MAP

Papa Leo XIV akisali mbele ya Kaburi la Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Mei 2025 Papa Leo XIV akisali mbele ya Kaburi la Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Mei 2025 

Papa Leo XIV Atembelea na Kusali Kwenye Kaburi la Papa Francisko

Papa Leo XIV, akiwa njiani kurejea kutoka kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mama wa Shauri Jema, alipitia kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, ili kutoa heshima zake sanjari na kusali kwenye Kaburi la Hayati Baba Mtakatifu Francisko, aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka 21 Aprili 2025. Amepata nafasi ya kusalimiana na waamini waliokuwa Kanisani hapo! Itakumbukwa kwamba, Papa Francisko alifariki dunia Jumatatu ya Pasaka tarehe 21 Aprili 2025

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo wa XIV, Jumamosi tarehe 10 Mei 2025 aliianza siku kwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Makardinali kwanza kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa waliyotenda tangu alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 21 Mei 2025 na kwamba, Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; kumbe, waendelee kulipenda na kuliombea Kanisa pamoja na kumuunga mkono Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa sala na kazi zao njema. Ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza: Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, pamoja na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia ambaye pia ni “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki; Kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbalimbali na kwa wakati huu, ni kifo cha Papa Francisko.

Kaburi la Papa Francisko
Kaburi la Papa Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Leo XIV amewakumbusha Makardinali kwamba, Kristo Yesu Mfufuka anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kwamba, viongozi wa Kanisa waendelee kuwasaidia watu wa Mungu kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao na kwamba, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican utaendelea kuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo: Kipaumbele cha kwanza ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka, Wongofu wa kimisionari kwa waamini wote; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Kimisionari na sanjari na Urika wa Maaskofu; Kwa sababu Mwenyezi Mungu huwajalia waamini wote silika ya imani “Sensus fidei” inayowasaidia kupambanua kile kilicho kweli cha Mungu sanjari na Ibada; Upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kukuza na hatimaye, kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene.

Papa Leo XIV tarehe 10 Mei 2025 amekutana na kuzungumza na Makardinali
Papa Leo XIV tarehe 10 Mei 2025 amekutana na kuzungumza na Makardinali   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo wa XIV anasema, Kanisa litaendelea kujizatiti kutafuta ukweli, haki, amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Papa Leo XIII; “Rerum Novarum.” Alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili. Aligusia haki msingi za wafanyakazi, mshahara na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki wa binafsi wa mali; wajibu wa Serikali, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Leo XIII alizivalia njuga changamoto zilizojitokeza wakati wa Mapinduzi ya Viwanda Barani Ulaya. Katika Ulimwengu mamboleo, Mama Kanisa anataka kutumia amana na utajiri wake kukabiliana na changamoto ya teknolojia ya akili unde, ili hatimaye, kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; haki na fursa za ajira. Ni matumaini yake, kwamba, uongozi wake kama Papa Leo XIV utakuwa kama mwanga unaopyaisha imani, mapendo sanjari na kuimarisha ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baada ya sehemu hii ya kwanza ya hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV walianza awamu ya pili ya mkutano wao kwa faragha ili kusikiliza: Ushauri, Mapendekezo na Mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika uhalisia wake: Mambo mengine tayari yalikwisha kujadiliwa kwenye Mikutano elekezi ya Baraza la Makardinali.

Papa Leo XIV akisali kwenye Madhabahu ya B. Maria Mama wa Shauri Jema
Papa Leo XIV akisali kwenye Madhabahu ya B. Maria Mama wa Shauri Jema   (ANSA)

Papa Leo XIV Jumamosi jioni, tarehe 10 Mei 2025 ametembelea Madhabahu ya Bikira Maria Mama wa Shauri Jema, huko Genazzano. Haya ni Madhabhu yaliyoanzishwa na Shirika la Waagostiniani na hapa kunahifadhiwa kumbukumbu ya Papa Leo wa XIII. Ametumia fursa hii kusali pamoja na waamini waliokuwepo mahali hapo. Lengo kuu ni kutoa maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo, kwa kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Shauri Jema, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Amewataka vijana waliokuwepo kumfuasa Kristo Yesu kwa mfano wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Papa Leo XIV, akiwa njiani kurejea kutoka kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mama wa Shauri Jema, alipitia kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, ili kutoa heshima zake sanjari na kusali kwenye Kaburi la Hayati Baba Mtakatifu Francisko, aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka tarehe 21 Aprili 2025. Amepata nafasi ya kusalimiana na waamini waliokuwa Kanisani hapo!

Papa Francisko
11 Mei 2025, 14:43