Papa Leo XIV:Uchaguzi wa jina kwa changamoto ya hadhi,haki na kazi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Leo XIV, ni jina ambalo linaonesha mpango mzima wa upapa wake. Ni Papa mwenyewe kwa jina Robert Prevost, aliyeeleza sababu kuu ya uchaguzi wa jina lake katika mkutano wake wa kwanza na Makardinali, yaani Baraza la Makardinali, sio tu wale waliomchagua katika Mkutano Mkuu, lakini hata wale ambao hawakuwa katika chumba cha mkutano wa uchaguzi ambao alikutana nao Jumamosi tarehe 10 Mei 2025 nyuma ya milango iliyofungwa katika Ukumbi wa Sinodi mjini Vatican. Kwa ufupo jina lake linarejea dhahiri kwa Papa Leo XIII ambaye, mwishoni mwa karne ya 19, pamoja na waraka wa kihistoria wa Rerum Novarum alishughulikia suala la kijamii katika muktadha wa mapinduzi makubwa ya kwanza ya viwanda na ambapo Papa alieleza changamoto ya sasa ambayo pia inajumuisha kasi ya kidijitali(Akili Nunde).
Baba Mtakatifu Leo XIV alisema: "Nawasalimu na kuwashukuru nyote kwa mkutano huu na kwa siku zilizotangulia, wenye uchungu kwa kumpoteza Hayati Baba Mtakatifu Francisko, majukumu makali yaliyowakabili pamoja na wakati huo huo, sawasawa na ahadi ambayo Yesu mwenyewe alituahidi, kwa wingi wa neema na faraja katika Roho (rej. Yh 14:25-27). Ninyi wapendwa Makardinali, ni washiriki wa karibu zaidi wa Papa, na hii ni faraja kubwa kwangu kwa kukubali nira ambayo ni wazi zaidi ya uwezo wangu, kwani ni zaidi ya mtu mwingine yeyote. Uwepo wenu unanikumbusha kwamba Bwana, aliyenikabidhi utume huu, haniachi peke yangu katika kubeba jukumu lake. Ninajua kwanza kabisa kwamba ninaweza daima kutegemea msaada wake, msaada wa Bwana, na, kwa Neema na Maandalizi yake, juu ya ukaribu wenu na ule wa kaka na dada wengi ulimwenguni kote wanaomwamini Mungu, wanaopenda Kanisa na kumuunga mkono Mfuasi wa Kristo kwa sala na matendo mema."
Baba Mtakatifu Leo alisema: Ninashukuru Dekano wa Baraza la Makardinali, Kardinali Giovanni Battista Re, anastahili kupigiwa makofi hata moja… walimpigia makofi… ambaye kwa hekima, tunda la maisha marefu na miaka mingi ya imani katika huduma ya Makao makuu ya Kitume , alitusaidia sana katika wakati huu. Ninamshukuru Camerlengo wa Kanisa Katoliki la Roma, Kardinali Kevin Joseph Farrell, ambaye yuko hapa … walimpongeza …kwa jukumu la thamani na la kudai sana alililojikita nalo wakati wa Kiti wazi na Baraza la Makardinali. Pia ninaelekeza mawazo yangu kwa ndugu Makardinali ambao, kwa sababu za kiafya, hawakuweza kuwepo na ninaungana nanyi katika ushirika wa upendo na sala."
Kumuombea hayati papa Francisko
Papa Leo XIV alisema "Kwa wakati huu, kwa huzuni na furaha, katika mwanga wa Pasaka, napenda tuangalie kwa pamoja kifo cha Hayati Baba Mtakatifu Francisko na kwenye Mkutano Mkuu kama tukio la Pasaka, hatua ya msafara mrefu ambao kupitia kwake Bwana anaendelea kutuongoza kuelekea utimilifu wa maisha; na kwa mtazamo huu tunamkabidhi “Baba mwenye rehema na Mungu wa faraja yote” (2Kor 1:3) roho ya marehemu Papa na pia mustakabali wa Kanisa."
Amefufuka yuko hapa
Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Amefufuka, yupo katikati yetu, ambaye analinda na kuongoza Kanisa na ambaye ataendelea kuhuisha katika matumaini, kwa njia ya upendo “uliomiminiwa mioyoni kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye tulipewa(Rm 5,5).
