Papa Leo XIV Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Nguzo za Kanisa na Mashuhuda wa Damu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Dominika tarehe 29 Juni 2025 inajikita katika mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha yaliyosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili kwani hawa walikuwa ni wachamungu! Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kuhusu Mtume Petro na Paulo, nguzo za Kanisa, amekazia kuhusu mambo makuu mawili: Umoja na ushirika wa Kanisa pamoja na ushuhuda wa maisha ya imani yaliyopelekea hata Mitume hawa wawili kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtume Petro alifungwa gerezani na hatimaye akahukumiwa kifo; kwa upande wake, Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema, wakati wa kufariki kwake umefika. Amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza na imani ameilinda. Mitume wote wawili walisadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili.
Umoja wa imani anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, umefikiwa baada ya safari ndefu ya kila mmoja wao kadiri ya maisha na utume wake. Wakaunganishwa katika udugu wa kibinadamu, ulioondoa tofauti zao. Mtakatifu Petro alikuwa ni mvuvi wa Galilaya wakati Paulo Mtume, alikuwa ni mwanazuoni na msomi mahiri. Mtume Petro akaacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu. Lakini Paulo Mtume, alilidhulumu Kanisa la Kristo, lakini baada ya kukutana na Kristo Mfufuka akaongoka na kuwa ni shuhuda na mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Mitume wote wawili, wakati mwingine walitofautiana kama binadamu, lakini tofauti zao msingi zikapata suluhu ya kudumu katika Mtaguso wa Kwanza wa Yerusalemu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujikita kutafuta: amani, utulivu na maridhiano, kila mtu akiheshimu uhuru wa ndugu yake na hatimaye Mitume wakawa wamoja katika maisha na utume wao: “Concordia apostolorum” kielelezo makini cha umoja wa shughuli za kitume katika Roho Mtakatifu; Na Mama Kanisa anawaadhimisha wote wawili siku moja, ingawa kila mmoja alifariki kwa wakati wake, lakini wakiwa ni wamoja katika roho.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Roho Mtakatifu anawezesha umoja na ushirika wa Kanisa, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Mitume wanajitahidi kuhakikisha wanadumisha umoja katika tofauti zao; ili kukuza umoja na ushirika wa watu wa Mungu. Huu ni ushirika kati ya Baba Mtakatifu, Askofu, Mapadre, Watawa na Waamini walei. Umoja na ushirika huu, viliwezeshe Kanisa kujikita katika: Sera na mikakati ya shughli za kichungaji; majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, Mama Kanisa anapenda kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii na walimwengu. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanatumia vyema fursa ya umoja na tofauti zao msingi kuwa ni mahabara ya: Umoja na ushirika; Udugu wa kibinadamu na Upatanisho, ili kila mwamini ndani ya Kanisa, katika historia yake, ajifunze kutembea pamoja na jirani zake. Watakatifu Petro na Paulo, Mitume wanawahamasisha watu wa Mungu kutangaza na kushuhudia maisha ya imani yao, ili kuondokana na ibada na mazoea; yanayoshindwa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Mitume hawa wawili wanawachangamotisha waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kuzingatia umuhimu wa kufanya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya, kwa kuanzia na maswali yanayobubujika kutoka kwa waamini mintarafu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kiini cha Injili kimefumbatwa katika kumtambua, kumkiri, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Kiri hii ya imani ilisaidia kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kati ya Kristo Yesu na wafuasi wake. Kristo Yesu awe ni chemchemi ya matumaini, mahusiano na mafungamano kati ya waja wake, tayari kumtangaza na kumshuhudia miongoni mwa watu wa Mataifa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka waamini kuendelea kujikita katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa, ili daima kuwawezesha waamini kuweza kuwa na njia mpya za kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa linaitwa na kutumwa kuwa ni alama ya umoja na ushirika; chemchemi ya imani hai; Jumuiya ya waamini wanaotangaza na kushuhudia furaha na faraja ya Injili mintarafu hali mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwatakia kheri na baraka, Maaskofu wakuu wapya 54 waliovikwa Pallio Takatifu, waendelee kuwa ni chanzo cha umoja, ushirika na imani ya Kanisa wanayopaswa kuiboresha katika maisha na utume wao kwenye Makanisa mahalia. Ametambua uwepo na ushiriki wa ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, pamoja naWajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraine. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, kwa kuwataka waamini ambao wamejengwa na kuimarishwa na watakatifu hawa, basi wajitahidi kutembea wakiwa wameshikamana katika imani, umoja na ushirika, wawaombe, ili kuwaombea neema na baraka kwa Mji wa Roma na Kanisa zima katika ujumla wake. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ni Siku maalum ambayo imetengwa na Mama Kanisa ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia utekelezaji wa Injili ya huduma ya upendo, huruma na ukarimu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mchango huu unalenga kufanikisha jitihada za huruma ya Mungu ambazo kimsingi zinafumbatwa katika Sakramenti za Kanisa na kumwilishwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa watu wanaosiginwa, utu, heshima na haki zao msingi kutokana na umaskini, ujinga na maradhi; kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa watu wanaokumbwa na majanga pamoja maafa mbalimbali kwa sasa. Mchango huu unamwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa mabegani na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki wanapokuwa katika majimbo yao pamoja na Mapatriaki. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, katika Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; daima wakikumbuka kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya masitahili na mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kondoo wa Kristo. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu wapya wamekuwa wakivishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Lakini, Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 29 Juni 2025 amerejea tena katika Mapokeo ya Mama Kanisa ya kuwavisha Pallio Takatifu Maaskofu wakuu na Mapatriaki 54 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kutoka Barani Afrika, kuna Maaskofu wakuu Saba nao ni: Kardinali Stephen Brislin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Johannesburg, Afrika ya Kusini; Askofu mkuu Robert Cisse wa Jimbo kuu la Bamako, Mali; Askofu mkuu Jacques Assanvo Ahiwa wa Jimbo kuu la Bovakè, Pwani ya Pembe; Askofu mkuu Birfuorè Dabirè wa Jimbo kuu la Bobo-Dioulasso, Burkina Faso; Askofu mkuu Andrè Gueye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal; Askofu mkuu Armand Konè wa Jimbo kuu la Korhogo, Pwani ya Pembe na hatimaye ni Askofu mkuu Jean Jacques Koffi Oi Koffi wa Jimbo kuu la Gagnoa, Pwani ya Pembe. Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, ulioshiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Dominika tarehe 29 Juni 2025 umeongozwa na Askofu mkuu Emanuel Hana Shaleta “Challita” (aliyezaliwa Novemba 11, 1956) wa Kanisa Katoliki la Wakaldayo.