Papa Leo XIV: Majadiliano ya Kiekumene Yanaendelea Kushika Kasi Katika Ukweli
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Mama Kanisa anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Ni katika muktadha huu wa majadiliano ya kiekumene, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 28 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, unaoshiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Dominika tarehe 29 Juni 2025. Kumekuwepo na Mapokeo ya kubadilishana wajumbe wakati wa maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulo, Wasimamizi na waombezi wa Kanisa la Roma na wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Andrea, Mtume, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli umewasili mjini Roma tarehe 27 na utakuwepo hadi tarehe 29 Juni 2025. Hii pia ni fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, linalosimamia na kuratibu juhudi za kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake ameridhishwa na majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika ukweli kati ya Makanisa haya mawili, jitihada zilizoanza kushika kasi wakati Mtakatifu Paulo VI alipokutana na Patriaki Athenagoras, na baadaye majadiliano haya yakaendelezwa na waandamizi wao, kama sehemu ya mchakato wa upatanisho, ili kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya karibu kati ya Makanisa haya mawili. Ujenzi wa umoja wa Kanisa unaweza kupatikana kwa msaada wa Mwenyezi Mungu unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana kwa makini pamoja na majadiliano ya udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, yuko tayari kusikiliza mawazo kutoka katika Kanisa la Kiothodox na daima ataendelea kuwashirikisha Maaskofu wa Kanisa Katoliki “Kwa maana Maaskofu wote huwajibika kukuza na kuhifadhi umoja wa imani na nidhamu iliyo moja kwa Kanisa lote, tena huwafundisha waamini wawe na upendo kwa Mwili wote wa Fumbo la Kristo.” LG 23.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wajumbe kwa uwepo wao na hasa katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani. Amewaomba kumfikishia salam na matashi mema Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na Sinodi Takatifu na kwamba, Kanisa Katoliki nalo kwa upande wake, litatuma wawakilishi katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Andrea inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Kwa maombezi ya watakatifu hawa walioungana katika umoja mkamilifu huko mbinguni, wawasindikize viongozi wa Makanisa katika jitihada zao za huduma kwa Injili ya Kristo Yesu.