杏MAP导航

Tafuta

2025.05.26 PAPA LEO XIV KATIKA KANISA KUU LA MTAKATIFU PETRO KWA  JUBILEI YA AFRIKA 2025.05.26 PAPA LEO XIV KATIKA KANISA KUU LA MTAKATIFU PETRO KWA JUBILEI YA AFRIKA 

Papa katika Hija ya Jubilei ya Bara la Afrika:Kuweni Ishara za Matumaini Ulimwenguni

Jumatatu tarehe 26 Mei 2025 alasiri,Baba Mtakatifu Leo XIV,aliwashangaza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro washiriki wa Ibada ya Hija ya Jubilei kwa ajili ya Amani Barani Afrika,mabalozi wa Afrika wenye utambulisho wa nchi zao mjini Vatican na Italia wakisindikizana na ndugu na jamaa zao mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Turkson.Papa alisisitiza ushuhuda mkubwa ambao bara la Afrika linatoa kwa ulimwengu mzima.

Vatican News

Mwaka huu Mtakatifu unawaalika wabatizwa wote kutafuta matumaini, lakini pia kuwa ishara za matumaini kwa binadamu. Na kwa maana hii, bara la Afrika linaupatia ulimwengu mzima ushuhuda mkubwa. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV alivyowaelekea washiriki wa hija ya Jubilei kwa ajili ya amani Barani Afrika kwa mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican na Italia, waliokutana nao kwa mshangao katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa alasiri Jumatatu tarehe 26 Mei 2025, na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Kansela wa Taasisi ya  Kipapa cha Sayansi na Taasisis ya  Kipapa cha Sayansi Jamii, akishirikiana na Kardinali Francis Arinze, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, pamoja na Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji.

Kutembea pamoja, umoja, katika huduma ya wengine

Akiongea kwa lugha ya Kiingereza, Baba Mtakatifu  Leo XIV alianza kwa salamu: "Habari za mchana kwa wote, hasa wawakilishi. Mnaweza kukaa, lakini mimi nitasimama. Nimekuja kwa ufupi tu kuwasalimu ninyi nyote na kuwakaribisha Roma, Vatican, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, na kujumuika nanyi kwa ufupi sana katika hija hii ya Jubilei katika Mwaka huu Mtakatifu, mwaka unaotutia moyo na kutualika sote kutazama matumaini, lakini pia kuwa ishara za matumaini."

Papa aliongeza: "Ni jinsi gani ilivyo muhimu  kwamba kila mtu aliyebatizwa ajisikie kuwa ameitwa na Mungu kuwa ishara ya tumaini katika ulimwengu wa leo. Imani yetu ndiyo inatupatia nguvu. Ni imani yetu inayotuwezesha kuona nuru ya Yesu Kristo katika maisha yetu na kuelewa jinsi ilivyo muhimu kuishi imani yetu.  Si Dominika tu, si wakati wa hija tu, bali kila siku ili tujazwe na tumaini ambalo ni Yesu Kristo pekee awezaye kutupatia na kwamba sisi sote kwa pamoja tutaendelea kutembea kwa umoja kama kaka na dada kumsifu Mungu wetu; kutambua kwamba kila kitu tulicho nacho na kila kitu jinsi tulivyo ni zawadi kutoka kwa Mungu, na kuweka karama hizo kwa huduma ya wengine."

Asante kwa kuishi imani yenu katika Kristo

Papa Leo XIV kwa hiyo aliwasalimia mabalozi, washirika wao na wanafamilia wote, akiwashukuru kwa kuishi imani yao katika Yesu Kristo: Ninayo furaha sana kuweza kuwasalimu nyote kwa muda mfupi sana mchana huu, lakini kuwaambia kila mmoja wenu: Asante kwa kuishi maisha yenu, imani yenu katika Yesu Kristo. Tayari mmesindikizwa vyema na Waheshimiwa wenu, Kardinali Turkson, Kardinali Arinze, pamoja na Askofu Mkuu Fortunatus, na sisi sote kwa pamoja, tukiwa tumejazwa na ushuhuda mkuu ambao wote mnautoa na ambao Bara la Afrika linautolea ulimwengu mzima. Tunasema, “Asante, Bwana Yesu, na jina lako lihimidiwe.” Mungu awabariki nyote. Kwa njia hiyo  ninamalizia kwa baraka. Bwana awe nanyi. Mungu Mwenyezi awabariki, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Amina. Amani ya Mungu iwe nanyi daima," alihitimisha.

Kauli mbiu ya hija ya Jubilei yao ilikuwa ni:  “Tumaini la Amani Barani Afrika”, na iliandaliwa katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kimataifa ya Afrika, iadhimishwayo kila ifikapo tarehe 25 Mei ya kila mwaka. Hafla hiyo ilihudhuriwa na takriban watu mia tano.

 

26 Mei 2025, 19:38