Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti: Injili ya Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kila Mwaka ifikapo tarehe 31 Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea binamu yake Elizabeti Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeti Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Wafranciskani walianza kuiadhimisha Sikukuu hii tangu mwaka 1263. Kunako mwaka 1389 Papa Urbano VI aliiweka ili iadhimishwe kwa Kanisa zima. Na Mtakatifu Paulo VI akaihamishia Sikukuu hii tarehe 31 Mei kati ya Sherehe ya Kupashwa Habari ya Kuzaliwa Bwana, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Machi sanjari na Sherehe ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji inayoadhimishwa tarehe 24 Juni ya kila mwaka. Sikukuu hii kwa Mwaka 2025 inabeba uzito wa pekee kwani ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 31 Mei 2025: Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti, anatarajia kutoa kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Rej. Lk 1:36. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumtembelea Elizabeti, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano bora wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha! Elizabeti anampokea Bikira Maria kama Mama wa Bwana wake. Rej. Lk 1:39-56. Hii ni Sikukuu ya utenzi wa Bikira Maria unaojikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni tukio la imani na upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji.
Mtakatifu Efremu wa Siro anasema, hapa Bikira Maria anakutana na mama tasa aliyekuwa mjamzito; Mtoto wa tasa anaruka kwa furaha tumboni mwa Mama yake, matendo makuu ya Mungu katika maadhimisho ya Sikukuu hii ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti. Huu ni mwaliko wa kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa Mungu na kwa ajili ya jirani, jambo ambalo lingeweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio linalosheheni furaha inayoyajaza maisha ya watu kutokana na ujasiri wa mwanamke mwenye uwezo wa kuona, kusikia na kuguswa na mahitaji ya ndugu yake na hivyo, kuwa ni chemchemi ya furaha inayowakutanisha ndugu hawa wawili. Haya ndiyo yanayosimulia na Mwinjili Luka; Injili inayobubujika furaha inayoijaza nyoyo za watu! Hii ni nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu: Bikira Maria anakutana na binamu yake Elizabeti; Kristo Yesu anakutana na Yohane Mbatizaji; Agano la Kale na Agano Jipya yanakutana. Kwa njia ya Bikira Maria hata Mama Kanisa anashiriki katika kuimba Utenzi wa Bikira Maria “Magnificat” Rej. Lk 1: 46-55. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakristo kuwa ni watu wenye nyuso za furaha na tabasamu la kukata na shoka, ujumbe unaosheheni Liturujia ya Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti kwa ajili ya huduma.
Bikira Maria ni kielelezo cha mwanamke msikivu, anayetafakari na kutenda kwa ujasiri na kwa haraka, kielelezo cha ujasiri na huduma; kama inavyojionesha kwa wanawake wengi wajasiri walioko ndani ya Kanisa. Hawa ni wanawake wanaosimama kidete kutoa elimu kwa watoto wao pamoja na kuhudumia wagonjwa ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Kwao huduma inakuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini.Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria na Elizabeti wanakutana katika kisima cha furaha, imani na matumaini kama kielelezo cha huduma makini kwa jamii, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani, jambo ambalo linaweza kuleta mabadiliko makubwa duniani. Kukutana ni sehemu ya maisha ya Kikristo yanayojikita katika huduma inayowasukuma Wakristo kutoka katika uchoyo na ubinafsi wao, ili kuwahudumia jirani zao kwa upendo. Mwenyezi Mungu yuko kati ya watu wake, ili kuwahudumia na kuwakutanisha katika kisima cha furaha, upendo na matumaini.