Papa Leo XIV:Mungu haoni haya,anafanya makao yake ndani mwetu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa mara ya kwanza, Papa leo XIV amechungulia kwenye dirisha la Jumba la Kitume tangu kuchaguliwa kwake. Mara ya mwisho wa Sala ya Malaika wa Bwana ya Hayati Papa Francisko katika Jumba hilo la Kitume ilikuwa ni tarehe 2 Februari 2025(karibu miezi minne iliyopita). Katika fursa ya Dominika ya VI ya Pasaka Mwaka C, tarehe 25 Mei 2025, Baba Mtakatifu akianza tafakari yake alisema: Wapendwa kaka na dada, Dominika njema! Bado niko mwanzoni mwa huduma yangu katikati yenu na ninapenda awali ya yote kuwashukuru kwa upendo wenu ambao mnanionesha, wakati nikiwaomba mnisindikize kwa sala zetu na ukaribu.
Katika yote hayo kwa Bwana, tunaitwa katika njia ya maisha kama ilivyo katika safari ya imani, tunahisi wakati mwingine kutostahili. Pamoja na hayo ni katika Injili ya Dominika hii (Yh 14,23-29) ambayo inatueleza kuwa hatupaswi kutazama nguvu zetu, lakini huruma ya Bwana ambaye alituchagua, kwa uhakika kwamba Roho Mtakatifu anatuongoza na kutufundisha kila kitu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaeleza waamini na mahujaji waliofika kutoka pande za dunia na Italia katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, kuwa Mitume ambao katika mkesha wa kifo cha Mwalimu, walikuwa na wasiwasi na uchungu na wakauliza ni jinsi gani wataweza kuendelea na kushuhuda Ufalme wa Mungu, Na Yesu alitangaza zawadi ya Roho Mtakatifu , kwa ahadi ya mshangao: “ Mtu akinipenda, atalishika neno langu na Baba yangu atampenda ; nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake(Yh 14, 23.)
Kwa njia hiyo Yesu anawaondolea wafuasi wake kila aina ya huzuni na wasi wasi na kuweza kusema: Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwa na woga”(Yh 14,27) Ikiwa tunabaki katika upendo wake, kiukweli Yeye mwenyewe anatengeneza makao yake ndani mwetu, maisha yetu yanageuka hekalu la Mungu na kwa upendo huo unatuangaza, unatengeneza nafasi katika namna yetu ya kufikiria na katika chaguzi zetu, hadi kujipanua hata kuelekea wengine, na kuangaza hali zote za maisha yetu.” Baba Mtakatifu Leo XIV kwa njia hiyo amesisitiza kuwa makao hayo ya Mungu katika sisi ndiyo hasa zawadi ya Roho Mtakatifu, ambaye anatushika mkono na kutufanya tufanye uzoefu, hata katika maisha ya kila siku, kwa uwepo na ukaribu wa Mungu kwa kufanya makao yake ndani mwetu.
Ni vizuri kwa kutazama katika wito wetu, Papa amesema na kuongeza “ katika hali halisi na kwa watu ambao tulikabidhiwa, kwa kazi yetu tunayopeleka mbele, kwa huduma ya Kanisa, kila mmoja wetu anaweza kusema kwa imani: Hata kama mimi ni mdhaifu, Bwana haoni haya ya ubinadamu wangu, badala yake anakuja kukaa ndani mwangu. Yeye ananisindikiza kwa Roho wake, ananiangazia na kunifanya niwe chombo cha upendo wake kwa wengine, kwa ajili ya jamii na kwa ulimwengu.
Papa aidha alisisitiza kwa wapendwa wote kuhusu msingi huu wa ahadi na kwamba tutembee katika furaha ya imani , kwa ajili ya kuwa hekalu takatifu la Bwana. Tujitahidi kupelekea upendo wake kila mahali, kwa kukumbuka kuwa kila kaka na kila dada ni makao ya Mungu na kwa uwepo wake unajionesha hasa katika walio wadogo, katika masikini na wale wote ambao wanateseka, wakituomba kuwa wakiduta makini na wenye huruma. Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu Leo XIV albainisha: “ na tumkabidhi wote kwa maaombezi ya Maria Mtakatifu. Kwa kazi ya Roho, Yeye aligeuka kuwa “Makao matakatifu ya Mungu.”Pamoja naye hata sisi tunaweza kufanya uzoefu wa furaha ya kukaribisha Bwana na kuwa ishara na chombo cha upendo wake.