Papa Leo XIV: Umuhimu wa Kukuza Na Kudumisha Uhuru wa Vyombo Vya Habari
Na Sarah Pelaji – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 12 Mei 2025 kwenye Ukumbi wa Paulo VI amezungumza na wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii Kimataifa waliofika mjini Vatican kushuhudia uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Papa Leo XIV ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa mchango wao mkubwa ambao ni neema kwa Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani. Aidha ameonesha mshikamano wa Mama Kanisa na waandishi wa habari waliofungwa au kupotea katika mazingira tatanishi akieleza kuwa, waandishi wa habari ni wahudumu wa ukweli; umuhimu wa kutumia vyema rasilimali muda. Pia amekazia umuhimu wa mawasiliano kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa; Matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” na kwamba, Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kukuza na kudumisha kiu ya haki na upendo, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, mawasiliano yasaidie kujenga amani. Amekazia kwa namna ya pekee kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
Papa Leo XIV ambaye ana uraia pacha wa Marekani na Perù, alipokelewa kwa shangwe na vifijo vya sauti za waandishi wa habari pamoja na familia zao alipoingia katika ukumbi wa Paulo VI ili kutoa hotuba yake ya kwanza mbele ya waandishi wa habari wapatao takribani 6,000 walioonesha kuguswa na maneno yake mazito katika hotuba yake ambayo kimsingi ilijikita katika shukrani na kujenga mshikamano na vyombo vya habari duniani huku akivisisitiza kuchochea Injili ya amani badala ya chuki na migogoro. Waandishi wa habari walionesha shauku ya kukutana na Papa mpya Leo XIV wa Shirika la Kimataifa la Mtakatifu Augustino mwenye umri wa miaka 69 huku wakiguswa na maneno katika hotuba yake hasa alipowashukuru wanahabari kwa kuwa mstari wa mbele kuhabarisha na kutoa taarifa wakati wa maadhimisho ya Juma kuu, Kifo na Maziko ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
"Kwa hivyo, nirudie leo kuhimiza mshikamano wa Kanisa na waandishi wa habari ambao wamefungwa kwa kutafuta na kuripoti ukweli hivyo ninaomba waachiliwe" Papa Leo XIV alisema. Takribani waandishi wa habari 550 walikuwa wanashikiliwa kote ulimwenguni mnamo Desemba 2024, kulingana na “Reporters Without Borders”, shirika lisiloegemea upande wowote ambalo linafanya kazi ya kuwalinda waandishi wa habari. Pia amewataka waandishi wa habari kuepuka lugha za kiitikadi au upendeleo ambazo zinaweza kuchochea chuki. "Hatuhitaji mawasiliano ya sauti za wenye nguvu bali mawasiliano ambayo yana uwezo wa kusikiliza na kukusanya sauti za wanyonge ambao hawana sauti," alisema Papa Leo XIV.
Amesema kuwa, wajibu wa waandishi wa habari duniani si tu kutoa taarifa bali kujikita katika kuimarisha mila na desturi njema zinazoijenga jamii. "Mko mstari wa mbele kuripoti juu ya migogoro na matarajio ya amani, juu ya ukosefu wa haki na umaskini, na juu ya kazi za watu wengi wanaojikita kujenga ulimwengu bora. Hivyo ninawaomba mchague kwa uangalifu na kwa ujasiri njia bora ya mawasiliano kwa ajili ya amani duniani." Papa Leo XIV alimalizia hotuba yake kwa kuwataka waandishi wa habari kuchagua njia ya mawasiliano kwa ajili ya kujenga amani kisha akaaagana nao kwa kupeana mikono na baadhi ya waliohudhuria. Katika mkutano wake huo wa kwanza na waandishi wa habari, Papa Leo XIV hakujibu maswali, kama ilivyo kawaida katika mikutano ya waandishi wa habari za Papa.
Pia imeelezwa kuwa, Mtangulizi wa Baba Mtakatifu Leo XIV, Hayati Papa Francisko, pia alikataa kujibu maswali katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari mnamo mwaka 2013. Mapapa watano wa mwisho wamekutana na vyombo vya habari katika siku za kwanza za utume wao kama Makhalifa wa Mtakatifu Petro. Tukio hilo linaonesha jinsi ambavyo Vatican inavyotambua thamani ya mawasiliano ya umma na tamaa yake ya kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye ni Papa wa kwanza kutoka Marekani kuliongoza Kanisa Katoliki duniani lililo na waamini wake takribani bilioni 1.4, ametumia siku za kwanza za utume wake kuahidi kujipatanisha na watu wa kawaida, huku akikemea vita na migogoro.