MAP

Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kwa Mwaka 2025 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Usiadhibu” Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kwa Mwaka 2025 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Usiadhibu”   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV:Siku ya Kupambana na Biashara Na Mtumizi Haramu ya Dawa za Kulevya 2025

Papa Leo XIV katika hotuba yake kwa washiriki wa Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani amekazia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru na kwamba, watu wanashinda ubaya kwa kuungana; waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, uraibu wa michezo ya kamari na upatu, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ni dira ya watu kukutana, ili kujenga na kudumisha uhuru, haki, amani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, “United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC” inasema, lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani, sanjari na biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake. Ni wazi kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga linaloiathiri jamii kwa ujumla. Dawa haramu zinazosambaa sokoni huchochea matatizo ya afya na usalama, na kuhatarisha maisha ya watu binafsi na wale wanaowazunguka. Hii ndiyo sababu ni muhimu kuendelea kuongeza ufahamu, kuzuia matumizi haramu ya dawa za kulevya, na kutoa nyenzo kusaidia wale wanaoathirika. Katika siku hii ya uhamasishaji, ni muhimu kukumbuka kuwa mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya sio lazima yawe ya kuadhibu tu, bali pia yaambatane na hatua za kuelimisha na za kuzuia. Uelimishaji ni nyenzo muhimu katika mapambano haya, kwani kupitia elimu, wananchi wanaweza kupata uelewa wa kutosha unaowasaidia kuepuka kujiingiza katika matumizi au biashara ya dawa hizo. Mbali na kutoa maarifa, kampeni hii ilenge pia kuwajengea watu uzalendo: Utu na maadili mema, ili wawe sehemu ya jamii inayokataa vitendo vya rushwa na matumizi ya dawa ya kulevya kwa dhati. Elimu sahihi huzaa jamii yenye maamuzi bora, inayojali afya, usalama na mustakabali wa taifa. Uwekezaji katika kuzuia ndio ufunguo wa kulinda jamii na kuhakikisha mustakabali mzuri wa kizazi kijacho.

Tarehe 26 Juni, Siku ya ya Kupambana na Biashara na matumizi haramu ya dawa
Tarehe 26 Juni, Siku ya ya Kupambana na Biashara na matumizi haramu ya dawa   (@Vatican Media)

Jumuiya ya Kimataifa inakumbushwa kwamba, kinga ni bora zaidi kuliko tiba, na kwamba kila hatua ya mtu binafsi inazingatiwa katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kupambana na biashara hii ambayo ina madhara makubwa katika afya, utawala bora, ulinzi na usalama wa raia na mali zao! Ikumbukwe kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kwa Mwaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu: “Usiadhibu” inayohamasisha ulimwengu mzima kuwa na sera za dawa zinazozingatia afya, haki msingi za binadamu na maendeleo endelevu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa washiriki wa Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani amekazia kuhusu: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru wa kweli na kwamba, watu wanashinda ubaya kwa kuungana; waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, uraibu wa michezo ya kamari na upatu, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ni dira ya watu kukutana, ili kujenga na kudumisha uhuru, haki, amani na matumaini.

Familia zina wajibu wa kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Familia zina wajibu wa kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: Matumaini na amani ni sawa na chanda na pete, mambo msingi ambayo Kristo Yesu aliwakirimia wanafunzi wake waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, changamoto kwa waamini kusimama kidete kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kushuhudia uhuru kamili ambao kimsingi ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli. Watu wanashinda ubaya kwa kuungana pamoja; kama ilivyo pia ukosefu wa haki msingi za binadamu ni mapambano ya wote, yanayowataka watu kuthaminiana na kuheshimiana. Serikali mbalimbali zimewekeza sana katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa kisingizio cha usalama wa Taifa, lakini walengwa wa vita hii ni watu maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na matokeo yake ni watu kukata tamaa ya maisha. Kanisa linajitambua kuwa ni Mama wa wote na kwa sababu hii, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alizisihi nchi zote kuwa na uwazi wa ukarimu ambao badala ya kuogopa kupoteza hadhi ya asili ya mahali, wataweza kuunda namna mpya za usanisi wa kitamaduni. Jinsi ilivyo mizuri ile miji inayoshinda hali ya kutoamiana inayofadhaisha, ikawakubali wale walio tofauti na kuifanya tofauti ukubaliano huu kuwa kipengele kipya cha maendeleo. Jinsi inavyovutia ile miji ambayo, hata katika usanifu wa majengo yake, imejaa nafasi zinazounganisha, zinazohusisha na kupendelea kuwatambua watu wengine. Rej. Evangelii gaudium, 210.

Waatyhirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana
Waatyhirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 yanajikita katika utamaduni wa watu kukutana kama njia ya usalama, kurejesha na kugawanya tena mali iliyokusanywa pasi na haki, kama njia ya upatanisho wa kibinafsi na wa kiraia: "Duniani kama huko mbinguni": mji wa Mungu unatukabidhi kutoa unabii katika mji wa wanadamu. Na hii - tunajua - inaweza pia kusababisha kifo cha ushuhuda leo hii. Mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya, kujitolea kielimu miongoni mwa maskini, utetezi wa jumuiya za kiasili na wahamiaji, uaminifu kwa mafundisho ya kijamii ya Kanisa katika sehemu nyingi huchukuliwa kuwa ni sehemu ya upotoshaji. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia vijana kwamba, wao si watazamaji bali ni wahusika wakuu kwani Mwenyezi Mungu hufanya mambo makuu pamoja na wale anaowakomboa kutoka kwenye maovu. Zaburi nyingine, ambayo Wakristo wa kwanza waliipenda sana, inasema: "Jiwe lililokataliwa na waashi limekuwa jiwe kuu la msingi" (Zab 117:22). Yesu alikataliwa na kusulubiwa nje ya malango ya mji wake. Lakini kwa sasa amekuwa ni Jiwe kuu la pembeni ambalo juu yake Mwenyezi Mungu amejenga upya ulimwenguni na kwamba, vijana ni mawe ya thamani katika ujenzi wa ubinadamu mpya. Kumbe, wanapaswa kuhisi kwamba, wanakubalika na kupendwa na jamii na hivyo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa mabadiliko mapya katika maisha yao.

Vipaumbele: Utu heshima na haki msingi za binadamu
Vipaumbele: Utu heshima na haki msingi za binadamu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, vijana wanapendwa na kuthaminiwa na Mama Kanisa, walimwengu waanawataka kama ilivyo elimu na wanasiasa wanayo hamu nao, jambo la msingi ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa hakika ulimwengu unahitaji kuona ushuhuda wa vijana unaoendelea kutendeka, kwa kuwa watu huru, wenye utu wao kama binadamu, ili kuchuchumia wito wa amani, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga maeneo mengi zaidi ya kuganga na kuwaponya waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana, kwa kuanzisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji na siasa za kijamii, kila mtu akipewa uzito anaostahili. Baba Mtakatifu amewaomba washiriki wa Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kwa Mwaka 2025, kumwombea ili utume wake uwe ni kwa ajili ya huduma ya matumaini kwa watu wote wa Mungu.

Kanisa ni Mama na Mwalimu: Utu na Heshima ya binadamu
Kanisa ni Mama na Mwalimu: Utu na Heshima ya binadamu   (@VATICAN MEDIA)

Itakumbukwa kwamba, Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sera na sheria wa kitaifa na kimataifa! Waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbalimbali za dunia. Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo miongoni mwa vijana!

Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Utu, heshima na haki msingi za binadamu   (@VATICAN MEDIA)

Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha. Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, Wakristo wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Kauli mbiu: Usiadhibu
Kauli mbiu: Usiadhibu   (@Vatican Media)

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbalimbali za dunia katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake. Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani, iwe ni fursa kwa familia kuhakikisha usalama wa watoto na vijana. Ikumbukwe kwamba, mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya yanapania kulinda na kudumisha utu, heshima sanjari na kuwakirimia watu matumaini na maisha bora kwa wote. Kwa upande wake Bwana Alfredo Mantovano, Naibu Katibu mkuu Baraza la Mawaziri la Serikali ya Italia katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV aweze kuzungumza na washiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kwa mwaka 2025, amekazia zaidi juu ya Injili ya matumaini baada ya mateso na mahangaiko makubwa kama ilivyoshuhudiwa na Paola Clericuzio kutoka katika Jumuiya ya San Patrignano na kwamba, hii ni changamoto ya kitamaduni na kiutu. Amekazia kuhusu umuhimu wa kuzuia, kuganga na kuponya; Dhamana na wajibu wa familia.

Dawa za Kulevya 2025

 

26 Juni 2025, 15:19