Papa Leo XIV:Mwenyeheri Hossu alijua kuwa milango ya uovu haitaishinda kazi ya Mungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, kwa Kiingereza, katika fursa ya kumbukumbu ya Kardinali Iuliu Hossu wa Romania (1885-1970), ambaye kama Askofu wa Kigiriki-Katoliki wa Cluj-Gherla, kati ya 1940 na 1944, alijitolea kwa ujasiri na kuchangia kuokoa maelfu ya Wayahudi kutoka kaskazini mwa Transylvania dhidi ya kifo. Baba Mtakatifu mbele ya waliokuwapo, Jumatatu jioni tarehe 2 Juni 2025 alianza kusema: “Tunakutana leo katika Kanisa la Sistine katika Mwaka wa Jubilei ya Matumaini, ili kukumbuka Mtume wa Matumaini: Mwenyeheri Iuliu Hossu, Askofu wa Kanisa Katoliki la Ugiriki Cluj-Gherla na shahidi kwa ajili ya imani wakati wa mateso ya Kikomunisti nchini Romania. Leo, kwa namna fulani, amengia katika Kikanisa hili, akiwa aliundwa kuwa Kardinali mikononi mwa Mtakatifu Paulo VI, tarehe 28 Aprili 1969, akiwa amefungwa kwa uaminifu wake kwa Kanisa la Roma.”
Kumuenzi Kardinali Hossu: kujitolea kwa ujasiri
Baba Mtakatifu Leo kwa njia hiyo alitoa salamu kwa furaha kwa wote waliohudhuria: wawakilishi wa Kanisa la Kigiriki-Katoliki nchini Romania, Mamlaka za kiraia na hasa, Mheshimiwa Silviu Vexler, Rais wa Shirikisho la Jumuiya za Kiyahudi nchini Romania. Papa Leo XIV alisema kuwa: “Tunasherehekea mwaka maalum wa kumuenzi Kardinali Iuliu Hossu, ishara ya udugu unaovuka mipaka yote ya kikabila na kidini. Mchakato wa kumpa jina la "Wenye Haki Kati ya Mataifa," ulianza mnamo 2022, ambao ulichochewa na kujitolea kwake kwa ujasiri kuunga mkono na kuokoa Wayahudi wa Kaskazini mwa Transylvania wakati, kati ya 1940 na 1944, Wanazi walikuwa wakitekeleza mpango wao mbaya wa kuwapeleka kwenye kambi za maangamizi. Akiwa katika hatari kubwa kwake mwenyewe na kwa Kanisa Katoliki la Ugiriki, Mwenyeheri Hossu alichukua shughuli nyingi kwa niaba ya Wayahudi zilizolenga kuzuia kufukuzwa kwao.”
Papa Leo XIV akiendelea kumbuka, alisema: “Katika majira ya kuchipua ya 1944, matayarisho yalipokuwa yakifanywa huko Cluj-Napoca (huko Kolozsvár ya Hungaria) na miji mingine katika Transylvania, ili kuanzisha ghetto kwa ajili ya Wayahudi, alihamasisha mapadre wa Kigiriki-Katholiki na waamini kupitia barua ya kichungaji iliyochapishwa tarehe 2 Aprili 1944.” Pia tunafahamu hili kupitia ushuhuda wa Moshe Carmilly-Weinberger, Mkuu wa zamani wa jumuiya ya Wayahudi ya Cluj-Napoca. Katika barua hiyo, alizindua wito mahiri na wa kina wa kibinadamu. “Ombi letu,” aliandika, “limeelekezwa kwenu nyote, ndugu waheshimiwa na watoto wapendwa, kuwasaidia Wayahudi si kwa mawazo yenu tu, bali pia kwa sadaka yenu, mkijua kwamba hakuna tendo jema zaidi linalopaswa kufanywa leo hii kuliko kutoa msaada wa Kikristo na Waromania, uliozaliwa na upendo wa kibinadamu wenye bidii. Wasiwasi wetu wa kwanza katika wakati huu lazima uwe kazi hii ya unafuu.” Kulingana na ushuhuda wa kibinafsi wa Mkuu wa zamani wa Kiyahudi, Kardinali Hossu alisaidia kuokoa maisha ya maelfu ya Wayahudi kaskazini mwa Transylvania kati ya 1940 na 1944.
Kanisa liko karibu na mateso ya watu
Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kuwa “Tumaini lililooneshwa na Mchungaji huyu mkuu lilikuwa la mtu wa imani, ambaye anajua kwamba milango ya uovu haitaishinda kazi ya Mungu. Maisha yake yalikuwa shuhuda wa imani iliyoishi kwa ukamilifu, katika sala na kujitolea kwa wengine. Mtu wa mazungumzo na nabii wa matumaini, alitangazwa kuwa mwenyeheri na Papa Francisko tarehe 2 Juni 2019 huko Blaj.” Papa Leo XIV akikumbuka tukio hilo alisisitiza kuwa “Katika mahubiri ya tukio hilo, Papa alinukuu maneno ya Kardinali ambayo yalifupisha maisha yake yote kuwa: “Mungu ametupeleka katika giza hili la mateso ili kutoa msamaha na kuombea wongofu wa wote.” Kwa kuongezea alisema “Maneno haya yanajumuisha roho ya wafia imani: imani isiyotikisika kwa Mungu, isiyo na chuki na iliyoambatana na roho ya huruma inayogeuza mateso kuwa upendo kwa mtesaji wa mtu. Hata sasa, maneno hayo yanasalia kuwa mwaliko wa kinabii wa kushinda chuki kupitia msamaha na kuishi imani ya mtu kwa heshima na ujasiri. Kanisa liko karibu na mateso ya watu wa Kiyahudi, ambayo yalifikia kilele cha maafa ya Kimbari. Linajua vizuri maana ya uchungu, kutengwa, na mateso. Kwa sababu hiyo, lihisi kujitolea, kama suala la dhamiri, kujenga jamii inayozingatia heshima ya hadhi ya mwanadamu.”
Maadhimisho ya miaka 60 ya Nostra Aetate yanakaribia
Papa Leo XIV aidha alisema kuwa “Ujumbe wa Kardinali Hossu unabaki kuwa wakati muafaka. Yale aliyowafanyia Wayahudi wa Romania, na juhudi zake za kumlinda jirani yake licha ya hatari na hatari zote, leo hii yanamfanya awe kielelezo cha uhuru, ujasiri na ukarimu, hata akajitolea kuwa mhanga mkuu. Ndiyo maana kauli mbiu yake ya “Imani Yetu ni Maisha Yetu,” inapaswa kuwa kauli mbiu ya kila mmoja wetu. Ni matumaini yangu ya maombi kwamba mfano wake, ambao ulitarajia fundisho lililotolewa baadaye katika Hati ya Nostra Aetate ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican - maadhimisho ya miaka sitini ambayo yanakaribia - pamoja na urafiki wao, itatumika kama mwanga kwa ulimwengu wa leo.” Papa Leo XIV kwa kuhitimisha alisema “ wacha tesema ‘hapana’ kwa unyanyasaji wa aina zote, na hata zaidi wakati unafanywa dhidi ya wale ambao hawana ulinzi na hatari, kama watoto na familia. Mungu awabariki kila mmoja wenu na wapendwa wenu!”