MAP

Maadhimisho ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji Msimamizi na Mwombezi wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta: Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na Mwanadamu kutakatifuzwa Maadhimisho ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji Msimamizi na Mwombezi wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta: Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na Mwanadamu kutakatifuzwa  (ANSA)

Papa Leo XIV: Sherehe ya Kuzaliwa Kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji Msimamizi na Mwombezi wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta anasema, lengo kuu ni kumtukuza Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa njia ya huduma makini, kama Kristo Yesu alivyotoa kwa maskini. Hawa ni watu wanaopaswa kutangaziwa Habari Njema na kushuhudiwa upendo wa Mungu unaookoa, kufariji na kusimikwa katika udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Huyu ni Mtakatifu pekee, ambaye Mama Kanisa anaadhimisha Siku yake ya kuzaliwa hapa duniani, ukiachilia mbali Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria. Hizi ni nguzo msingi zinazoaminika katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Yohane Mbatizaji, alitumwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni shuhuda wa nuru, ili watu wasitembee tena gizani, watubu na kumwongokea Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji Msimamizi na Mwombezi wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” anasema, lengo kuu ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa njia ya huduma makini, kama Kristo Yesu alivyotoa kwa maskini na wale wote waliokuwa wanatengwa na jamii. Hawa ni watu wanaopaswa kutangaziwa Habari Njema na kushuhudiwa upendo wa Mungu unaookoa na kufariji; upendo unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu; upendo unaowakirimia watu wa Mungu furaha na hivyo kuendelea kuwarithisha imani inayotoka kwa Mungu ambaye kimsingi ni upendo, anayeonesha ukaribu wake. Watambue kwamba wao ni walinzi wa imani na huduma ya maskini. “Tuitio fidei et l’obsequium pauperum.”

Papa Leo XIV akiwa na wanachama wa Chama cha Kitume cha Kijeshi
Papa Leo XIV akiwa na wanachama wa Chama cha Kitume cha Kijeshi   (@VATICAN MEDIA)

Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” kimeendelea kufanya kazi za kitume sehemu mbalimbali za dunia kama chemchemi ya huruma na upendo. Waamini wanapaswa kujitahidi kumfuasa na hatimaye kufika kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hiki ni kiini cha Habari Njema inayopaswa kutangazwa kwa njia ya unyenyekevu; udugu; imani na utii kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulitegemeza Kanisa kwa nyakati mbalimbali za maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni kielelezo makini cha uhusiano wa kina kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewapongeza wanachama wa Chama hiki cha kitume kwa kuhitimisha kuandika tafakari juu ya Katiba ya Chama chao, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwa makini ili kamwe wasimezwe na malimwengu, kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, kama chanzo na asili ya chama chao cha kitume.

Huduma kwa maskini ni kati ya vipaumbele vya Chama cha Malta
Huduma kwa maskini ni kati ya vipaumbele vya Chama cha Malta   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waendelee kujikita katika toba na wongofu wa ndani sanjari na huduma makini kwa watu wa Mungu, ushuhuda uliotolewa na Mwenyeheri Gerardi na hivyo kuendelea kujitakasa. Malezi na majiundo ni mambo msingi, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Haya ni malezi na majiundo yanayokita mizizi yake katika: Sala binafsi, Liturujia ya Kanisa inayorutubishwa na ukimya pamoja na upweke chanya, kwa ajili ya kujisadaka na kujitoa bla ya kujibakiza kwa ajili ya huduma, kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu. Wajenge na kudumisha maisha ya kijumuiya yanayosimikwa katika nadhiri ya: Ufukara, Utii na Usafi wa moyo, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Watu wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu, na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyokita mizizi yake kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Mtakatifu Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.

Wao ni walinzi wa imani na huduma ya maskini
Wao ni walinzi wa imani na huduma ya maskini   (@Vatican Media)

Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Hili ni tukio ambalo lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Kristo Yesu akiwa katikati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Kristo Yesu akajionesha kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji ni kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu.

Yohane Mbatizaji

 

24 Juni 2025, 15:05