ÐÓMAPµ¼º½

Papa Leo XIV na Salamu Malkia wa kwanza 11 Mei 2025. Papa Leo XIV na Salamu Malkia wa kwanza 11 Mei 2025.  (ANSA)

Papa Leo XIV azungumza kwa simu na rais Zelensky wa Ukraine

Papa Leo XIV na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walizungumza kwa njia ya simu kufuatia ombi la Papa:"kwamba kila juhudi ifanyike" kwa ajili ya amani ya muda mrefu na ya kudumu nchini Ukraine na kwamba watoto wote warejeshwe katika familia zao.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Papa Leo XIV na Rais wa Ukraine Zelensky walizungumza kwa njia ya simu, kwa mujibu wa Msemaji wa Ofisi ya Vyombo  ya habari  vya Vatican  Matteo Bruni. Simu hiyo ilifuatia ombi la Papa kwa ajili ya amani nchini Ukraine wakati wa hotuba yake katika Sala ya Malkia wa Mbingu Dominika tarehe 11 Mei 2025 aliyotoa kwa mara ya kwanza akiwa katikati ya dirisha la Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Wito kwa ajili ya  amani ya kweli, ya haki na ya kudumu kwa watu wapendwa wa Kiukreni

Wakati wa matamshi yake, alisema: "Ninabeba moyoni mwangu mateso ya watu wapendwa wa Ukraine," akihimiza kwamba: "kila juhudi zifanywe kufikia amani ya kweli, ya haki, na ya kudumu haraka iwezekanavyo." Papa aliendelea kusema kuwa "Wafungwa wote waachiliwe, na watoto warudishwe kwa familia zao," Papa alikuwa amekumbusha mnamo tarehe  tarehe 8 Mei 2025, siku ya kuchaguliwa kwake kwamba:  "janga kubwa la Vita vya Pili vya Ulimwengu" lilifikia mwisho mwa miaka 80 mapema, baada ya kusababisha vifo vya milioni 60." Kisha alitoa wito kwamba kusiwe na vita tena, akitoa wito maalum kwa ajili ya Ukraine, Gaza na kwenye mpaka wa India na Pakistani.

Rais Zelensky: 'Tunathamini sana maneno yake'

Kufuatia mazungumzo na Papa, Rais Zelensky alichapisha kwenye X kuhusu mazungumzo yake ya kwanza na Papa Leo XIV, akisema anamshukuru Papa kwa msaada wake kwa Ukraine. "Tunathamini sana maneno yake kuhusu hitaji la kupata amani ya haki na ya kudumu kwa nchi yetu na kuachiliwa kwa wafungwa," Rais wa Ukraine alisema, akiongeza pia walijadili "maelfu ya watoto wa Ukraine waliofukuzwa na Urusi." Rais alisisitiza, Ukraine, inategemea usaidizi wa Vatican katika kuwaleta nyumbani kwa familia zao. Aidha, alisema alimfahamisha Papa kuhusu "makubaliano kati ya Ukraine na washirika wetu kwamba, kuanzia leo, usitishaji vita kamili na usio na masharti kwa angalau siku 30 lazima uanze."

Kutaka vita iishe

Rais wa Ukraine aliongeza kuwa alithibitisha tena "utayari wa Ukraine kwa mazungumzo zaidi katika muundo wowote, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya moja kwa moja." Kwa mtazamo huu, alisema, "Ukraine inataka kumaliza vita hivi na inafanya kila kitu kufikia hilo," na kwamba Ukraine "inasubiri hatua sawa na Urusi." Rais Zelensky alibainisha kuwa amemwalika Papa Leo XIV kufanya Safari ya Kitume nchini Ukraine, akisema ziara hiyo "italeta matumaini ya kweli kwa waumini wote na watu wetu wote." "Tulikubaliana kuendelea kuwasiliana na kupanga mkutano wa ana kwa ana katika siku za usoni," alisema.

Papa Leo XIV na Zelensiky
14 Mei 2025, 10:26