ÐÓMAPµ¼º½

Dominika tarehe 11 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake. Dominika tarehe 11 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Ibada ya Misa Takatifu Kwenye Makaburi ya Mapapa Mjini Vatican

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema anamshukuru Mungu kwa kuanza utume wake, wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Kristo Yesu mchungaji mwema, changamoto na mwaliko wa kusikiliza sauti ya Mchungaji mwema, kumfahamu na hatimaye kumfuata. Kristo Yesu alisadaka maisha yake, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Siku ya 62 ya Kuombea Miito.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani yananogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini: Zawadi ya maisha kwa ukarimu. Hayati Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa tarehe 11 Mei 2025 anasema, wito ni zawadi ya thamani ambayo Mungu hupanda mioyoni, wito wa kutoka ndani ya nafsi yako ili kuanza safari ya upendo na huduma. Anawaalika waamini kuwa ni mahujaji wa matumaini kwa kusadaka maisha yao kwa ukarimu na kwamba, maisha ya wakfu ni alama ya matumaini ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuyapandikiza miongoni mwa watoto wake. Ukosefu wa fursa za ajira na tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kimaadili pamoja na mkanganyiko wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; ukosefu wa haki msingi za binadamu, uchoyo na ubinafsi pamoja na vita ni mambo yanayotishia maisha mema na adili, ndiyo maana waamini wanaitwa na kutumwa kama mahujaji wa matumaini.

Papa Leo XIV akisali kwenye Makaburi ya Mapapa mjini Vatican
Papa Leo XIV akisali kwenye Makaburi ya Mapapa mjini Vatican   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa Bendi za Muziki na Wasanii, kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko nchini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye alipata fursa ya kusali kwa kitambo kwenye Makaburi haya. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema anamshukuru Mungu kwa kuanza utume wake, wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Kristo Yesu mchungaji mwema, changamoto na mwaliko wa kusikiliza sauti ya Mchungaji mwema, kumfahamu na hatimaye kumfuata. Kristo Yesu alisadaka maisha yake, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima.

Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Mapapa mjini Vatican
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Mapapa mjini Vatican   (@Vatican Media)

Dominika tarehe 11 Mei 2025 nchi mbalimbali zimeadhimisha Siku ya Akina Mama Duniani. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kuwatakia kheri na baraka akina Mama mahali popote pale walipo. Upendo unaobubujika kutoka kwa akina mama, na hasa kwa watoto na wajukuu wao, ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Papa Leo XIV amesema, katika mikutano elekezi ya Makardinali wamegusia sana umuhimu wa kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za furaha ya Injili, bila kuwakatisha wengine tamaa, bali kuangalia njia muafaka itakayo wahamasisha vijana wengi zaidi kusikiliza na kuitikia sauti ya Kristo Yesu, Mchungaji Mwema, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani kwa hakika, Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema.

Walioshiriki katika Ibada ya Misa ya Papa Leo XIV
Walioshiriki katika Ibada ya Misa ya Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anatambua dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa watu wote wa Mataifa kama ilivyokuwa kwa Paulo na Barnaba walivyokuwa tayari kusikiliza sauti ya Kristo Mchungaji mwema, na hivyo wakajikita zaidi kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa watu wa Mataifa, ili waweze kuwa ni nuru ya Mataifa na wokovu hata miisho ya dunia. Mdo 13:14; 43-52. Mitume hawa walifunga safari na kuwaendea watu wa Mataifa na hatimaye, Mtakatifu Paulo akayamimina maisha yake mjini Roma, mfano wa Mchungaji mwema. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa watu wote wa Mataifa bila woga, hata ikibidi kuyasadaka maisha yao. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuanzisha majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; tayari kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kushirikishana tunu na kweli za maisha. Kumbe, kipaumbele cha kwanza ni kusikiliza Neno la Mungu na hivyo kuwa tayari kuwahudumia watu wa Mungu kwa moyo wa unyenyekevu.

Papa Leo XIV Sala ya Malkia wa Mbingu 11. 05. 2025
Papa Leo XIV Sala ya Malkia wa Mbingu 11. 05. 2025   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 11 Mei 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amegusia madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, iliyomalizika tarehe 8 Mei, kwa kurejea maneno ya Papa Francisko aliyekaza kusema, vita isitokee tena ulimwenguni. Papa ameonesha masikitiko yake kutokana na mateso kwa watu wa Mungu nchini Ukraine, huku akiombea amani ya kudumu na kwamba, mateka wa vita waachiliwe huru na watoto waweze kurejea tena kwenye familia zao. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka watu wa Mungu wote wanaoteseka kutokana na madhara ya vita chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Mateka na wafungwa wa vita kule Ukanda wa Gaza waachilewe huru na kwamba, amefurahia kusikia kwamba, India na Pakistani wameamua kupatana na kuanza kujikita katika majadiliano, ili amani ya kudumu iweze kupatikana. Mwishoni, amewasalimu mahujaji na wageni waliofika Roma.

Papa Leo XIV akisali kwenye Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican
Papa Leo XIV akisali kwenye Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, akiwa ameambatana na viongozi wakuu wa Vatican, alifungua Jumba la Kitume, lililokuwa limefungwa tangu tarehe 21 Aprili 2025 kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Francisko

Papa Leo XIV Misa
12 Mei 2025, 14:42