze na maisha yetu, kwa mioyo yetu (taz. Mahubiri 311; Maoni juu ya Injili ya Mtakatifu Yohana, Homilia 77). Na hivyo basi, kwa maana hiyo, mnapokusanyika kama jumuiya ya imani, mnaposherehekea Jimbo kuu la Chicago, mnapotoa uzoefu wenu wa furaha na matumaini, mnaweza kuelewa, mnaweza kugundua kwamba ninyi pia ni vinara wa matumaini. Nuru hiyo, ambayo labda kwenye upeo wa macho si rahisi kuona; na bado, tunapokua katika umoja wetu, tunapokusanyika katika ushirika, tunagundua kwamba nuru hiyo inazidi kung'aa zaidi. Nuru hiyo ambayo, kiukweli, ni imani yetu katika Yesu Kristo.
Na tunaweza kuwa ujumbe huo wa tumaini, ili kuendeleza amani na umoja ulimwenguni pote. Sote tunaishi na maswali mengi mioyoni mwetu. Mtakatifu Agostino anazungumza mara nyingi juu ya moyo wetu "usio na utulivu" na kusema: "moyo wetu hautulii mpaka utulie ndani yako, Bwana" (Ukiri 1,1,1). Kutotulia huku sio jambo baya, na tunapaswa kutafuta njia za kuzima moto, kuondoa au hata kujitia ganzi kwa mivutano tunayohisi, shida tunazopata. Badala yake, tunapaswa kuwasiliana na mioyo yetu na kutambua kwamba Mungu anaweza kufanya kazi katika maisha yetu, kupitia maisha yetu na, kupitia sisi, kuwafikia watu wengine. Papa Leo alipenda kuhitimisha ujumbe huo mfupi kwa wote akitoa mwaliko wa kuwa kweli nuru ya matumaini. “Tumaini halikatishi tamaa,” Mtakatifu Paulo anatuambia katika barua yake kwa Warumi (5:5). Ninapowaona kila mmoja wenu, ninapoona jinsi watu wanavyokusanyika kusherehekea imani yao, ninatambua jinsi tumaini liko duniani. Katika Mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, Kristo, ambaye ni tumaini letu, kwa hakika anatuita sote kukusanyika pamoja, ili tuweze kuwa kielelezo hai cha kweli: mwanga wa matumaini katika ulimwengu wa leo.
Kwa hiyo Papa Leo XIV aliwaalika wote kutafuta muda, kufungua mioyo yao kwa Mungu, kwa upendo wa Mungu, kwa amani hiyo ambayo Bwana pekee anaweza kutupatia. Ili kuhisi jinsi upendo wa Mungu ulivyo wa maana sana, jinsi ulivyo na nguvu, katika maisha yetu. Na kutambua kwamba, ingawa hatufanyi lolote ili kustahili upendo wa Mungu, Mungu, kwa ukarimu wake, anaendelea kumimina upendo wake juu yetu. Na anapotupa upendo wake, anatuomba tu tuwe wakarimu na tuwagawie wengine yale ambayo ametupatia. “Mbarikiwe sana mnapokusanyika kwa ajili ya sherehe hii. Upendo na amani ya Bwana iwashukie kila mmoja wenu, juu ya familia zenu, na Mungu awabariki ninyi nyote, ili daima muwe vinara wa matumaini, ishara ya matumaini na amani katika dunia nzima. Na baraka ya Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, iwashukie na kukaa nanyi milele. Amina.”