ĐÓMAPµĽş˝

Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko nchini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko nchini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  

Papa Leo XIV: Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema! Sifa Za Mchungaji Mwema

Papa Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Roma dominika ya Yesu Mchungaji mwema kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko nchini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika, tarehe 11 Mei 2025 ametaja sifa za mchungaji mwema ni kwamba: anawafahamu na kuwapenda kondoo wake na kwamba, anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani yananogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini: Zawadi ya maisha kwa ukarimu. Hayati Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa tarehe 11 Mei 2025 anasema, wito ni zawadi ya thamani ambayo Mungu hupanda mioyoni, wito wa kutoka ndani ya nafsi yako ili kuanza safari ya upendo na huduma. Anawaalika waamini kuwa ni mahujaji wa matumaini kwa kusadaka maisha yao kwa ukarimu na kwamba, maisha ya wakfu ni alama ya matumaini ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuyapandikiza miongoni mwa watoto wake. Ukosefu wa fursa za ajira na tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kimaadili pamoja na mkanganyiko wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; ukosefu wa haki msingi za binadamu, uchoyo na ubinafsi pamoja na vita ni mambo yanayotishia maisha mema na adili, ndiyo maana waamini wanaitwa na kutumwa kama mahujaji wa matumaini.

Dominika ya Mchungaji Mwema: Siku ya 62 ya Kuombea Miito
Dominika ya Mchungaji Mwema: Siku ya 62 ya Kuombea Miito   (AFP or licensors)

Waamini, lakini zaidi viongozi wa Kanisa wanaalikwa kupokea, kufanya mang’amuzi na kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya katika safari ya maisha yao ya wito na kwamba, vijana wanahamasishwa kuwa ni wadau wanaoshirikiana na Roho Mtakatifu, anayeamsha ndani mwao ile kiu ya kutaka kusadaka maisha yao kama zawadi ya upendo. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wa kizazi kipya kuiga mfano wa vijana watakatifu kama vile: Mtakatifu Rosa wa Lima, Mtakatifu Dominiko Savio, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Mtakatifu Gabrieli, bila kuwasahau wenyeheri Carlo Acutis na Pier Giorgio Frassati wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu wakati wowote kuanzia sasa. Wawe wasikivu wa Neno la Mungu. Wito na Utume ni sawa na chanda na pete kwani ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa; miito inayorutubishwa kwa uaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu, sala, mang’amuzi pamoja na huduma ya upendo na kwa njia ya sadaka yenye furaha, vijana wa kizazi kipya wanaweza kuwa kweli ni mitume wamisionari wa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Maelfu ya watu waliohudhuria Sala ya Malkia wa Mbingu 11.5.2025
Maelfu ya watu waliohudhuria Sala ya Malkia wa Mbingu 11.5.2025

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wa kizazi kipya kufanya mang’amuzi yanayopata chimbuko lake kutoka katika historia ya maisha yao, tayari kutoa jibu makini kwa wito Mtakatifu, lakini zaidi kwa kusikiliza sauti ya Mungu pamoja na sauti ya maskini wanaowazunguka. Hawa ni wale watu wanaojisikia kusukumizwa pembezoni, ni watu waliojeruhiwa na kutengwa na kwamba, kwa namna ya pekee waamini walei wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa mwanga na chachu ya Ufalme wa Mungu kwa njia ya huduma na taaluma zao. Wadau wa miito mitakatifu wanapaswa kuwa ni wasindikizaji wa maisha ya kiroho kwa vijana huku wakijikita katika matumaini na uvumilivu. Vijana wajenge ndani mwao utamaduni wa kusikiliza kwa makini; wawe wakarimu, tayari kusoma alama za nyakati katika safari yao ya maisha ya kiroho. Waamini wajenge utamaduni wa kukoleza miito mitakatifu katika medani mbalimbali za maisha, ili vijana waweze kutambua miito yao. Mama Kanisa anawahitaji viongozi, wamisionari, watu wa ndoa pamoja na watawa, wanaoweza kujibu “Ndiyo” kwa imani na matumaini.  Wito unakuwa na kuchanua katika jumuiya za waaamini; watu wanaoamini, wanaopenda na kutumainia; kumbe, kusali kwa ajili ya kuombea Miito Mtakatifu ni kwa ajili ya Kanisa zima. Walimwengu wanahitaji vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini; watu wanaoweza kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wakovu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu yanayobubujika kutoka katika furaha ya Injili. Kamwe waamini wasichoke kumwomba Bwana wa mavuno ili apeleke watenda kazi, wema, watakatifu na wasikivu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha. Mwishoni mwa ujumbe wake, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawakabidhi vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa na miito yote.

Papa Leo XIV akitoa baraka yake ya kwanza 11.05.2025
Papa Leo XIV akitoa baraka yake ya kwanza 11.05.2025   (AFP or licensors)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa Bendi za Muziki na Wasanii, kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Leo XIV ameanza utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa kusali Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko nchini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye alipata fursa ya kusali kwa kitambo kwenye Makaburi haya. Katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika, tarehe 11 Mei 2025 ametaja sifa za mchungaji mwema ni kwamba: anawafahamu na kuwapenda kondoo wake na kwamba, anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Rej Yn 10: 1-22. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wanamuziki na wasanii wanaoendelea kuipamba siku kuu ya Kristo Mchungaji mwema. Kristo Yesu na kwa njia ya Roho Mtakatifu, analiongoza Kanisa lake, kama Mchungaji mkuu, Katika Injili, Kristo Yesu anasema, anawafahamu kondoo wake nao wanaisikiliza sauti yake na wanamfuata Rej Yn 20: 27. Hii ni changamoto kwa waamini kujibu ukarimu huu kwa upendo wa dhati.

Papa Leo XIV akiangalia umati mkubwa watu wa Mungu
Papa Leo XIV akiangalia umati mkubwa watu wa Mungu

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa mara ya kwanza, anayo furaha kubwa kuweza kuungana na watu wa Mungu kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hususan wito wa utawa na upadre. Amewataka waamini kujenga utamaduni wa: ukarimu, kusikiliza kwa makini pamoja kuwatia shime vijana wa kizazi kipya katika safari ya maisha ya miito yao mbalimbali, ili hatimaye, waweze kupata mifano ya waamini ambao kwa hakika ni mashuhuda waaminifu na wakarimu kwa Mungu na jirani zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini katika maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani, kuupokea wito wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko wa kuwasindikiza vijana katika safari ya mang’amuzi ya miito yao. Waamini wasali na kuombeana “nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.” Rej. Yer 3:15. Waamini wajenge utamaduni wa kusaidiana na watembee katika upendo na ukweli. Bikira Maria aliyesadaka maisha yake kama jibu makini kutoka kwa Mwenyezi Mungu, awasindikize waamini katika wito wa kumfuasa Kristo Yesu.

Sala ya Malkia wa Mbingu

 

 

11 Mei 2025, 15:19