Papa Leo XIV Jubilei ya Miaka 350 ya Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV amemteua Kardinali Bustillo François-Xavier, O.F.M. Conv. Askofu wa Jimbo Katoliki la Ajaccio, lililoko nchini Hispania kuwa Mwakilishi wake maalum katika kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, changamoto kubwa kwa wakati huu ni kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazoendelea kusiginwa katika ulimwengu mamboleo. Jubilei hii ni muda muafaka kwa waamini kuendelea kukua na kukomaa katika kufanana na Kristo Yesu, kudumisha umoja na uaminifu kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea, kumbe, matukio haya mawili yanaweza kuwa ni chemchemi ya neema na baraka kwa watu wa Mungu. Ni fursa ya kuendeleza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na kudumisha kazi za kichungaji. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 27 Juni 2025, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku Maalum ya Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha ya Mapadre. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema uteuzi wa Kardinali Bustillo François-Xavier, O.F.M. Conv. Ni kutaka kuonesha hisia na ukaribu wake kwa watu wa Mungu katika maadhimisho haya na kwamba, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na katika mahubiri yake akazie zaidi amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, mto wa maji ya uzima yanayoponya majeraha ya mwanadamu, ili hatimaye, watu wa Mungu waweze kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu unaosimikwa katika: haki, umoja na udugu wa kibinadamu.
Toba na upatanisho ni wazo linalojitokeza mara nyingi katika Maandiko Matakatifu na katika Agano la Kale limechukua mwelekeo wa kijamii wa fidia kwa ovu lililotendwa. Hii ndiyo Sheria ya Musa inayotoa fursa ya kurejesha kile kilichoibiwa au kujenga tena uhusiano uliosababishwa na ovu lililotendwa au kulipa fidia kwa kumtia mtu hasarani. Rej. Kut 22: 1-15 na Law 6:1-7. Hiki kilikuwa ni kitendo cha haki kilichojenga na kulinda maisha jamii. Katika Agano Jipya mwelekeo huu unakuwa ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kiroho ndani ya mfumo wa Ukombozi ulioletwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawa ni fidia ya dhambi za walimwengu. Hiki ni kieleelzo cha neema, rehema na upendo wa Mungu kwa wenye dhambi. Kumbe, malipizi huchangia kukoleza upatanisho kati ya watu wenyewe, na pia upatinisho na Mwenyezi Mungu kwa sababu uovu unaotendwa dhidi ya jirani zako ni dhambi inayotendwa pia dhidi ya Mwenyezi Mungu. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari mmoja wapo alipomchoma Kristo Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama ya Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Mwezi Juni, umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya maisha na utakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumpelekea Kristo Yesu: shida, mahangaiko na matamanio yao halali, kwa imani na matumaini, naye atasikiliza na kujibu kilio chao! Huu ni mwaliko wa kumpelekea Kristo Yesu, amana na utajiri wao; udhaifu na mapungufu ya maisha, bila kusahau mahangaiko ya jirani zao, kwa hakika Kristo Yesu atasikiliza na kujibu kilio chao. Waendelee kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kukuza uchumi unaosimikwa katika kanuni maadili, utu wema na haki. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 alitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa ni Siku ya Kuombea: Toba, Wongofu na Utakatifu wa mapadre. Yote haya ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko mjini Paray-le-Monial, nchini Ufaransa na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Maadhimisho haya yalianza kutimua vumbi tarehe 27 Desemba 2023 na yanahitimishwa rasmi tarehe 27 Juni 2025 katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kurejesha upendo kwa upendo” tema inayomwilishwa katika hija mbalimbali, maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa pamoja na mikutano ambayo imekuwa ikiendeshwa kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, changamoto kubwa ni kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazoendelea kusiginwa katika ulimwengu mamboleo. Ni vyema waamini wakajitambua kwamba, wao ni wadhambi, tayari kukiri udhaifu wao na kuomba msamaha. Sadaka ya Kristo Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa binadamu mdhambi, chachu ya upatanisho kati ya Mwanadamu na Mwenyezi Mungu na kati ya binadamu wenyewe. Mwenyezi Mungu anaendelea kutoa machozi kutokana na kusiginwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia na hata kati ya watu wateule na watakatifu wa Mungu.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya, inaonesha kwamba, makovu yanaweza kugangwa na kuponywa, ikiwa kama kuna utashi wa kutenda hivyo kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kurejesha amani na utulivu wa moyo! Toba na wongofu wa ndani pamoja na mambo mengine, inafumbatwa katika maisha ya mwamini kwa kutambua kwamba, ni mdhambi na anapaswa kuomba msamaha wa dhambi alizotenda na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko tayari kumpokea mwamini aliyevunjika na kupondeka moyo, ili aweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Toba na msamaha ni kutambua dhambi zilizotendwa kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu aliyetambua ndani mwake kwamba, amekosa juu ya mbingu na mbele ya Baba yake Mwenye huruma. Rej. Lk 15:21. Kuomba msamaha kunafungua majadiliano yanayopania pamoja na mambo mengine, kurejesha mahusiano na mafungamano katika upendo wa kidugu, tayari kuonja faraja, pamoja na kupokea msamaha unaotolewa na huo ni mwanzo wa kuchipua tena fadhila ya upendo ili kuganga madonda ya moyo! Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, alimwomba, watu wafanye toba na malipizi kwa maondoleo ya dhambi zinazoendelea kuutesa Moyo wake Mtakatifu.