MAP

Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza wajumbe wa “Arena di Pace” kwa kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya amani dhidi ya utamaduni wa kifo Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza wajumbe wa “Arena di Pace” kwa kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya amani dhidi ya utamaduni wa kifo   (ANSA)

Papa Leo XIV: Jengeni na Kudumisha Utamaduni wa Injili ya Amani

Papa Leo XIV katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujizatiti katika kutafuta na kudumisha amani, inayowawezesha watu kushikamana na hivyo kufanya kazi kwa pamoja. Umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kujenga utamaduni wa amani dhidi ya vitendo vya kigaidi, vita, biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, ili kuheshimiana na kuthaminiana. Ili kujenga na kudumisha Injili ya amani kuna haja ya kujenga taasisi za amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kunako tarehe 18 Mei 2024 wajumbe wa “Arena di Pace” walikutana na kuzungumza na Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Wajumbe wa “Arena di Pace” wanaundwa na Kanisa la Jimbo Katoliki la Verona pamoja na Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, maarufu kama Wamisionari wa Comboni wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, mchakato wa maendeleo endelevu unaofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa unakuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wake, kwa kukazia misingi ya haki, amani na maridhiano. Ujumbe wa watu 300 wa “Arena di Pace” kutoka Verona, ukiongozwa na Askofu Domenico Pompili, Ijumaa tarehe 30 Mei 2025, umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujizatiti katika kutafuta, kujenga na kudumisha Injili ya amani, inayowawezesha watu kushirikiana na kushikamana na hivyo kufanya kazi kwa pamoja. Umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kujenga utamaduni wa amani dhidi ya vitendo vya kigaidi, vita, biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, ili kuheshimiana na kuthaminiana. Ili kujenga na kudumisha Injili ya amani kuna haja ya kujenga taasisi za amani.

Papa Leo XIV: Jengeni utamaduni wa Injili ya amani
Papa Leo XIV: Jengeni utamaduni wa Injili ya amani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza wajumbe wa “Arena di Pace” kwa kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya amani dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Amewakumbushia mauaji yaliyofanywa na Hamas na Jeshi la Israeli, wale waathirika, leo hii wamepatana na hivyo kuwa ni mashuhuda wa matumaini. Huu ni mwaliko kwa jamii kuendelea kujikita katika kuragibisha Injili ya amani, ili nyoyo na akili za watu, zijielekezwe katika Injili ya upendo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hija ya amani ni mchakato unaowahusu watu wengi kwa sababu amani ni tunu isiyoonekana, lakini ni kwa ajili ya wengi na kwamba, inaishi katika dhamiri ya watu, changamoto na mwaliko kwa watu kujizatiti kwa ajili ya mafao ya wengi.

Jengeni utamaduni wa Injili ya amani
Jengeni utamaduni wa Injili ya amani   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwamba, Injili ya amani inahitaji uvumilivu, kuanzia chini kwenda juu, kuanzia mahali pa chini sana, kuendelea katika jumuiya na hatimaye katika taasisi mahalia, kwa kujenga tabia ya kusikiliza; ili kutatua changamoto za kutokubaliana kwa kukubali uwepo wake, kujitahidi kuzielewa na hatimaye, kuzishughulikia kwa kujikita kwenye majadiliano katika ukweli na uwazi na huo ni mwanzo wa kuchipua kwa utamaduni na Injili ya amani inayowawezesha wadau mbalimbali kujielekeza katika huduma, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwa hakika hii inakuwa ni chemchemi ya matumaini. Katika ulimwengu unaosimikwa katika: vita, vitendo vya kigaidi, biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo, uvunjifu wa haki, watoto na vijana wa kizazi kipya wanapaswa kupata uzoefu na mang’amuzi ya Injili ya maisha, majadiliano pamoja na tabia ya watu kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu. Kimsingi ni watu wanaopaswa kushuhudia utamaduni wa amani katika ngazi mbalimbali na kwamba, wale ambao wamekoseshwa haki na amani, wasitumbukie katika ombwe la kutafuta kulipiza kisasi na kwa njia hii, watakuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya amani, kama mbinu mkakati na mtindo wa maisha unaowapambanua kwa maamuzi, mahusiano, mafungamano pamoja na matendo yao!

Jengeni Injili ya amani kwa kuheshimu utu, heshima na haki msingi
Jengeni Injili ya amani kwa kuheshimu utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Biblia Takatifu, Mama Kanisa na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni msingi katika ujenzi wa Injili ya amani duniani, dira na mwongozo unaohimiza ujenzi wa utamaduni wa amani. Hii ni dhamana ya watu wote wa Mungu wanaopaswa kuongozwa na haki, utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi. Amani ya kweli inasimikwa katika ujenzi wa taasisi za amani zinazosimikwa katika masuala ya: elimu, uchumi na mambo ya kijamii na wala si katika taasisi za kisiasa, kwa kujenga na kudumisha ari na moyo wa mshikamano! Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wajumbe wa “Arena di Pace” kutoka Verona kuendelea kujikita katika historia, kama chachu ya umoja na ushirika na kwamba,  udugu wa kibinadamu ni dhana inayopaswa kugunduliwa tena, kupendwa, kufanyiwa mang’amuzi, kutangazwa na kushuhudiwa mintarafu Injili ya matumaini ambayo yanawezekana kutokana na pendo la Mungu ambalo limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Rej Rum 5:5. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewasihi wajumbe hao waendelee kuwa wavumilivu na wadumifu na kwamba, anawasindikiza kwa sala na baraka zake za kitume.

Arena di Pace
30 Mei 2025, 16:13