Tumeona ukuu wa kweli wa Kanisa wakati wa kifo cha Papa
Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kwamba: Ni juu yetu kuwa wasikilizaji wasikivu wa sauti yake na wahudumu waaminifu wa mipango yake ya kuokoa, tukikumbuka kwamba Mungu anapenda kuwasiliana mwenyewe, zaidi ya sauti ya radi na tetemeko la ardhi, katika “mnong’ono wa upepo mtulivu” ( 1 Wafalme 19:12 ) au, kama wengine wanavyotafsiri, kwa “sauti tulivu ya ukimya”. Huu ni mkutano muhimu, si wa kukosa, na ambao tunapaswa kuwaelimisha na kuwasindikiza Watu wote watakatifu wa Mungu waliokabidhiwa kwetu. Katika siku za hivi karibuni, tumeweza kuona uzuri na kuhisi nguvu ya jumuiya hii kubwa, ambayo kwa upendo na kujitolea sana ilimuaga na kuomboleza Mchungaji wake, ikiandamana naye kwa imani na maombi wakati wa kukutana kwake kwa hakika na Bwana. Tumeona ni nini ukuu wa kweli wa Kanisa, ambalo linaishi katika aina mbalimbali za washiriki wake waliounganishwa na Kichwa kimoja, Kristo, "mchungaji na mlezi" (1 Petro 2:25) mchungaji wa roho zetu.
Kurudi katika Evangelii gaudium
Papa mpya alisisitiza kuwa: Na katika suala hili, ningependa tupyaishe kwa pamoja leo ufuasi wetu kamili, katika safari hii, kwa njia ambayo Kanisa la kiulimwengu limekuwa likiifuata kwa miongo kadhaa baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Papa Francisko amekumbuka na kusasisha kwa ustadi zaidi yaliyomo katika Waraka wa Kitume Evangelii gaudium, ambayo ningependa kusisitiza mifano kadhaa ya kimsingi: kurudi katika ukuu wa Kristo katika kutangaza (kifungu. 11); uwongofu wa kimisionari wa jumuiya nzima ya Kikristo (rej. kifungu 9); ukuaji wa ushirikiano na kisinodi (kifungu. 33); umakini na maana ya imani (sensus fidei) (reje kifungu cha 119-120), hasa katika maumbo yake mahususi na jumuishi, kama vile ibada maarufu za watu wa Mungu(rej. kifungu 123); utunzaji wa upendo kwa walio wa mwisho na waliotupwa (kifungu 53); mazungumzo ya ujasiri na ya kuaminiana na ulimwengu wa sasa katika vipengele na uhalisia wake mbalimbali (taz. kifungu 84; Mtaguso wa II wa Vatican katika Katiba ya Kichungaji Gaudium et Spes, 1-2).
Sababu za kuchagua kuitwa Leo XIV
Kwa kusisitiza zaidi alibanisha kuwa "Hizi ni kanuni za Injili ambazo daima zimehuisha na kuhamasisha maisha na kazi ya Familia ya Mungu, maadili ambayo kwayo uso wa huruma wa Baba umejidhihirisha na unaendelea kujidhihirisha katika Mwana aliyefanywa mwanadamu, tumaini kuu la mtu ye yote anayetafuta ukweli, haki, amani na udugu kwa dhati (taz.Benedikto XVI katika Waraka wake wa Spe salvi, 2; Hati ya Papa Francisko ya kutangaza Jubilei ya Spes non confundit, 3 matumaini hayakatishi tamaa). Hasa kwa sababu ya kuhisi kuitwa kuendelea katika njia hii, nilifikiria kuchukua jina la Leo XIV.
Kuna sababu kadhaa, lakini moja kuu ni kwa hakika, Papa Leo XIII, pamoja na Warka wake wa kihistoria wa Rerum novarum, alishughulikia suala la kijamii katika muktadha wa mapinduzi makubwa ya kwanza ya viwanda; na leo Kanisa linamtolea kila mtu urithi wake wa mafundisho ya kijamii ili kukabiliana na mapinduzi mengine ya viwanda na maendeleo ya Akili Mnemba (AI), ambayo huleta changamoto mpya kwa ajili ya ulinzi wa hadhi, haki na kazi ya binadamu."
Hitimisho:Mwali mkuu wa imani na upendo:bila msaada wa Mungu hakuna kitu
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa: “Ndugu wapendwa, ningependa kuhitimisha sehemu hii ya kwanza ya mkutano wetu kwa kufanya mapendekezo yangu mwenyewe - kwenu pia - tumaini ambalo Mtakatifu Paulo VI, mnamo 1963, aliweka mwanzoni mwa Huduma yake ya Petro: "Na ipite juu ya ulimwengu wote kama mwali mkuu wa imani na upendo unaowaangazia watu wote wenye mapenzi mema, kuwaangazia njia za ushirikiano wa pande zote, na kuvuta juu ya wanadamu, tena na daima, utajiri mwingi wa kimungu, nguvu yenyewe ya Mungu, bila msaada wake, hakuna kitu halali, na hakuna kitu kitakatifu."(Ujumbe wa familia nzima ya kibinadamu Qui fausto die, 22 Juni 1963). Na hizi pia ziwe hisia zetu, zifasiriwe katika maombi na kujitolea, kwa msaada wa Bwana. Asante!” Alihitimisha