Papa Leo XIV Kutoa Daraja Takatifu ya Upadre Kwa Mapadre wa Jimbo Kuu la Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema kwamba, Mapadri wanaitwa na kuwekwa wakfu ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza… na watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu kwa njia ya Roho wake. Wahudumu wa Daraja Takatifu wamepewa mamlaka ya kutoa huduma hii bila ya mastahili yao na tena wamepewa bure (Mt 10:8.) Kwa hiyo, wahudumu wa Daraja Takatifu wanapaswa kutoa huduma yao ya utumishi kwa bidii na kwa nguvu zao zote bila masharti wala ubaguzi. Hata hivyo, kwa namna ya pekee, wamekabidhiwa hasa walio maskini na wanyonge zaidi. Ni vizuri viongozi wa Daraja Takatifu wakatafakari namna na jinsi wanavyotekeleza agizo hilo. Namna wanavyotoa huduma za kichungaji katika Jumuiya, Kigango, Parokia na pengine hata nje ya majimbo yao. Ni aina gani ya watu wanaokuwa nao karibu zaidi? Je? Maskini na wanyonge wanayo nafasi mioyoni mwao? Wahudumu wa Daraja Takatifu, inabidi wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya yule aliyewatuma (taz. Yn 4:34; 5: 30; 6:38.) Kazi ya Kimungu ambayo walichukuliwa na Roho Mtakatifu kwayo, inapita nguvu na uwezo pia hekima ya wanadamu; kwa sababu: “Mungu alivichagua vitu vidhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu” (1Kor 1:27.) Kwa hiyo, mhudumu wa Daraja Takatifu anapaswa kutambua udhaifu wake na kufanya kazi kwa unyenyekevu, akijihakikishia ni nini impendezayo Bwana na, hali amefungwa na Roho, anaongozwa katika yote na mapenzi yake yule anayetaka watu wote waokolewe; nayo mapenzi ya Mungu ataweza kuyagundua na kuyafuata katika mambo ya kila siku akiwatumikia kwa unyenyevu wote waliokabidhiwa kwake na Mungu kutokana na dhima anayotakiwa kutekeleza, na matukio mbalimbali ya maisha yake.
Kimsingi Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama alivyofanya Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 31 Mei 2025: Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti, anatarajia kutoa kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tukio hili linatanguliwa na mkesha wa Sala kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa kunogeshwa pia na shuhuda za Mapadre watarajiwa. Mashemasi hawa wanapewa Daraja Takatifu ya Upadre wakati Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti, yaani tarehe 31 Mei 2025. Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele.
Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeti Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Rej. Lk 1:36. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumtembelea Elizabeti, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano bora wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha! Elizabeti anampokea Bikira Maria kama Mama wa Bwana wake. Rej. Lk 1:39-56. Hii ni Sikukuu ya utenzi wa Bikira Maria unaojikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni tukio la imani na upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji. Mtakatifu Efremu wa Siro anasema, hapa Bikira Maria anakutana na mama tasa aliyekuwa mjamzito; Mtoto wa tasa anaruka kwa furaha tumboni mwa Mama yake, matendo makuu ya Mungu katika maadhimisho ya Sikukuu hii ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti. Huu ni mwaliko wa kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa Mungu na kwa ajili ya jirani, jambo ambalo lingeweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio linalosheheni furaha inayoyajaza maisha ya watu kutokana na ujasiri wa mwanamke mwenye uwezo wa kuona, kusikia na kuguswa na mahitaji ya ndugu yake na hivyo, kuwa ni chemchemi ya furaha inayowakutanisha ndugu hawa wawili. Haya ndiyo yanayosimulia na Mwinjili Luka; Injili inayobubujika furaha inayoijaza nyoyo za watu! Hii ni nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu: Bikira Maria anakutana na binamu yake Elizabeti; Kristo Yesu anakutana na Yohane Mbatizaji; Agano la Kale na Agano Jipya yanakutana. Kwa njia ya Bikira Maria hata Mama Kanisa anashiriki katika kuimba Utenzi wa Bikira Maria “Magnificat” Rej. Lk 1: 46-55.