Ajali ya Ndege India Yauwa Watu Zaidi ya 240 Papa Leo XIV Atuma Salam za Rambirambi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ndege ya Shirika la Ndege la India, Air India AI171, aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, iliyokuwa na abiria 232 na wafanyakazi 12, iliyokuwa ikielekea kwenye uwanja wa ndege wa London Gatwick nchini Uingereza, siku ya Alhamisi, tarehe 12 Juni 2025 ilianguka katika eneo la makazi ya watu huko Meghani Nagar dakika chache baada ya kuanza safari kutoka uwanja wa ndege wa Ahmedabad, Magharibi mwa India. Ni katika muktadha wa masikitiko haya makubwa, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anasema kwamba, amesikitishwa sana na taarifa ya ajali hii ya ndege, anapenda kutuma salam zake za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mkubwa.
Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake; anapenda kuwatia shime, wale wote waliojihusisha na zoezi la uokoaji. Mwishoni, anapenda kuziweka roho za marehemu wote katika huruma ya Mungu, ili wapumzike kwenye usingi wa amani. Amina. Wakati huo huo, Kamishna wa Polisi wa Ahmedabad GS Malik ameliambia Shirika la Habari la ANI kuwa raia wa Uingereza Vishwash Kumar Ramesh ndiye abiria pekee aliyenusurika kwenye ndege ya Boeing 787-8 iliyokuwa ikielekea London na kwamba yuko hospitalini na anaendelea na matibabu. Kulikuwa na raia wa India 169, Waingereza 53, raia saba wa Ureno na Mcanada mmoja kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick, nchini Uingereza. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X amesema ameshtushwa sana na ajali hiyo ya ndege, imehuzunisha na kuwavunja watu moyo!